Musoma. Zaidi ya wakulima wadogo 700 mkoani Mara wanatarajiwa kunufaika na kilimo cha umwagiliaji kufuatia utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima vya umwagiliaji, ambao unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh244 milioni.
Mradi huu unahusisha uwekaji wa miundombinu ya umwagiliaji na unatarajiwa kunufaisha wakulima kutoka wilaya nne za mkoa huo. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita kuanzia sasa.
Akizungumza katika Kijiji cha Kwikuba, Wilaya ya Musoma wakati wa kumkabidhi mkandarasi kazi hiyo leo Februari 18, 2025, Mhandisi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Mara, Adelialidy Mwesiga amesema mradi huu unahusisha uchimbaji wa visima saba.
“Wilaya zitakazonufaika na mradi huu ni pamoja na Musoma, Butiama, Bunda na Tarime zitakazopata kisima kimoja kila moja na Serengeti itakayonufaika na visima vitatu,” amesema.
Amefafanua kuwa mradi huo utatekelezwa kwa awamu tofauti, ya kwanza ikihusisha visima hivyo saba. Awamu ya pili itaanza mara baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza.
Kwa mujibu wa Mwesiga, kisima kimoja kitakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wakulima 100 kupitia vikundi vyao maalumu, ambavyo vitaendeshwa chini ya usimamizi wa wataalamu wa kilimo na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, amesisitiza kuwa mradi huu ni muhimu kwa wakulima kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri kilimo cha mvua, hivyo utekelezwe kwa wakati.
“Nauona mwanga wa maisha bora kupitia kilimo cha umwagiliaji kwani ndicho cha uhakika kulingana na mabadiliko ya tabianchi. Mkandarasi asilete ucheleweshaji wowote, nataka kuona mradi huu unakamilika kwa wakati,” amesema.
Aidha, Mtambi ameziagiza halmashauri za wilaya husika kuanza kuandaa mikakati ya upatikanaji wa masoko ya mazao yatakayozalishwa kupitia mradi huo ili kilimo hicho kiwe endelevu na cha manufaa.
Mtambi pia ameonya kuwa uundwaji wa vikundi vya wakulima unapaswa kufanyika kwa misingi ya haki bila upendeleo.
“Sitaki kusikia vikundi vinaundwa kwa upendeleo, yaani wale wenye ushawishi pekee ndio wanufaike. Lengo la Serikali ni kuona kila mwananchi mwenye sifa anapata nafasi ya kunufaika na mradi huu,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kwikuba wamesema mradi huu utakuwa mkombozi wa wananchi wengi na wameomba awamu ya pili ianze haraka.
Kamunyiro Domiko, mmoja wa wanakijiji hao amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, yeye na wenzake wamepoteza shughuli zao za kiuchumi, hivyo kilimo cha umwagiliaji kitawasaidia sana.
“Hapa tulikuwa tunategemea kilimo na uvuvi, lakini siku hizi hata ziwani hakuna samaki na kilimo hakina mavuno kwa sababu mvua hakuna. Hili litakuwa suluhisho kwetu,” amesema.
Kwa upande wake Nyanjiga Masatu ameomba Serikali kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati, akibainisha kuwa wananchi wamesubiri mradi kama huu kwa muda mrefu.
“Mradi kama huu ulitakiwa kuanza miaka mingi sana, tumeteseka kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi, lakini sasa tunauona mwanga wa matumaini,” amesema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya ukandarasi ya MNFM, Mubarak Ngwada,amesema wanatarajia kukamilisha mradi huo mwishoni mwa Aprili 2025.
“Mradi ni wa miezi sita, lakini tunaanza utekelezaji mwezi Machi, na mwishoni mwa Aprili tutakuwa tumekamilisha kazi zote,” amesema.
Mradi huu unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo mkoani Mara kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wakulima.