Simu, runinga hatari kwa watoto wa umri huu

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa sasa, matumizi ya simu za mkononi na vifaa vingine vya kiteknolojia kama vile televisheni yanaendelea kuongezeka.

Hali hiyo imesababisha matumizi ya vifaa hivyo kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku, kwa kuwezesha watu kujifunza, kupata habari na hata kuburudika.

Kutokana na faida zake lukuki katika dunia ya sasa, matumizi ya vifaa hivyo kwa sasa yamevunja mnyororo wa rika, kwani watoto wadogo, vijana hata wazee wamekuwa wakitumia katika shughuli mbalimbali.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Watoto Duniani (Unicef) mwaka 2022 ulionyesha kuwa watoto 67 kati ya 100 wenye miaka 12-17, wanatumia bidhaa za mawasiliano ikiwemo simu janja, kompyuta mpakato na runinga.

Hata hivyo,wataalamu mbalimbali wa afya wanataadharisha matumizi ya muda mrefu ya vifaa hivyo kwa watoto kutokana na madhara yanayoweza kujitokeza hapo baadaye, huku wakasisitiza matumizi hayo yaendane na umri wa mtoto husika.

Mwana saikolojia, Modesta Kimonga anaeleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa matumizi ya vifaa hivyo kwa muda mrefu, yanapunguza uwezo wa ubongo kufanya kazi yake vyema na hilo sio kwa mtoto pekee bali hata mtu mzima.

“Ninashauri kwa ustawi wa afya ya ubongo wako ni vyema kuepuka matumizi ya vifaa hivyo kwa muda mrefu na hakikisha unapata mapumziko “

Kwa upande wa watoto, miongozo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) inabainisha kuwa  mtoto wa chini ya miaka miwili,  haruhusiwi kabisa kuangalia televisheni au kutumia vifaa kama vile kompyuta mpakato, vishkwambi na vinginevyo

 “Kuanzia miaka mitano na kuendelea muda wa mtoto kutumia vifaa hivyo unaweza kuongezwa taratibu kadri anavyozidi kukua, lakini kabla ya kufikisha miaka 18 mtoto hatakiwi kutumia vifaa hivyo kwa zaidi ya saa tatu”anasema.

Hata hivyo,  anaeleza kuwa wazazi wengi hawana uelewa juu ya hatari ya  watoto kutumia kwa muda mrefu vifaa hivyo, hali inayowaweka kwenye hatari ya kupata changamoto mbalimbali za kiafya.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kupata maumivu ya kichwa, kuumwa macho pamoja na kutopata usingizi wa kutosha kutokana na kutumia muda mwingi kuangalia vifaa hivyo.

Daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Fredrick Mashili,  anaeleza kuwa mtoto kuangalia televisheni au vifaa hivyo vya kidigitali kwa muda mrefu,  kunaweza kumnyima fursa ya kuchangamana na watoto wenzake jambo ambalo si jema kwa ustawi wa afya ya ubongo wake.

“Anaweza kutengeneza tabia ya kupenda kukaa akiwa mpweke, kujitenga na kushindwa kuchangamana na wenzake jambo ambalo si zuri kwa afya yake ya mwili na akili,”anaeleza.

Related Posts