Misukosuko, msisimko wa safari ya kufika kileleni Kilimanjaro -2

Moshi. “Unatokea Tanzania? Mlima Kilimanjaro ukoje? Umewahi kupanda? Napanga kuja siku moja nasikia ni uzoefu mzuri, hata picha za mtandao nilizoziona zinavutia.”

Ni kauli ya binti wa Kizulu niliyekutana naye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Doha, nchini Qatar, Juni, 2023.

Haikuwa mara ya kwanza kuulizwa na wageni ninaokutana nao ughaibuni kuhusu Mlima Kilimanjaro, ambao ni moja ya vivutio vya utalii nchini Tanzania.

Mlima huu nimekuwa nikiuona pichani, mara moja mwaka 2018 niliushuhudia nikiwa angani niliposafiri kwa ndege kuelekea jijini Mwanza kupita Kilimanjaro.

Mzulu niliyekutana naye Doha, kwao ni jimbo la Port Elizabeth, Afrika Kusini. Miezi mitano tangu tulipokutana nilipata safari ya kikazi Cape Town, nchini humo tukawasiliana.

Hakuwa nchini humo, lakini aliniambia nisiondoke Cape Town bila kupanda mlima maarufu uliopo hapo, Table Mountain. Nilikutana na Mzulu mwingine (Duduzile) alinishawishi kuupanda nikakubali.

Kilele cha mlima huo kipo urefu wa mita 1,086. Unaweza kupanda kwa gari la waya au kutembea, Duduzile alinitembeza. Nilichoka lakini nilifurahi baada ya saa 12 za kupanda na kushuka nikiwa hoi, wakati yeye ni kama alikuwa ametoka matembezi.

Alinieleza ana mpango wa kupanda Mlima Kilimanjaro, nikapata shauku nikapanga safari, huku baadhi ya marafiki na ndugu zangu wakinizuia.

“Ni hatari kwenda huko, nilipoteza rafiki yangu kwa kuporomokewa na barafu,” alinieleza kaka yangu mkubwa niliyemshawishi tuungane kupanda mlima huo.

“Unafuata nini huko, ni lazima uende? Kuna mengi ya kufurahia duniani siyo kupanda milima,” aliniambia kaka yangu mwingine.

Dada yangu pekee nilipompa taarifa alisema: “Ila babu una hatari wewe, haya!”

Mke wangu alinitumia video ya watu wakishushwa mlimani kwa machela akaniambia: “Uwe makini familia bado inakupenda na kukuhitaji.”

Binti yangu haelewi chochote aliomba zawadi ya pipi. Ushauri ulikuwa mwingi, lakini nilikuwa nimefikia uamuzi. Kutokana na hofu sikuwaaga wazazi wangu, niliamua nitawatumia picha.

Niliwaaga wapendwa wangu nikaanza safari kuelekea mkoani Kilimanjaro. Njiani basi nililopanda liligonga bodaboda eneo la Same, tukakaa kituoni muda mrefu, Moshi niliingia saa 10:00 alfajiri.

Safari ya kupanda mlima ilitakiwa kuanza baadaye siku hiyo, hivyo nilitafuta eneo nikalala muda huo ikiwa saa 11:00 asubuhi. Saa moja asubuhi mwenyeji wangu alinipigia simu ili kuanza safari ya kwenda Marangu, niliomba saa moja zaidi ya kulala.

Saa 2:00 asubuhi nilikwenda Marangu ambako baada ya kukamilisha taratibu na kupatiwa vifaa nilitambulishwa kwa watu watano ambao ningeambatana nao safarini.

Nilipiga picha kadhaa getini nikazituma kwenye mtandao wa kijamii. Tukapima uzito mabegi, safari ikaanza saa saba mchana. Watatu walipita njia yao, mimi na aliyeniongoza tukapita yetu.

Begi langu lilikuwa na uzito wa kilo nane, nilivaa viatu vya kupandia milima, suruali nyepesi na fulana ya mikono mifupi, hali ya hewa ilikuwa shwari.

Tulikatiza msitu wenye miti mingi ya asili, muda wote sauti za ndege na miti inayogongana au matawi kuanguka ndiyo sauti iliyosikika.

