Sh78 bilioni kuwainua wakulima, wafugaji

Pemba. Katika kuwakomboa wakulima na wafugaji, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetenga Sh78 bilioni kwa ajili ya mikopo itakayosaidia kukuza shughuli na uchumi wao katika sekta ya kilimo.

Fedha hizo zitatolewa na Benki ya Maendeleo (TADB) kwa kushirikiana na Shirika la Heifer International Tanzania.

Akitoa ufafanuzi juu ya mikopo kupitia benki hiyo leo Februari 18, 2025 katika ofisi za kilimo Chamangwe, Pemba, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Heifer International Tanzania, Mark Tsove amesema mikopo hiyo itatolewa kupitia vikundi hadi kwa mkulima au mfugaji mmoja-mmoja lakini ni vyema wakajiunga katika vikundi vya ushirika kwani itakuwa rahisi kupata mikopo hiyo.

Amesema wakati wafugaji watapokuwa katika vikundi, benki hiyo inatoa kipaumbele cha kutoa mikopo hata kwa mtu mmojammoja lakini ahakikishe anakuwa kwenye kikundi.

“Tumetenga kiwango hicho cha fedha kwa lengo la kuwainua wafugaji. Mikopo hii itaangalia zaidi wafugaji waliojiunga kwenye vikundi vya ushirika, tunaomba ambao hawajajiunga wafanye hivyo,” amesema.

Ofisa biashara kutoka shirika hilo, Wema Chuwa  amesema mradi huo unatekelezwa nchini na tayari wametoa mafunzo ya ufugaji na elimu ya biashara ya maziwa kwa wafugaji 1,500 wa Unguja na 786 wa Pemba.

“Kwa sasa wakulima na wafugaji hawana budi kuchangamkia fursa ili kujiendeleza zaidi katika kufuatilia mikopo hiyo itakayowawezesha kujiendesha kimaisha,” amesema.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis amesema wizara itaendelea kushirikiana na wadau kuinua juhudi za wakulima na wafugaji katika kuleta mabadiliko makubwa kiuchumi kupitia sekta hiyo.

“Kutokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na mashirika mbalimbali wakulima watapiga hatua kubwa kimaendeleo, kikubwa kwao ni kuongeza juhudi katika kazi zao,” amesema.

Mmoja wa wakulima waliopatiwa mafunzo hayo, Ame Ameir amesema mpango huo utawakaomboa wakulima na wafugaji ambao awali walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea.

Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hamad Hassan Chande amewataka wakulima na wafugaji kuhakikisha wanachangamkia fursa zinazokuja kutoka serikalini na wadau ili kujikwamua katika shughuli zao.

Related Posts