NA DENIS MLOWE,IRINGA
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB). Dr.Thomas Masanja amesema THBUB inatarajia kutoa elimu kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa Wakazi na Wanafunzi wa Shule za Sekondari na Vyuo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuwawezesha kutambua haki zao na kudumisha utawala unaozingatia haki za binadamu.
Masanja ambaye aliambatana na maafisa mbalimbali wa tume hiyo aliyasema hayo wakati akizungumza na wanahabari mkoani hapa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuwa licha ya jamii kunufaika na elimu hiyo wataongea na watendaji kata na viongozi wa kila kijiji mkoani hapa na kuwapa elimu juu ya haki za binadamu ambapo mafunzo hayo yalianza Februari 17 ambapo watahitimisha Machi 7 mwaka huu.
Alisema Tume hiyo itatoa elimu kwa wakazi wa mkoa wa Iringa kupitia mikutano ya hadhara, itapokea malalamiko yanayohusu haki za binadamu na utawala bora kwenye maeneo yao, na pia Tume itawafikia wanafunzi wa Shule za Sekondari na Vyuo vilivyopo mkoani hapa ambao jumla ya vyuo vitatu vitafikiwa ikiwemo Rucu, Chuo Kikuu Iringa (Tumaini), na Mkwawa.
Aidha, zoezi hilo litaambatana na kutembelea Magereza za Mkoa huo kwa lengo kukagua na kutathmini haki za watu wanaozuiliwa, na kutoa mapendekezo jinsi ya kutatua matatizo yaliyopo kwa mujibu wa taratibu na Sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na kukagua viwango vya kimataifa na kikanda vinavyolinda na kutetea haki za binadamu ikiwemo makundi ya watu waliozuiliwa.
Masanja alisema kuwa lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwakumbusha watendaji hao ni namna gani wanaweza kutekeleza majukumu yao kwa kufuata haki za binadamu pamoja na misingi ya utawala bora.
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Iringa, Frank Leonard aliwapongeza tume hiyo kwa kufika mkoani hapa na kutoa elimu kwa jamii na wanahabari kwani ndio wakati sahihi kuweza kupata elimu hiyo ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia vyombo wanavyofanyia kazi kwa kueneza elimu hiyo kwa wananchi mkoani kuzitambua haki zao na kukuza misingi ya utawala bora nchini.
Leonard alisema kuwa dhana ya utawala bora ni zoezi la watu wenye mamlaka na madaraka kutoa maamuzi ya namna gani rasilimali za taifa zitumike katika kuboresha maisha ya wananchi hivyo uwepo na ujao wa tume ya haki za binadamu utasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa wanahabar na wananchi kwa ujumla kutambua haki zao za msingi na utawala bora.