CCM inavyopenya Pemba, ngome ya upinzani Zanzibar

Kwa muda mrefu Kisiwa cha Pemba kimekuwa ngome ya upinzani, tangu uchaguzi wa kwanza baada ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa mwaka 1995, kisiwa hicho kilikuwa ngome ya Chama cha Wananchi (CUF).

Hata baada ya waliokuwa makada wa CUF na kuhamia ACT Wazalendo, bado kisiwa hicho kimeendelea kuwa kambi ya upinzani tu.

Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni, CCM imebadilisha uelekeo na kuongeza uwekezaji mkubwa katika kisiwa hicho, ikilenga kukiteka kisiasa.

Hatua ya kuteua viongozi wa Serikali ambao ni wenyeji wa kisiwa hicho, kupeleka miradi ya miundombinu, afya, umeme na uwekezaji ni mbinu inayolenga kukinasua kisiwa hicho mikononi mwa wapinzani.

Hali hiyo inaelezwa na Profesa Mohamed Makame wa Chuo Kikuu cha Suza Zanzibar kuwa, huenda ikabadilisha mioyo ya Wapemba.

Mabadiliko yanategemea na sera za vyama vya siasa na mwamko wa wananchi katika ustawi na maendeleo.

“Pemba imekuwa ngome ya upinzani kutokana na ushawishi wa vyama vilivyopo na tofauti kati ya Kisiwa cha Pemba na Unguja na sababu za kihistoria.

“Lakini kumekuwa na mabadiliko makubwa yanayofanywa na Serikali na hata malalamiko mengi aliyokuwanayo wananchi sasa yanafanyiwa kazi, sasa hiyo itasaidia kupunguza upinzani uliokuwepo,” alisema Profesa Makame.

Aligusia ziara ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliyoifanya hivi karibuni kisiwani humo, akisema kulikuwa na dalili ya wafuasi wa CCM kuongezeka.

Chimbuko la upinzani Pemba

Historia ya upinzani kisiwani Pemba inarudi tangu wakati wa mapambano ya kuondoa ukoloni, ambapo chama cha ASP kilikuwa na nguvu kubwa Unguja, huku vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) vikiwa na nguvu Pemba.

Katika uchaguzi mkuu ulifanyika Zanzibar Julai 1963, idadi ya viti iliongezwa kutoka 22 hadi 31, na matokeo yake yakawa ushindi wa Muungano wa ZNP na ZPPP, ambao ulipata viti 18, licha ya kwamba Chama cha Afro-Shirazi kilichoshinda viti 13, kilijipatia asilimia 54.2 ya kura. Idadi ya wapigakura ilikadiriwa kuwa asilimia 99.1.

Hata hivyo, Januari 12, 1964 yalifanyika mapinduzi ya kuung’oa utaala wa Sultan na hivyo ASP kuingia madarakani.

Tangu wakati huo, kumekuwa na malalamiko ya Wapemba kutengwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hata baada ya Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake kufukuzwa CCM mwaka 1988 kwa madai ya uhaini, chuki za Wapemba ziliendelea na ndiyo maana baada ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa mwaka 1992, Maalim Seif na wenzake walipoanzisha CUF wakishirikiana na James Mapalala, chama hicho kilipata nguvu kubwa Zanzibar hususan Pemba.

Katika uchaguzi wa 1995, CCM haikuambulia hata kiti kimoja kisiwani Pemba. Awali kituo cha televisheni cha DTV, kilimpa ushindi Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Salmin Amour Juma.

Hata hivyo, matokeo ya mwisho yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), yalitoa ushindi wa asilimia 50.24 kwa CCM dhidi ya asilimia 49.76 za CUF.

Matokeo hayo nusura yavuruge amani ya Zanzibar. Ni matokeo ambayo pia yaliishtua CCM kwa sababu ilishindwa vibaya katika kisiwa cha Pemba anakotoka Maalim kiasi cha kutopata kiti hata kimoja cha ubunge wala uwakilishi.

Wafuasi wa CUF Pemba. Picha na Maktaba

Baada ya matokeo hayo, wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CUF walisusia vikao vya Bunge na Baraza. Hali hiyo ilizua sintofahamu, hadi yalipoanza mazungumzo ya mwafaka kati ya CCM na CUF, lakini hayakuzaa matunda yaliyotarajiwa.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Maalim aliwania tena urais na Amani Karume wa CCM.

