Tanga. Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko amewataka wanawake na wananchi wengine kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la mpigakura, kabla ya zoezi hilo kufungwa kesho, Februari 19, 2025.
Ombi hilo amelitoa leo, Februari 18, 2025, wakati wa ziara yake ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kuboresha taarifa zao ili waweze kutimiza haki yao ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ikiwemo uchaguzi wa Rais, madiwani na wabunge.
Sekiboko amesema kuwa kitambulisho cha mpigakura ni muhimu kwa kila mwananchi ili apate haki ya kuchagua viongozi wanaowataka na kuongeza kwamba kama mtu hakuboresha taarifa zake, inaweza kumzuia kutekeleza haki yake ya kupiga kura.
“Tukiboresha taarifa zetu katika daftari la mpiga kura, itatusaidia kumchagua Rais, ambaye tayari chama chetu, CCM, kimeshampitisha mgombea pekee wa kiti cha urais.”
Mbunge huyo amefanya uhamasishaji katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Tanga, ikiwa ni pamoja na Pangani, Handeni, na Kilindi na anatarajia kumalizia ziara yake Lushoto.

Zoezi la kuboresha taarifa katika daftari la kudumu la mpigakura lilianza Februari 13, 2025 na linatarajiwa kumalizika kesho Februari 19, mwaka huu.
Mwajuma Sempule ni Diwani wa Kata ya Kwediboma wilayani Kilindi amesema kwenye kata yake mwitikio wa wananchi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ni mkubwa nakwamba wanawake wanaongoza kujitokeza.
Katibu wa CCM Wilaya ya Handeni, Mayasa Kimbau amemshukuru mbunge huyo kwa kufika Handeni kuongeza nguvu ya watu kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari hilo.