Kwa kuwa ilikuwa Desemba, dakika 20 baada ya safari kuanza mvua ilinyesha kukawa na utelezi. Takribani muda wote wa safari siku ya kwanza kulikuwa na mvua. Nilivaa jaketi la mvua, lakini kuanzia magotini kwenda chini nililowa.

Saa tisa alasiri tulipata chakula. Kituo cha kwanza (Mandara) tulifika saa 11:00 jioni. Siku hii nilitembea hatua 15,182, umbali wa kilomita nane.

Njiani mwongoza watalii aliniuliza iwapo nilifanya mazoezi kabla ya kupanda mlima. Niliitikia ndiyo, lakini ulikuwa uongo. Siku moja kabla ya safari nilitoka klabu alfajiri.

Si kwamba sifanyi mazoezi, isipokuwa kila ninapopanga kufanya hivyo sikosi sababu. Nimewahi kulipia ‘gym’ mara mbili ila sijawahi kufika hata siku moja.

Kilichonifanya nijiamini ni uzoefu wa kupanda na kushuka Table Mountain kwa siku moja, wakati sikuwa na mazoezi. Pia niliamini kuna muda nitalala hivyo siwezi kushindwa.

Nilipumzika takribani mara nne kabla ya kufika Mandara ambako nilipiga picha ya kumbukumbu, kwani baadhi ya watu hapo ni kituo chao cha mwisho.

Nilikunywa chai na karanga. Siku hiyo tulilala hapo wote watano, nikaelekezwa kazi ya kila mmoja. Kuna mpishi, mbeba mizigo, mhudumu, mbeba maji na mwingine chakula ambacho tutakula siku zote tutakazokuwa mlimani. Walikuwa wakarimu.

Aliyeniongoza alisisitiza nilale mapema, akisema siku inayofuata safari ni ndefu. Hata hivyo, sikutii kulikuwa na Wi-Fi ya bure kwa dakika 30, baada ya hapo unatakiwa kulipa Sh25,000 kwa siku.

Nilielekezwa eneo la kupata mtandao wa simu ninaotumia, nilisimama kwa saa kadhaa kufanya mawasiliano nikiwa nimevaa tochi kichwani ili kuona na kuonekana na wenzangu.

Eneo la kulala ni mfano wa bweni, kila mtu na kitanda chake. Niliambiwa hamna kuoga, asubuhi nililetewa maji ya moto ya kunawa, nikanywa chai tukaanza safari.

Umbali kuelekea Horombo ni kilomita 11, muda unaotajwa kufika eneo hilo ni saa tano, lakini nilitumia saa saba. Safari ilianza saa 1:30 asubuhi tukafika Horombo saa nane kasoro mchana.

Kabla ya safari mwongozaji alinipima kiwango cha mzunguko wa hewa ya oksijeni mwilini, akaniambia naweza kuendelea na safari. Nikabeba begi mwendo ukaaanza.

Tofauti na siku ya kwanza, licha ya kuwa uzito ni uleule, nilihisi nimebeba kilo 15. Muda mfupi baada ya kutoka Mandara tuliachana na msitu mnene, tukaingia eneo lenye tabia ya nchi ya yabisi (savana). Hapa kuna nyasi fupi, miti michache na hali ya hewa ni nzito ikilinganishwa na chini.

Nilianza kuingiwa hofu baada ya kuona watu waliobebwa kwenye machela baada ya kuugua wakiwa juu mlimani (mountain sickness).

Machela yenyewe ni toroli lililochongwa kwa chuma, lina tairi moja la pikipiki, waendeshaji hulivuta kutokea mbele, wengine wakisukuma. Pia helikopta hutoa huduma.

Safari siku ya pili na ya tatu

Siku ya pili nilitembea hatua 23,142, safari ya kilomita 11. Ilifika mahali kila baada ya saa moja naomba kupumzika na kunywa maji.

Mpaka kufika Horombo nilikuwa nimechoka sana, njiani mwongozaji alinisaidia kubeba begi ambalo lilikuwa na chakula cha njiani, maji, mwavuli na mavazi ya dharura endapo hali ya hewa itabadilika.

