Siri Rais Samia kuendelea kung’ara majukwaa ya kimataifa

Miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani imekuwa na ushawishi mkubwa katika jumuiya ya kimataifa kutokana na kuaminiwa na kupewa majukumu kwenye jumuiya za kikanda na ulimwenguni kwa ujumla.

Tangu ameapishwa Machi 19, 2021, Rais Samia ameendelea kuwa kinara katika shughuli tofauti za kimataifa, akiirudisha sifa ya Tanzania kwenye ushirikiano wa kimataifa ambayo ilikuwa imepotea miaka michache kabla hajaingia madarakani.

Kauli ya kuifungua nchi sasa imeshika kasi na Rais Samia kama kiongozi anayebeba ajenda hiyo akiiwakilisha vema Tanzania kwenye majukwaa ya kimataifa huku maono yake yakiiongoza Tanzania kwenye mwelekeo huo.

Licha ya kuwa miongoni mwa marais wanawake wachache barani Afrika na ulimwenguni kwa ujumla, Rais Samia ameonyesha utofauti ambao umemfanya kuwa kinara katika mikutano na vyombo vya uamuzi vya kimataifa.

Pengine kutokana na msingi huo, Watanzania wengine wanapewa imani katika majukwaa na vyombo vya kimataifa wanavyoomba kuviongoza.

Mfano, tulishuhudia Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akichaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Vilevile, kabla ya kifo chake, Faustine Ndugulile alikuwa amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya wa Tanzania, Dk Ntuli Kapologwe ameibuka mshindi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA – HC).

Wachambuzi wa siasa na duru za kimataifa wanaeleza kwamba utayari wake katika kushirikiana na mataifa mengine ni moja ya siri zilizomfanya ang’ae na kuaminiwa katika majukumu mengine ya kimataifa.

Katika mkutano wa kawaida wa 38 wa Umoja wa Afrika (AU) uliohitimishwa Februari 15, mwaka huu, Tanzania ilichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Umoja wa Afrika (Bureua of the African Union Assembly) kwa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, kamati hiyo inaundwa na Angola kutoka Kanda ya Kusini (Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika 2025); Burundi kutoka Kanda ya Kati (Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti); Ghana kutoka Kanda ya Magharibi (Makamu wa Pili wa Mwenyekiti) na Tanzania kutoka Kanda ya Mashariki (Makamu wa Tatu wa Mwenyekiti).

Taarifa hiyo inabainisha kwamba Mauritania iliyokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2024 kutoka Kanda ya Kaskazini itakuwa Katibu wa Kamati hiyo.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo anasema kazi kubwa ya Rais Samia katika majukumu mapya kama mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya AU, itakuwa ni kuhakikisha Afrika inakuwa na amani na mapinduzi ya serikali ambayo yamekuwa yakifanyika Afrika Magharibi, hayatokei tena.

“Role (kazi) yake kubwa itakuwa ni kuhakikisha kwamba Afrika inapata amani na mambo ya kuangushwa kwa serikali yanapungua, pamoja na utunzaji wa mazingira unazingatiwa ili kuwaletea maendeleo Waafrika,” anasema.

Mwishoni mwa mwaka 2023, katika Mkutano wa 28 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), Rais Samia alizindua Programu ya Nishati Safi ya Kupikia ya Kusaidia Wanawake Barani Afrika (AWCCSP) ambayo ilipokewa vyema kimataifa na sasa utekelezaji wake unaendelea.

Mkutano wa Mei 14, 2024, Rais Samia alikuwa mwenyekiti mwenza katika mkutano wa nishati safi ya kupikia kwa Afrika uliofanyika nchini Ufaransa.

Rais Samia alialikwa kwenye mkutano huo na Dk Fatih Birol, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati (IEA). Wawili hao hao walikuwa wenyeviti wenza katika mkutano huo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais Samia alishiriki mkutano huo kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuifanya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha kimataifa.

Taarifa hiyo ya wizara ilieleza kwamba mwaliko huo kwa Rais Samia ulitokana na mchango wake katika kutambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuweka msukumo katika kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kupikia na athari zake.

Mchambuzi wa siasa, Chrispin Masalu anasema ameshuhudia namna Rais Samia alivyoibeba kampeni ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania, kwani huko vijijini na mijini Serikali yake imekuwa ikigawa mitungi ya gesi sambamba na kutoa elimu kwa wananchi.

“Kwa kuwa ni mwanamke, anajua vizuri adha kubwa wanazozipata wanawake wakati kupitia nishati chafu wanazotumia kama kuni na mkaa. Kwa kuwa ni Rais mwanamke, wenzake wakaona wambebeshe hilo jukumu ili alisimamie kikamilifu,” anasema.

Agosti 17, 2024, Rais Samia aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc – Organ Troika) kwenye mkutano wa kawaida wa 44 wa Sadc uliofanyika Harare, Zimbabwe.

