Serikali kuzibana SImba, Yanga ishu ya viwanja

Serikali imepanga kutoa maelekezo kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu zikiwemo Simba na Yanga kuwa na viwanja vyao vitakavyotumika kwa mechi za mashindano kwa sababu miundombinu ni uti wa mgongo wa michezo nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita jana jijini Dodoma.

“Kwa Yanga na Simba sio ushauri tu tuna mpango wa kuja kutoa maelekezo sio tu kwa timu za Yanga na Simba tu. Tunakoelekea nadhani tutatoa muda kwa vilabu vyote vinavyoshiriki ligi kuu ni vizuri wakawa na viwanja vyao.

“Kwa hiyo tunawapa muda wa matazamio, tutakaa nao, tutazungumza nao, Serikali itatoa maelekezo sasa ifike mahali vikawa na viwanja vyao. Tumeshasema back born (uti wa mgongo) ni miundombinu sasa kwa klabu kubwa kama hizi uhakika hawashindwi kujenga,”amesema Msitha.

Amesema ni suala la msukumo na kuwa kabla ya kulifanya watakaa na kuzungumza nao kisha Serikali itakuja na taarifa kwa sababu wanaweza kufanya hivyo na watakapotaka usaidizi watawapa.

Kuhusu mabadiliko ya timu za Yanga na Simba alisema hakuna kinachokwamisha bali isipokuwa kuna mchakato unaoendelea kwa sababu ni jambo jipya ambalo linahitaji uzoefu kwa hiyo limeshindwa kufanyika kwa haraka.

“Makosa kadhaa yamekuwa yakifanyika kila tukienda kukutana ili kufikia makubaliano hivyo ni matarajio yetu kwamba  yatakwenda kukamilika si muda mrefu na ikumbuke kuwa haya mabadiliko yanahusisha taasisi tofauti.

“Kwa sasa tumekaa pamoja na taasisi zote na tumekubaliana. Tumeona maeneo gani yaliyokuwa yanakwamisha na tukawapa vilabu na tayari wanafanyia kazi. Na kwa sababu si vilabu vya watu binafsi bali vya wananchi vinahitaji umakini,”amesema Msitha.

Kwa upande wa kukaa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kuimarisha viwanja vinavyomilikiwa na chama hicho, Neema alisema walishakaa na kuona ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana na katika kuviboresha kwa kutafuta wawekezaji ama kufanya jambo lingine lolote.

Aidha, Neema alisema ipo changamoto katika uwasilishaji wa kalenda na mipango kazi ya vyama vya michezo ambayo inawasaidia na wao kuwaweka katika mipango yao ya maendeleo ya mwaka.

“Tuna changamoto ya kutokuwa na uelewa ama kutowajibika vizuri katika vyama vyetu vya michezo. Hii timu ni kweli tuna taarifa yake (timu ya ngumi ya wanawake) na walishawasilisha taarifa zao kwetu kwamba wanasafiri lakini kabla hata hatujakaa nayo kuzungumza nao tukakuta tayari wameshaenda kuzungumza huko ambako wanadhani kuna msaada ,”alisema.

Neema alisema Serikali inaongeza pale chama kimefanya na kwamba huwezi kutegemea Serikali ikafanya kwa asilimia 100 na kwamba chama kutegemea asilimia 100 uwezeshaji kutoka kwa Serikali hakuna haja ya uwepo wao.

Pia alisema kuwa Serikali itajenga vituo vya mafunzo nchini ambapo mwaka huu wataanza na ujenzi wa kituo cha mafunzo cha michezo ya riadha katika Mkoa wa Manyara.

Alisema uamuzi wa kujenga kituo hicho mkoani humo unatokana na hali ya hewa kuruhusu kwa michezo hiyo na wanamichezo mahiri wa mchezo huo kutoka katika mikoa ya Arusha, Manyara na Dodoma.

Related Posts