NCCR Mageuzi: Hatuko tayari kuungana na vyama vingine uchaguzi ujao

Dar es Salaam. Chama cha NCCR Mageuzi kimesema hakiko tayari kuungana na chama chochote kwenye uchaguzi mkuu ujao ambao kimethibitisha kitashiriki kikamilifu.

Msimamo huo umekuja baada ya wito wa kuunganisha vyama vya upinzani kwenye uchaguzi ujao, uliotolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi, wiki iliyopita.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, chama hicho kilikuwa miongoni mwa vyama vya upinzani vilivyoungana kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kikiwa pamoja na vyama vingine kama Chadema, CUF, na NLD.

Katika umoja huo, walisimamisha mgombea mmoja katika nafasi za ubunge na udiwani na kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, hayati Edward Lowassa, ili kuikabili Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akitoa msimamo huo leo Jumanne Februari 18, 2025 mbele ya waandishi wa habari, mwenyekiti wa chama hicho, Ambar Haji Khamis, amesema mwaka huu wameamua waende kwenye uchaguzi huo wenyewe na hawataki ushirikiano wowote. “Tunaenda kwenye uchaguzi wa mwaka huu kama chama, yote haya ni kwa sababu hatujasahau maumivu tuliyoyapata katika uchaguzi wa 2015. Kwani baada ya kuungana na wenzetu, walivunja makubaliano tuliyoyafanya kwenye vikao vya ndani wakatunyang’anya majimbo yetu.

Wakati tunaingia kwenye umoja huo, tulikuwa na wabunge wanne, lakini baada ya uchaguzi tukabakia na mbunge mmoja, huku wao wakiongeza idadi ya wabunge wao,” amesema na kuongeza;

“Mfano, Chadema waliokuwa na wabunge 24, wakapata zaidi ya 30, CUF waliokuwa na wabunge wawili, wakapata wabunge 10, hivyo hatutaki kurudia makosa hayo tena,” amesema Khamis.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Ambar Haji Khamis (katikati) wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne Februari 18, 2025.

Akitoa maoni kuhusu msimamo huo wa NCCR Mageuzi, mchambuzi wa masuala ya siasa na mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie, amesema bado muungano wa vyama vya siasa kwa Tanzania ni jambo gumu ukilinganisha na Kenya.

Dk Loisulie amesema hiyo ni kutokana na historia ya uanzishwaji wa vyama hivyo ambapo ametolea mfano wakati vinaanza, NCCR kilikuwa na nguvu enzi hizo, mwenyekiti wake akiwa marehemu Augustino Mrema.

“NCCR ikaja ikafifia, CUF ikachukua nafasi na baadaye Chadema. Hivyo, kutokana na historia hizi, wahusika wanaona hakuna manufaa katika kuungana,” amesema mhadhiri huyo.

Sababu nyingine, mchambuzi huyo amesema ni viongozi wengi wa upinzani kutoaminiana na wengine kwenda mbali kwa kueleza kuna mamluki au kuuita chama fulani CCM B.

 “Pia, suala la sheria zinazosimamia vyama vya siasa, amesema nayo sio rafiki kwa kuviwezesha kuungana, na mwisho wa siku wanaofanya hivyo hujikuta wanakinufaisha chama kilichopo madarakani,” ameongeza.

Ili hayo yawezekane, Dk Loisulie amesema wakati ndio utazungumza ambapo anaamini ipo siku wananchi wataamua wanataka nini, lakini kusema viongozi wa vyama vya upinzani ndio watawezesha hili sio kweli.

Wazungumzia “No Reform, No Election”

Kuhusu kauli ya Chadema ya kuwa “Hakuna uchaguzi bila mabadiliko,” chama hicho kimesema hakiungi mkono msimamo huo na kueleza kuwa watakapoona wenzao hao wanaenda kuleta vurugu kwa msimamo wao huo, hawatasita kutoka mbele kukemea.

“Hakuna kitu kizuri kama kuitunza amani ya nchi yetu. Tunaposema kila mtu ana haki ya kufaidi keki ya taifa, ni pamoja na amani hii tuliyonayo, hivyo hatutakuwa tayari kuona mtu anaiharibu halafu tukakaa kimya.

“Nasema hivi kwa sababu kwa msimamo walionao wenzetu, wamekuwa wakizungumza mara kwa mara, ni wazi kwamba huenda wakaingia barabarani kama wanalolitaka halitatekelezwa,” amesema mwenyekiti huyo.

Katika mkutano huo, Khamis pia amezungumzia chama chao kufanya uchaguzi Aprili mwaka huu. Katika uchaguzi huo, utakaofanyika ndani ya mwezi mmoja, amesema watachagua viongozi mbalimbali wakiwemo wa kitaifa na tayari katika ngazi za shina na tawi mchakato huo umeshaanza.

 “Kama mlivyoona, vyama vya wenzetu wameshafanya chaguzi zao, sisi ilikuwa bado kutokana na sintofahamu tulizopitia hapo katikati na kukosekana kwa fedha, lakini pamoja na ukata wetu huu, tunaenda kuufanya hivyohivyo kwa michango ya wanachama na ile ya wadau,” amesema kiongozi huyo.

Aidha, katika mkutano mkuu huo, pamoja na uchaguzi, amesema watautumia kupitisha mabadiliko madogo ya katiba waliyoyafanya Septemba 2022, jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine, iliweka ukomo wa kuwepo madarakani kwa mwenyekiti wa chama.

Katika ukomo huo, Khamis amesema iliamuliwa mwenyekiti awe madarakani kwa miaka 10 pekee na si vinginevyo, hata kama mwenyekiti husika anapendwa kiasi gani.

Related Posts