Ilitarajiwa pia Maalim Seif angeshinda, hata kupitishwa kwa Karume kulikuwa na mivutano ndani ya CCM, lakini haikuwa hivyo, kwani matokeo yalipotoka, Maalim Seif alipata asilimia 32.96, huku Karume akitangazwa kuwa mshindi kwa kupata asilimia 67.04 ya kura.

Matokeo hayo yaliwatia hasira wafuasi wa Maalim Seif kiasi kwamba Januari 28, 2001, waliandamana kupinga matokeo katika visiwa vya Pemba na Unguja na jijini Dar es Salaam.

Maandamano hayo yalisababisha mauaji na baadhi ya wananchi, hasa wa Pemba kukimbilia uhamishoni Mombasa, nchini Kenya.

Hali iliendelea hivyo hivyo katika chaguzi za 2005, 2010, 2015 ambapo CUF iliungana na Chadema na kumsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyegombea urais wa Jamhuri ya Muungano, huku aliyekuwa kiongozi wa CUF Zanzibar, Juma Haji Duni akiwa mgombea mwenza.

Kuungana kwa Chadema na CUF na vyama vingine vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), haukumfurahisha Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na ndipo alipojiuzulu nafasi yake.

Katika uchaguzi huo, kwa upande wa Jamhuri ya Muungano, Lowassa alipata asilimia 39.97 ya kura nyuma ya Rais John Magufuli, aliyepata asilimia 58.46 ya kura.

Kwa upande wa Zanzibar hali ilikuwa mbaya zaidi, kwani aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alitangaza kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi visiwani humo akisema uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi.

Baada ya hapo uchaguzi ulirejewa tena Machi 2016 na CCM ikashinda.

Baada ya hapo, CUF ikaingia kwenye mzozo ambapo Profesa Lipumba aliyekuwa amejiweka kando alirejea na kuzua tafrani kati yake na Katibu Mkuu Maalim Seif.

Mgogoro huo ulidumu hadi mwaka 2019, baada ya upande wa Maalim Seif kufungua kesi mahakamani, ambapo walishindwa na Profesa Lipumba akahalalishwa kama mwenyekiti halali.

Hapo ndipo Maalim Seif na wafuasi wake wengi kutoka Zanzibar waliamua kujiunga na ACT Wazalendo, walipo mpaka sasa.

Baada ya Maalim Seif na wafuasi wake kuhamia huko, sasa ACT wazalendo kimerithi mikoba ya CUF katika ngome yao ya Pemba na maeneo mengine ya Unguja.

Wafuasi wa ACT Wazalendo Pemba

Katika uchaguzi wa 2020, mambo yaliendelea kuwa yaleyale, kwani mgombea wa CCM, Dk Hussein Mwinyi alitangazwa kuwa mshindi wa Urais Zanzibar kwa asilimia 76. 27, huku mpinzani wake, Maalim Seif akiwa mshindi wa pili kwa asilimia 19.87.

Mbali na matokeo ya urais, ACT Wazalendo ilipata pigo Kisiwani Pemba, kwani iliambulia majimbo manne tu kati ya 18 na hivyo kuifanya CCM kupata majimbo 14 Pemba na mengine 30 Kisiwani Uguja.

Uchaguzi huo ulitawaliwa na vurugu zilizosababisha baadhi ya watu kuuawa, wengine kujeruhiwa.

Kutokana na mabadiliko ya Katiba ya Zanibar ya 2010, Maalim Seif aliendelea kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, hadi alipofariki Februari 2021.

CCM inavyopenya kisiwani Pemba

Licha ya madai ya kutumia majeshi na vikosi vya ulinzi na usalama vya Zanzibar, CCM imeendelea kupenya kisiwani Pemba, ikiwemo Serikali kupeleka miradi ya maendeleo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Visiwani Zanzibar, Hamis Mbeto Hamis anasema kwa muda mrefu Serikali ilikuwa imekisahau kisiwa hicho, lakini sasa inawekeza nguvu.

“Tangu Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipoingia madarakani, amefanya mabadiliko makubwa, kwanza ameteua mawaziri sita kutoka Pemba,” anasema.

Anawataja viongozi waliotoka kisiwani Pemba kuwa ni pamoja na Makamu wa kwanza wa Rais, Othman Masoud ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, anayetoka Pandani kisiwani humo, huku Makamu wa pili, Hemed Suleiman Abdallah naye akitokea Kiwani kisiwani humo.

Anawataja pia mawaziri, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduara anayetoka Chake Chake, Waziri wa Serikali za Mitaa na Idara Maalumu, Masoud Ali Mohammed anayetokea Ole.

