Museveni atoa kauli Besigye kuendelea kushikiliwa

Rais Yoweri Museveni ameweka wazi msimamo wake kuhusu utata unaozunguka kizuizini kwa Dk Kizza Besigye akisema kuwa swali sahihi siyo kwa nini Dk Besigye alipelekwa rumande, bali ni kwa nini alikamatwa.

“Iwapo unataka nchi yenye utulivu, swali sahihi zaidi linapaswa kuwa: Kwa nini Dk Besigye alikamatwa?” Museveni amesema. “Jibu la hilo ni kesi ya haraka ili ukweli ujulikane.”

Kauli ya Museveni imekuja siku moja tangu Dk Bsigye alipofikishwa hospitali baada ya afya yake kuzorota kufuatia mgomo wake wa kula.

Kwa mujibu wa BBC, kiongozi huyo wa upinzani amesharudishwa tena rumande ya kijeshi.

Dk Besigye alikamatwa Novemba 16, 2024 akiwa jijini Nairobi nchini Kenya na kusafirishwa hadi Uganda ambako amekuwa akishitakiwa kwenye Mahakama ya kijeshi akituhumiwa kukutwa na bastola kinyume cha sheria na kwamba alikuwa na mpango wa kununua silaha nje ya nchi. 

Katika taarifa aliyochapisha kwenye akaunti yake ya X leo Jumanne, Februari 18, 2025, Rais Museveni amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji, hasa kwa wale wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa.

“Hatuko kwa ajili ya kulipiza kisasi, lakini hatari inayotokana na wauaji lazima iondolewe,” amesema.

Ameongeza kuwa, historia ya Uganda imejikita katika maridhiano na msamaha, lakini hilo halipaswi kuja kwa gharama ya uwajibikaji.

Kuhusu afya ya Dk Besigye, Museveni amebainisha kuwa kuna hospitali ya Serikali ndani ya gereza na kwamba madaktari wake binafsi wamekuwa wakimtembelea. Hata hivyo, amesisitiza kuwa mgomo wake wa kula umechangia kudhoofika kwake.

“Je, hiyo si hadaa isiyo na misingi?” Museveni amehoji.

Ameongeza, “Unawezaje kushtakiwa kwa makosa mazito kisha ukajibu kwa mgomo wa kula ili upate huruma na kupewa dhamana? Kwa nini husisitiza kesi kusikilizwa haraka?”

Museveni pia alizungumzia kucheleweshwa kwa kesi ya Dk Besigye, ambayo inapaswa kuhamishwa kutoka mahakama ya kijeshi hadi mahakama ya kiraia.

“Nani aliyekwamisha mchakato wa kesi? Ni Mahakama zenyewe zilizoonyesha kasoro fulani katika Mahakama za Kijeshi na zikatoa agizo la kesi kuhamishiwa Mahakama za Kiraia,” amesema.

Mkewe amtembelea gerezani

Akiandika katika mtandao wa X, mke wa Dk Besigye, Winnie Byanyima amesema alimtembelea mumewe katika chumba chake cha gereza leo Februari 18, 2025.

“Alikuwa amelala kwenye kitanda kidogo ambacho kinachukua urefu wote wa chumba. Rundo la magazeti ya zamani na masanduku mawili ya kadibodi yaliyochakaa vilikuwa pembeni ya kitanda chake, yakiacha nafasi tu ya kigoda kimoja cha kukalia.

“Kulikuwa na takriban milango sita au saba iliyofungwa niliyopitia kabla ya kufika chumbani kwake, ambacho kipo katika korido nyembamba na yenye giza. Mtu mmoja aliniambia kuwa hii ni gereza maalum kwa washukiwa wa ugaidi.

Ilikuwa uchungu sana kumkuta @kizzabesigye1 katika hali ya fedheha kiasi hiki.”

Ameongeza, “Kiiza Besigye ni dhaifu, amepungua uzito kwa kiwango cha kutisha, na anahisi kizunguzungu hajala kwa siku tano. Huu si tu mfungo usio wa kisheria, bali ni utekaji nyara. Nimekasirishwa sana na ninataka @KagutaMuseveni na mwanawe, mkuu wa jeshi, wamuachilie mara moja. Yeye ni raia mwenye haki—kama wao!”

Related Posts