Unguja. Changamoto ya wananchi wanaoishi katika visiwa vidogo kuzifikia huduma za afya Zanzibar, huenda ikapata mwarobaini baada ya kuzinduliwa boti tano za dharura (Emergency Ambulance Boat) zitakazosafirisha wagonjwa katika maeneo hayo, zenye thamani ya Sh257 bilioni.
Miongoni mwa visiwa vinavyotarajiwa kugawiwa boti hizo ni pamoja na Tumbatu, Kokota, Kojani na Kisiwa Panza.
Akizungumza leo Jumatano, Februari 19, 2025 wakati wa kuzindua boti hizo zenye thamani ya Dola za Marekani 100 milioni (sawa Sh257.5 bilioni) Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema uzinduzi wa boti hizo itaiwezesha serikali kufikia dhamira yake ya kuimarisha sekta ya afya.
Amesema hiyo ni sehemu ya uimarishaji wa huduma za dharura na mfumo wa rufaa kwa wagonjwa, hasa wanaotoka visiwani wanaopewa rufaa kutoka vituo vya afya kwenda hospitali za wilaya, mkoa na Taifa.
Boti hizo zina kitanda kimoja cha mgonjwa, eneo la wahudumu wa afya wawili, sehemu ya kukaa jamaa wa mgonjwa, vifaa mbalimbali vya kutoa huduma za awali kama Monitor, mashine ya kupimia sukari, visaidizi hewa na vifaa vya matumizi ya dharura.

Moja ya boti tano za dharura zilizozinduliwa kutoa huduma za afya katika visiwa vidogovidogo Zanzibar
“Lengo la serikali ni kuhakikisha wagonjwa wanafikishwa katika huduma kwa wakati, ili kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika ikiwemo vifo vya wajawazito na watoto wachanga,” amesema.
Amebainisha kuwa serikali inatambua katika visiwa vidogo vidogo, kuna changamoto za usafiri wa uhakika wa kusafirisha wagonjwa hasa mama wajawazito wakati wa kujifungua au inapojitokeza dharura yoyote ikiwemo ajali.
Alitumia nafasi hiyo kuipongeza Benki ya Dunia kwa kusaidia gharama za ununuzi wa boti hizo na Kampuni ya Qiro Limited, iliyopewa kazi ya kutengeneza boti hizo ambazo zitatoa huduma za dharura kwa wananchi.
Ili zidumu, ameitaka wizara ya afya kuandaa utaratibu mzuri wa kuzisimamia boti hizo ikiwemo kuzifanyia matengenezo kila inapohitajikal, ili kuhakikisha zinafanya kazi muda wote na kufikia lengo lilokusudiwa.
Hata hivyo, amesema boti hizo zitapelekwa kwenye maeneo yenye changamoto kubwa zaidi na maeneo yaliyobaki yatafanyiwa utaratibu wa haraka baadaye.
Amewasihi wananchi kuendelea kutumia huduma za afya kulingana na taratibu za rufaa zilizowekwa na wizara na kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kwa dharura yoyote inayojitokeza ili waweze kuwasaidia kupata huduma haraka.
Awali, Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazuri, amesema uzinduzi wa boti hizo ambazo zimeshakamilika na tayari kutoa huduma kwa wananchi, ni mafanikio yaliyokuja kutokana na maelekezo ya Rais Mwinyi kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma bora za afya alipo.
Amesema kilio cha wananchi na wahudumu wa afya ni hali mbaya ya usafiri wa dharura katika visiwa vidogo vidogo, wakati wa dharura na kusabababisha maafa na vifo kwa wananchi lakini ujio wa boti hizo zitasaidia kuondosha changamoto hiyo.
Waziri Mazrui amesema boti hizo zitagawiwa kwenye visiwa vidogo vidogo Unguja na Pemba ikiwemo Tumbatu, Kokota, Kojani na kisiwa Panza.

Ametoa wito kwa watendaji wa afya kuhakikisha hakuna mtu anayekosa huduma hasa kinamama kwa kisingizio cha kukosa usafiri wa dharura, na badala yake kupambana ili waweze kupunguza madhara kwa wananchi.
Ameipongeza kampuni ya Qiro Group Campany Limited kwa kukabidhi boti tatu na kuamini mbili zilizobaki watakabidhisha ndani ya muda waliokubaliana ndani ya mkataba.
Mbali na hayo, ameipongeza Benki ya Dunia kwani mbali ya boti tano pia kuna magari 20 ya kubebea wagonjwa, gari la kukusanya damu, magari ya kuzolea taka na kwamba dawa na vifaa tiba zitaingia hivi karibuni.
Mwakilishi wa Benki ya dunia, Dk Ernest Masaya amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali hasa sekta ya afya kuona wananchi wanapata huduma bora na nzuri.
Hivyo, ameahidi kuwa benki hiyo itaendelea kutoa mchango huo kila kunapohitajika
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mngereza Mzee Miraji amesema kwa mujibu wa makubaliano, boti hizo zinatakiwa kufanya kazi chini ya uangalizi kwa kipindi cha miaka miwili.
Amebainisha kuwa boti hizo zinatarajiwa kuunganishwa na mfumo wa huduma za dharura, zitakazoweza kuonekana kupitia mfumo wa kidigitali ulioko katika kituo cha afya call center.