Hali ya hewa katika kituo hiki kilichopo urefu wa mita 3,720 kutoka usawa wa bahari ni hafifu ikilinganishwa na cha Mandara ambacho kipo mita 2,720 juu ya usawa wa bahari.

Horombo nilipewa chai, baadaye maji ya kunawa. Tulikutana watu wengi hapa maana ni kituo cha wanaopanda na kushuka mlima. Asilimia kubwa walikuwa watu wa mataifa ya kigeni.

Siku ya tatu safari ilianza mapema, ni umbali wa kilomita tisa muda unaotajwa kutembea ni saa tano. Nilitumia saa saba kuanzia saa 1:30 asubuhi nilifika Kibo (kituo cha mwisho) saa 7:33 mchana. Nilitembea hatua 14,322, zilizonichosha kwa sababu ya mchanga na mawe.

Kibo ipo kwenye mwinuko wa mita 4,720 kutoka usawa wa bahari. Tabia ya nchini ni mchanganyiko wa wastani na kibara. Kadri unavyokwenda juu baridi inaongezeka oksijeni ikipungua.

Kuanzia Horombo hadi Kibo kuna uoto wa nyasi fupi, baadaye jangwa. Unakatiza katikati ya Mlima Mawezi na Kilimanjaro na hapo mlima unauona vizuri, unaweza kudhani unakikaribia kilele.

Kabla ya kufika Kibo nilipata changamoto ya msuli, nilichua safari ikaendelea. Upepo ulianza kuwa mkali na baridi isiyomithilika.

Kadri unavyozidi kupanda hamu ya kula inapungua. Kwa tabu nilikula zaidi nanasi na magimbi kidogo. Kila siku kulingana na tulipo kulikuwa na mlo wake.

Kibo hali ya hewa si rafiki, oksijeni ni ndogo na baridi ni kali. Nilishtuka kuwaona watu wanatoka mlimani wakiwa wamebebwa na walegevu. Helikopta ya uokozi ilifika kuwasaidia, nikajiona katika hali ile saa chache zijazo.

Mwongozaji alinisihi nilale, kwani usiku huohuo tutaanza safari kuelekea kileleni. Nilihisi kukata tamaa. Usingizi ulikuwa wa tabu, oksijeni ni ndogo. Saa nne usiku niliamshwa kuendelea na safari.

Nimewahi kuishi nchi zenye baridi kali, sikufikiri ingekuwa changamoto kwangu, lakini mwongozaji alisisitiza nifuate anachonielekeza. Nilivaa nguo za kunisitiri na baridi kali, soksi aina tatu, suruali, kichwani mzula na kofia ya koti.

Safari kutoka Kibo kwenda kileleni ilianza, kichwani nilivaa tochi mithili ya wachimbaji mgodini nikiwa na fimbo mbili mkononi.

Tofauti na nilikopita awali, safari ya kilomita sita kufika kileleni ilikuwa ngumu zaidi, muda wa kufika nilielezwa ni saa sita, nilitumia tisa. Eneo lina mwinuko mkali, mawe, miamba, mchanga mwingi, chini barafu.

Baada ya saa mbili za mwanzo niliomba kumpumzika. Mwili ulikuwa umechoka, usingizi mzito na changamoto ya kupumua. Siku hiyo sikubeba chochote, chakula na maji alibeba aliyeniongoza.

Zaidi ya mara tatu kabla ya kufika kituo cha Gilmans nilimweleza anayeniongoza nimeshindwa, naomba nirejee chini au uniache nilale. Kuna wakati alinipa dakika tano za kulala, nikajiegesha kwenye mwamba. Aliniamsha akasema ni hatari kuna wakati udongo au barafu huporomoka.

Ilifika mahali alinikatia tamaa akaniuliza iwapo naweza kuendelea au turudi. Tulikuwa tukipishana mawazo, muda anaosema turudi nakuwa nimepata nguvu kidogo, muda ninaopendekeza turudi ananitia moyo, ananipa maji ninywe.

