MABAO mawili ya kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua yote yakiwa ya mikwaju ya penalti katika dakika ya tano ya nyongeza ya kipindi cha kwanza na 72, na moja la Mganda Steven Mukwala katika dakika ya 90, yametosha kuipa timu hiyo pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo FC.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa, Lindi, ulianza kugubikwa na matukio tata baada ya dakika ya 35, beki wa kati wa Namungo, Derrick Mukombozi kuonyeshwa kadi nyekundu iliyozua utata mkubwa.
Mukombozi alipewa kadi hiyo na mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Japhet Smart kutoka Katavi huku ikishindwa kueleweka ni kosa gani nyota huyo alilifanya, hali iliyozua utata kwa wachezaji wa kikosi hicho na mashabiki waliokuwa wanafuatilia.
Mbali na kadi hiyo iliyozua sintofahamu, ilishuhudiwa pia penalti tatu zikitolewa ambapo mbili kati ya hizo zimefungwa na Ahoua, huku moja ya Leonel Ateba akikoswa baada ya kudakiwa na kipa, Jonathan Nahimana.
Penalti hiyo kwa Ateba ni ya kwanza kwake msimu huu kukosa kwani kabla ya hapo tayari alikuwa ameshafunga nne ambazo zimemfanya hadi sasa kufikisha mabao manane nyuma ya mshambuliaji kinara wa Yanga, Clement Mzize mwenye mabao 10.
Kiujumla penalti za leo za Simba zinafika 10 katika Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hizo ni moja tu iliyokoswa na Leonel Ateba aliyepiga tano, sawa na Ahoua aliyepiga pia tano ambapo zote amefunga na kufikisha mabao 10.
Ushindi huu unaifanya Simba kufikisha pointi 50 baada ya kucheza michezo 19, ikishinda 16, sare miwili na kupoteza mmoja tu, huku kwa upande wa Namungo ikisalia nafasi ya 13 na pointi 21, kufuatia kushinda sita, sare mitatu na kuchapwa 11.
Akizungumzia mchezo wa leo na kilichotokea, Kocha wa Namungo, Juma Mgunda aliyewahi kuifundisha pia Simba, amesema asingependa kuzungumzia sana kuhusu waamuzi, huku akiweka wazi kadi nyekundu ya beki wake, Derrick Mukombozi iliharibu mipango yao waliyoingia nayo.
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Fadlu Davids amesema ni jambo nzuri kwao kupata pointi tatu ugenini na kuondoka na ‘Clean Sheets’, huku akieleza nyota wawili, Jean Ahoua na Leonel Ateba yeyote ana uwezo wa kupiga penalti kwani wanaelewana vizuri.
Kwa kutoruhusu bao leo, kipa Mousa Camara amefikisha mechi ya 15 bila nyavu zake kutikiswa na hivyo anaendelea kuongoza chati ya makipa ambao hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa mara nyingi.