Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, imethibitisha mauaji ya watoto wiki iliyopita katika Mji wa Bukavu, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Taarifa iliyochapishwa leo Jumanne Februari 18, 2025 mtandao wa RFI imeeleza kuwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk amethibitisha mauaji ya watoto yaliyotekelezwa na M23 inayodaiwa kuungwa mkono na Rwanda baada ya kuingia katika mji wa Bukavu wiki iliyopita.
“Tunatoa wito kwa Rwanda na M23 kuhakikisha haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu zinaheshimiwa,” amesema msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Shamdasani amesema amewaambia wanahabari hao kuwa Umoja wa Mataifa unajua kuwa watoto wanamiliki silaha,
“Hatuna idadi kamili ya mauaji kwa sababu hali ni tete. Watoto watatu waliouawa siku ya Jumapili iliyopita Bukavu walipokuwa wakikusanya silaha katika maeneo yaliyotelekezwa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
“Waliamriwa kuweka chini silaha zao, walikataa na wakauawa,” amesema Shamdasani.
Kamishna Mkuu huyo, ametoa wito kwa Rwanda na M23 kuheshimu haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu (IHL).
Kwa mujibu wa mtandao huo, Türk amepata taarifa za watu kukamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini, sambamba na shutuma za kurejea kwa lazima kwa vijana wa Kongo waliokimbia ghasia katika nchi jirani.
Mtandao huo umeandika kuwa Umoja wa Mataifa pia umepokea maombi ya ulinzi kutoka kwa waathiriwa na mashahidi wa ukiukaji wa haki za binadamu kufuatia maasi siku chache zilizopita kutoka kwa magereza kadhaa ambapo wafungwa walitoroka.
Türk ametoa wito kwa Rwanda na M23 kuhakikisha ulinzi wa watu wote.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema kati ya watu 10,000 na 15,000 wamefika Burundi katika siku za hivi karibuni, hasa kutoka mkoa wa Kivu Kusini na Mashariki mwa DRC, karibu watu 350,000 hawana makazi.
Kulingana na Umoja wa Mataifa pamoja na mamlaka ya DRC, ghasia zilizotokea hivi karibuni zilizosababisha kutekwa kwa mji wa Goma na waasi wa M23 zimewaathiriwa watu 3,000, huku maelfu ya watu pia walijeruhiwa.