Visa vya watoto wa pili kwenye familia

Dar es Salaam. Kwa mujibu wa utafiti nafasi ya mtoto kuzaliwa katika familia, inaweza kuathiri tabia zake.

Inaelezwa kwa mfano, wakati watoto wa kwanza huwa na tabia za uongozi katika kufanya majukumu yao na hata kuwaongoza wadogo zao; watoto wa mwisho au vitinda mimba wanaongoza kwa kudeka.

Aghalabu, huona kila majukumu wanayopewa kama hawastahili. Watoto hawa hupenda kuwadekea wazazi au wale waliowatangulia katika kuzaliwa. Si vibaya nikisema kuwa hata wanaoongoza kwa uvivu hawa ni nambari moja!

Watoto wa pili au wa katikati nao?

Hata hivyo, watafiti wa makuzi wana hadithi tofauti kuhusu watoto wanaozaliwa katikati. Mara nyingi  hawa  huwa na tabia za kutafuta njia za kujitofautisha na ndugu zao, hasa katika mitazamo na maamuzi ya nini wafanye au wawe nani katika maisha.

 Kwa mujibu wa utafiti wa mtandao wa  ‘Educativefeed’, mtoto wa pili huwa na hali ya kipekee inayomtofautisha na ndugu zake wa kwanza na wa  mwisho.

Utafiti unasema mtoto huyo hukutana na changamoto ya kutotaka kufanana na wenzake katika familia.

 Hii inamaanisha kuwa, mtoto wa pili anaweza kuwa na tabia ya kutafuta uhuru na kujitengenezea njia yake mwenyewe,huku akijitahidi kumzidi ndugu yake wa kwanza na wa mwisho. Hii mara nyingi hutokea wakati wa utoaji wa maoni.

 Pia, watoto wa pili huwa na ujasiri na kujiamini kutokana na kujifunza kutoka kwa ndugu zake wa kwanza. Watoto hawa huwa na hamu ya kutafuta njia nyingine ya kuthibitisha kuwa wao ni jasiri.

Kwa mujibu wa utafiti huo, sifa nyingine za watoto hawa ni wasumbufu,wenye maamuzi ya kushtua, watundu na wadadisi katika kila walifanyalo.

Related Posts