Wengine ni Waziri wa Elimu, Leyla Mohamed anayetokea Ole, Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis anatokea Micheweni na Waziri wa uwekezaji anatokea Wete.

Pamoja na hao, anasema wapo wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, akisema kwa sasa wanaoteuliwa ni wa kisiwa hicho.

“Zamani wakuu wa wilaya na wakuu na mikoa walikuwa wanatokea Unguja wanakuja Pemba, lakini kwa sasa hata wakuu wa wilaya wote wanne wanatokea Pemba.

“Mabadiliko yote hayo yanalenga kuwaleta karibu Wapemba wasione kama wametengwa,” anasema.

Kuhusu miradi ya maendeleo, Mbeto anasema Rais Mwinyi amepeleka maendeleo Pemba.

“Mfano kwenye miundombinu, mtandao wa barabara una zaidi ya kilomita 1,380, Dk Mwinyi amejenga kilomita 800, kati ya hizo kilomita 400 ziko Pemba.

“Kwa sasa unajengwa uwanja wa ndege wa kimataifa utakaokuwa na njia ya kupaa ndege mkubwa kuliko viwanja vyote Tanzania. Pia zinajengwa bandari tatu, ambapo moja imeshakamilika,” amesema.

Ametaja pia mradi wa viwanda unaojengwa eneo la Micheweni na mradi wa ng’ombe wa maziwa.

“Kwenye umeme Rais Mwinyi amepunguza gharama ya kuunganishwa umeme kutoka Sh400,000 hadi Sh200,000, hivi sasa ukipita vijijini kila mtu ana umeme,” anasema.

Hata hivyo, Katibu wa habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Salum Bimani amesisitiza kuwa Pemba bado ni ngome ya ACT Wazalendo.

“Pemba ipo kama ilivyo, hayo wanayosema CCM ni usanii tu. Hakuna lolote la maana walilofanya zaidi ya kuleta maumivu kwa wananchi.

“Mfano kwenye mfumo wa demokrasia, wanazuiwa kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, kila uchaguzi ukifika ndio unakuwa umefika wakati wa ukatili, kwenye uchumi, vijana hawana ajira, umasikini umetamalaki Pemba.

“Kwa hali hiyo, mwaka huu uchaguzi CCM itashindwa vibaya kama ambavyo imekuwa ikshindwa miaka yote. Wapemba na Wazanzibari kwa ujumla hawaipendi CCM, kwa sababu imeshindwa kusimamia haki zao kwa muda mrefu,” anasema.

Anasema katika uchaguzi wa 2020 CCM ilishinda kupitia vitendo vya ukatili ikiacha vifo, majeruhi na watoto yatima. “Rais alitangazwa hata kabla ya majumuisho, tumeachwa na vifo, majeruhi, akiwamo Makamu mwenyekiti wetu Zanzibar, Ismail Jussa na mayatima.”

Akijibu hoja hizo, Mbeto wa CCM anasema CCM ina haki ya kufanya siasa Pemba na itapambana.

“Pemba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kila chama kina haki ya kufanya siasa popote katika eneo hilo. Miaka yote wapinzani walikuwa wakidanganya kuwa anashinda kisiwani Pemba, lakini ulikuwa ni wizi tu unaofanyika.

“Halafu wamekuwa wakiwarubuni watu wajione kama wanaonewa, kwamba ametelekezwa na Serikal, wakati si kweli, ndio maana sasa CCM imeanza kuwa karibu na wananchi na kushirikiana nao,” amesema.

Akijibu madai ya kuvuruga uchaguzi wa mwaka 2020, Mbeto amesema CCM ilishinda kihalali kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

“Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018 ibara ya 15 wakati wa uandikishaji wapigakura, kila chama kitakuwa na mawakala, atakayeandikishwa ni yule aliyeishi miezi 36, yaani miaka mitatu, pia anatakiwa kuwa na kitambulisho cha Uzanzibari (Zan ID),

“Sasa leo mtu hajatimiza hivyo vigezo, halafu anataka aandikishwe. Inawezekanaje?” anahoji.

Ameendelea kufafanua sheria hiyo, akisema vituo vya kuandikisha wapigakura huwa vitageuka kuwa vituo vya kupigia kura na kila chama kitathibitisha wapigakura walioandikishwa kwenye Daftari la Wapigakura.

“Baada ya kura kupigwa, zitamwagwa hadharani na zitahesabiwa kwa uwazi. Mwaka 2020 uchaguzi ulifuata sheria na kura zihesabishwa na kwenda kwenye majumuisho kituo cha Maruhubi,” anasema.

Related Posts