Kituo cha Gilmans kilichopo mita 5,681 kutoka usawa wa bahari tulifika saa 12:30 asubuhi. Mlimani mapambazuko huwahi, nilikuwa nimechoka sana, akaniambia nikiishia hapo naweza kupewa cheti cha kufika kileleni lakini siyo Uhuru.

Nikaomba kupumzika, baridi iliongezeka, hali ya hewa haikuwa rafiki, upepo wenye theluji ulivuma mithili ya mtu arushaye mchanga. Kwa kuwa kuna mawe makubwa nilijibanza sehemu nikapumzika. Nikamuuliza bado umbali gani akasema kilomita mbili.

Mwinuko ulikuwa umeisha, lakini safari haikuwa rahisi kutokana na barafu, njia haikuwa ikionekana tulifuata nyayo za waliotangulia. 

Njiani nilikaa na kulala kwenye barafu kutokana na usingizi na uchovu, mwongozaji alinionya hilo ni hatari kwa afya, ninaweza kuganda, hivyo ama tuendelee na safari au turudi chini.

Nilikumbuka kila aliyenishauri kuhusu safari, kuna muda nilichungulia makorongo yaliyopo nikaona mauti ikinijia, nilisali na kujipa moyo wa kuendelea.

Safari ya nusu saa kutoka kituo cha Gilmans kwenda Stella nilitumia saa moja. Nilihisi kumkwaza mwongozaji, lakini hakukuwa na namna.

Kutoka Stella kwenda Uhuru ni umbali wa nusu saa, nilitumia saa moja pia, baada ya kusimama mara kadhaa nikijikongoja mithili ya mgonjwa wa miguu nilianza kukiona kilele cha Uhuru.

Nikapata nguvu ya kusonga mbele. Nilifika kileleni saa 2:30 asubuhi. Nilikaa kwenye ubao wa kilele dakika kadhaa nikapiga picha. Kuna wakati nilivua miwani kidogo ili sura ionekane, kesho watu wasije wakasema sikufika.

Miwani kileleni inalinda macho kutokana na miale ya jua inayotokana na kuakisi kwenye barafu. Pia inayalinda kutokana na upepo mkali unaorusha theluji.

Nilimweleza mwongozaji: “Nimetoboa, turudi.” Nikimwangalia usoni naye amechoka, anajikaza.

Tulitembea hadi Gilmans, safari hii changamoto ilikuwa barafu kuteleza, lakini fimbo zilinisaidia. Tulipofika tulipata chakula na maji ambayo yalianza kuganda.

Tulianza safari ya kuteremka, nilikuwa na furaha, nilitamani nifike sehemu yenye mtandao niposti picha. Mwili umechoka, lakini taratibu zinasema nikitoka kileleni lazima nikalale Horombo.

Nilifundishwa kuteleza kwenye mchanga ili safari iende haraka, nilifika Kibo saa saba mchana nikaomba nilale walau kwa saa mbili, kisha niendelee na safari kushuka Horombo. Nililala, tukaendelea na safari tukafika saa nne usiku.

Jumla ya hatua siku hiyo zilikuwa 34,899. Kutokana na uchovu sikuweza hata kutumia ofa ya Wi-Fi ya bure, nililala fofofo nikijua kesho yake safari ni ndefu pengine sawa na hiyo.

Asubuhi niliamshwa, nikapewa maji ya kunawa na kifungua kinywa. Tulianza safari ya Mandara, kisha getini Marangu, ambako tulifika saa 9:00 alasiri.

Baada ya siku tano nikiwa tena Marangu nilijiona kwenye ulimwengu mwingine. Mamlaka ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) ilinitunuku cheti kwa kufika kileleni.

Nilipata chakula cha mchana nikaanza safari kuelekea Moshi ambako nilioga kwa mara ya kwanza baada ya takribani wiki.

Awali, sikujua ukubwa wa jambo hilo, ila baada ya kuchapisha picha zangu mtandaoni nikiwa kilele cha Mlima Kilimanjaro, ujumbe ulioandikwa ulinionyesha ukubwa wake baadhi wakiniita shujaa.

Habari hii imeandikwa kwa udhamini wa Taasisi ya Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts