Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hatima ya mpango wa kuunda muungano mseto wa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kukikabili Chama cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu 2025, itajulikana baada ya chama hicho kupima faida na hasara.
Chama hicho kimedai ingawa hadi sasa bado hakijafuatwa rasmi, suala hilo wamelisikia likizungumzwa na linahitaji mchakato wenye tija kupitia vikao vyao vya ndani kuangalia muundo wake na iwapo kutakuwa na faida watakuwa tayari.
Hayo yanabainishwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Mohamed Abdallah, wakati anafanya mazungumzo na Mwananchi kwenye mahojiano baada ya kutembelea ofisi za Chama hicho Rozana, Buguruni Jijini Dar es Salaam.
Hoja ya vyama hivyo kushirikiana ilianza kuzungumzwa na viongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, kwa nyakati tofauti, hata hivi karibuni Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu amedai wapo tayari kushirikiana na vyama vingine vya upinzani katika uchaguzi huo.
Katika kutekeleza azma hiyo, anasema walishaenda kuongea na vyama vya upinzani kuona haja ya kufanya ushirikiano ili kuunganisha nguvu katika uchaguzi huo kukabiliana na CCM katika nafasi mbalimbali za Ubunge, Udiwani na Urais.
Katika chaguzi za nchi za Afrika, muungano wa vyama vya upinzani umekuwa silaha ya kukabiliana na vyama vikongwe ambavyo vimetawala mataifa yao kwa muda mrefu tangu kwenye harakati za ukombozi hadi zama hizi za ulimwengu wa kisasa.
Baadhi yamataifa ya Afrika yameonesha mfano bora kwa vyama vya upinzani kuungana na kufanikiwa kushika dola na kuviondoa vyama tawala vilivyokaa madarakani kwa muda mrefu na miongo kadhaa.
Mathalani, miaka ya hivi karibuni tulishuhudia Botswana vyama vya upinzani vilivyoungana na kufanikiwa kukiondoa chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP), ambacho kilikuwa madarakani tangu mwaka 1966.
Tanzania muungano wa vyama vya upinzani si jambo jipya, kwani mwaka 2015 ulifanyika, baada ya kuanzishwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ulioleta mafanikio makubwa kwa vyama vya upinzani kupata mafanikio makubwa, ikiwemo idadi ya wabunge.
Pamoja na manufaa yaliyojitokeza, Husna anasema suala la kuanzisha muungano wa kuikabili CCM, katika uchaguzi ujao ni suala linalohitaji mchakato ili kufanya maamuzi yenye tija.
“Bado hatujafuatwa, ila ni lazima tuwasikilize wanaohitaji kuungana ili tuangalie CUF tutanufaika vipi na jambo gani tunaweza kupoteza, lakini mwisho wa siku maamuzi ya kuungana au kutokuungana yatatokana na vikao,” anasema.
Husna anasema kwa mtazamo wake, suala la kuungana linaweza kuwa na tija na hasara, lakini ili wajue ni lazima wakutane kwanza pande husika zinazohitaji kufanya hivyo.
“Tusikilize dhamira za wale wanaohitaji kuungana, baada ya kutafakari tutajua kama kuna faida kiasi gani,” anasema.
Msingi wa hoja ya Husna anasema licha ya kwamba siku zote chama hicho kimekuwa kikiunga mkono mashirikiano, ikiwemo ule wa mwaka 2015, vyama vingine vimekuwa vikikwamisha.
Akizungumzia alivyolipokea vuguvugu la kudai mifumo huru ya uchaguzi kupitia falsafa ya ‘No reform no Elections’ iliyoanzishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Husna anasema huo bado unabaki kuwa mtazamo wao.
“CUF, kwa upande wetu tunasema tutashiriki uchaguzi ingawa tunahitaji mabadiliko na tutaendelea kudai hadi pale yatakapopatikana, huku tukiingia kwenye chaguzi,” anasema.
Husna anasema ingawa hoja yao hiyo ina msingi mkubwa, wao wanaona kugomea uchaguzi ni jambo baya. “Pamoja na kwamba tunahitaji mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi, haimaanishi hatutashiriki uchaguzi.
“Tunakubali kuna changamoto kwenye mifumo ya uchaguzi, lakini suluhisho si kususia, CUF tulishasusia mara nyingi, hata Zanzibar mwaka 2015 vyama vya siasa viligomea na kukiacha CCM na Alliance for Democratic Change (ADC), na walifanikiwa kutengeneza sheria zote kandamizi,” anasema.
Anasema moja ya sheria kandamizi walizopitia ni kura ya siku mbili, jambo ambalo ni ajabu na waliowengi wanashangaa jinsi Zanzibar ilivyokuwa na idadi ya watu kidogo inakuwaje kura zinapigwa siku mbili.
“Tunaamini kugomea si suluhisho, ni muhimu kuendelea kudai huku tukishiriki uchaguzi hadi hapo haki itakapopatikana, naamini kwa mazingira yaliyopo na sheria hizi tunaweza kupata wawakilishi kwenye nafasi za maamuzi kutusaidia kupaza sauti zetu,” anasema.
Anasema suala la kuweka wajumbe kwenye mihimili ya kutunga sheria, ikiwemo Bunge ni jambo la muhimu, kwani watakuwa wanawasilisha mawazo na nguvu ya kubadilisha sheria zinazokandamiza.
“Kugomea ni kuzidi kuipa nguvu CCM na serikali iliyopo kuendelea kutamba, kwani wao watashiriki na watakuwa wengi kwenye vyombo vya kutunga sheria na itakuwa si sawa,” anasema.
Husna, ambaye ni Katibu mkuu wa sita na wa kwanza mwanamke tangu kuanzishwa CUF, Mei 28, 1992 anazungumzia hali ya kisiasa kwa pande mbili, akianza na kusema Tanzania imepiga hatua ikilinganishwa na miaka iliyopita kipindi cha Rais wa awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli.
“Angalau watu wanaruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa kwa uhuru, lakini kwa upande mwingine sina imani na upoteaji wa watu kama hautaendelea, kwani ni jambo linalozusha hofu hasa kwa vyama vya upinzani na wanaishi kwa wasiwasi,” anasema.
Anasema hawana imani kama uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa wa huru na haki, huku akifanya rejea uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka uliopita uliokatisha tamaa wengi.
“CUF tulipendekeza uchaguzi ufutwe kwa sababu ulionyesha kuminywa na kuporomoka kwa demokrasia Tanzania, tungeweza kutumia nguvu ya umma, lakini kwa kuwa tunahitaji amani tunatumia mdomo kuongea,” anasema.
Anasema wanajua wakiandamana watu watapata madhara makubwa na Tanzania ni maskini, wananchi watahangaika na wanabaki kwenye upande wa amani na kuitaka Serikali kusimama kwenye uadilifu, kwani wao hawataki kuvunja amani.
Husna, aliyedhamiri kuwainua wanawake katika nafasi za maamuzi ndani ya chama hicho, anasema tayari wameshafungua pazia kwa wale wanaojiona wanania ya kuwania nafasi mbalimbali za kugombea uongozi kupitia chama hicho katika uchaguzi ujao.
“Na nitumie fursa hii kwa yeyote anayejiona anatosha kugombea na ana sifa tunamkaribisha kugombea kwa masharti ya Kikatiba, ikiwemo awe mwanachama wa CUF, awe ametimiza miaka 18 na kuendelea,” anasema.
Husna anasema hata waliopo nje ya chama hicho wanakaribishwa kujiunga na CUF ili waweze kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, huku akieleza milango iko wazi.