Ninapotafakari kwa kina mgogoro unaoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ninakumbuka falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan. Kama ingetekelezwa ipasavyo, inaonekana kuwa ingeweza kuumaliza mgogoro huu mara moja.
Swali linalojitokeza: Kwa nini wasaidizi wa Rais Samia hawachukui hatua kuhakikisha falsafa hii inatumika katika kutatua mgogoro huu?
Kazi ya kiongozi ni kuonyesha njia, kisha wengine wafuate. Rais Samia alipoingia madarakani, alikuta nchi ikiwa na changamoto za kisiasa, na akaja na falsafa yake ya 4R kama suluhisho la kuzitatua. Mgogoro wa DRC unaohusisha waasi wa M23 pia ungeweza kushughulikiwa kupitia falsafa hii na kufikia suluhisho la haraka.
Falsafa ya 4R inajikita katika misingi ya: Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Ujenzi wa Taifa upya (Rebuilding).
Kinachoendelea DRC ni matokeo ya mgogoro wa muda mrefu. Serikali ya DRC inahesabu M23 kama waasi wa Kinyarwanda na inataka waondoke kwenye ardhi yake. Kwa upande mwingine, M23 wanajitambua kama Wanyamulenge, wakazi wa asili wa Goma, hivyo hawaoni sababu ya kuondoka. Rwanda inaunga mkono madai yao ili wapate haki yao ya kutambuliwa.
Fursa kwa Tanzania katika usuluhishi
Wiki iliyopita, nilimpongeza Rais Samia kwa kuitisha mkutano wa wakuu wa nchi za SADC na EAC kujadili mgogoro wa DRC. Hata hivyo, nilisikitika kuona kuwa taarifa za mkutano huo zilitolewa kwa Kiingereza, Kifaransa na Kireno pekee, bila Kiswahili. Tanzania, ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo, inatumia Kiswahili, Goma ni eneo linalotumia Kiswahili, na hata waasi wa M23 wanazungumza Kiswahili. Kwa nini basi Kiswahili kimepuuzwa?
Pia, mkutano huo ulijadili mgogoro wa DRC bila kuwahusisha waasi wa M23, jambo ambalo ni makosa. Haiwezekani kupata suluhisho la mgogoro bila kuwashirikisha wahusika wakuu. Hatua ya kwanza katika usuluhishi ni maridhiano na kusitisha vita.
Mgogoro huu ni fursa adhimu kwa Tanzania kuonyesha uwezo wake wa kutatua matatizo ya Afrika kwa njia za Kiafrika. Ikiwa 4R zitatumika kwa ufanisi, Rais Samia ataonyesha kuwa Tanzania inaweza kuwa kinara wa suluhisho za Kiafrika kwa migogoro ya bara hili.
Njia ya kutatua mgogoro wa DRC kwa 4R ni pamoja na maridhiano (Reconciliation) – Serikali ya DRC inapaswa kukubali kuwa M23 ni sehemu ya raia wake na kufanya mazungumzo ya maridhiano ili kusitisha vita. Lakini pia ustahimilivu (Resilience), yaani DRC inapaswa kujifunza kuvumilia na kukubali uwepo wa raia wake wenye asili ya Rwanda. Vilevile, M23 wanapaswa kuonyesha ustahimilivu kwa kusitisha mapambano na kukubali mazungumzo. Njia nyingine nia mageuzi (Reforms), yaani M23 waachane na jina la waasi na badala yake waonekane kama jeshi la ukombozi wa Banyamulenge. Lazima kufanyike mageuzi ya kijeshi na kisha M23 waingizwe rasmi ndani ya jeshi la DRC.
Na mwisho ni ujenzi wa Taifa upya (Rebuilding), DRC inapaswa kujengwa upya kama taifa lenye mshikamano, linalowahusisha raia wake wote bila ubaguzi wa asili.
Ikiwa falsafa ya 4R itatumika ipasavyo, mgogoro huu unaweza kutatuliwa ndani ya muda mfupi. Suluhisho la kweli linatokana na ukweli kwamba M23 ni sehemu ya DRC na wanapaswa kushirikishwa katika ujenzi wa amani badala ya kuendelea na vita. Rwanda na Uganda zitaacha kuwaunga mkono M23 pindi DRC itakapokubali ukweli huu na kufanya maridhiano ya kweli.
Rais Samia ana nafasi ya pekee ya kulitatua hili kwa kutumia falsafa yake. Ikiwa hatua sahihi zitachukuliwa, Tanzania itang’ara kimataifa kama taifa linaloweza kutoa suluhisho kwa migogoro ya Afrika.
Mungu mbariki Rais Samia, Mungu ibariki Tanzania.