Katika mkutano huo, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Sadc huku Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina akiwa ni mwenyekiti ajaye baada ya Mnangagwa kumaliza muda wake wa mwaka mmoja.

Nafasi ya mwenyekiti wa asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ni ya mwaka mmoja na inakwenda kwa mzunguko kama ilivyo kwa nafasi ya mwenyekiti wa Sadc, hivyo anayeteuliwa anatumikia kwa mwaka mmoja kabla ya kukabidhi kijiti kwa mwingine.

Viongozi watatu wa asasi, wanaratibu na kutoa maelekezo kwa nchi zinazokabiliwa na mizozo ya kiusalama, kisha watatoa ripoti yao kwenye mkutano mkuu wa Sadc kuhusu mizozo waliyoishughulikia na mapendekezo yao.

Itakumbukwa kwamba Januari 28, mwaka huu, baada ya mkutano wa Nishati Afrika uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania, Rais Samia aliitisha mkutano wa dharura wa Sadc Organ Troika kujadili mapigano yanayoendea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mtanzania anayeishi Afrika Kusini, Filbert Kimani anasema Rais Samia amefanikiwa kuirejesha Tanzania kwenye nafasi yake kimataifa kutokana na utayari wake wa kushirikiana na mataifa mengine duniani.

“Watanzania tunajisikia fahari sana tunapoona Rais wetu akitambulika kwa kazi anazofanya. Hata hapa Johannesburg ukijitambulisha unatoka Tanzania, wanatuona ni ndugu zao, tunaishi nao kwa amani. Rais Samia aendeleze ushirikiano huo,” anasema.

Mwenyeji mikutano ya kimataifa

Rais Samia amekuwa mwenyeji wa mikutano kadhaa ya kimataifa ambayo imeandaliwa na kufanyika hapa Tanzania. Mmoja wa mikutano hiyo ni ule uliowakutanisha pamoja viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Sadc kujadili hali ya usalama mashariki mwa DRC.

Katika mkutano huo uliofanyika Februari 8, 2025, Rais wa Kenya, Dk William Ruto ambaye ni Mwenyekiti wa EAC, alimshukuru Rais Samia kwa kukubali ombi lake la kuandaa mkutano huo uliowaleta pamoja marais wa kanda hizo mbili.

Mbali na mkutano huo, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa Nishati Afrika (Ajenda300) uliowaleta pamoja marais 21 wa Afrika, rekodi ya pekee ya viongozi wengi kukutana pamoja Tanzania, ambayo haikuwahi kutokea tangu uhuru.

Mkutano huo ulijadili masuala ya nishati na kutengeneza azimio la kuwafikisha nishati ya umeme watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030.

Azimio hilo la Dar es Salaam liliridhiwa na AU kwenye mkutano wake wa Februari 15 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Si hiyo tu, Novemba 19, 2024, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa madini uliowakutanisha pamoja watu 1,500 kutoka ndani na nje ya Tanzania. Mkutano huo uliofunguliwa na Rais Samia, ulihudhuriwa pia na mawaziri wa madini kutoka nchi mbalimbali.

Akizungumzia sababu ya kuwa mwenyeji, Shoo anasema hali ya utulivu ambayo Tanzania inayo, imekuwa ni mfano bora kwa nchi nyingine, hivyo amesema mataifa mengine yanapendekeza mikutano hiyo ifanyikie Tanzania.

Sababu nyingine, anasema katika bara la Afrika viongozi kwenye nafasi za Rais au Waziri Mkuu ni wachache, lakini Tanzania yupo Rais Samia, hiyo anasema inawapa watu imani kubwa katika ulimwengu wa siasa.

“Tangu Rais Samia ameingia madarakani, ameifungua nchi kimataifa kwa sababu amefungua balozi mpya kubwa na ndogo, hivyo Watanzania wengine wanahudumiwa kwenye mataifa mengine na pia wageni wengi wanakuja Tanzania,” anasema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema mrengo wa kidemokrasia alioingia nao Rais Samia ni tofauti na mtangulizi wake, ni wakati huo ikaibuka kaulimbiu ya kuifungua nchi.

“Badala ya kufunga ule ukuta na wadau wengine, sasa umefunguliwa. Gia aliyoingia nayo ni ya ushirikiano zaidi kuliko ya utengano,” anasema Dk Loisulie akiongeza kwamba falsafa yake ya 4R pia imemuuza kimataifa na kuimarisha ushirikiano.

Anasema Rais Samia anachangamana zaidi na mataifa mengine tofauti na mtangulizi wake, hivyo wamemwamini kwa sababu wanashirikiana kwenye majukwaa na taasisi tofauti ambazo anakwenda.

“Jina la Tanzania, pamoja na changamoto zote, bado linaaminika. Tanzania imejijengea jina zuri miaka ya nyuma, hivyo jina hilo linamfanya anatamba katika majukwaa ya kimataifa,” anasema mwanazuoni huyo.

Related Posts