Djigui Diarra, Yanga kikao kizito

UNAKUMBUKA mabao matatu ya hivi karibuni aliyofungwa Yanga? Sasa kocha wa timu hiyo Hamdi Miloud ameona usinchezee. Ameamua kufanya uamuzi wa haraka ili kunusuru jahazi hilo na misukosuko haswa wakati huu wa dakika za lala salama kuelekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Ameitisha kikao cha ghafla na kipa wa timu hiyo Djigui Diarra ajenda kuu ikiwa ni kutathmini utendaji wake lakini kuona ni nini cha kufanya kwa haraka.

Yanga inaongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 52 lakini ikiwa na kasi nzuri ya kufunga mabao baada ya kuwa kinara pia kwa kupachika 50 lakini ikiruhusu mabao tisa, huku matatu yakiwa ni ya mechi za hivi karibuni.

Hata hivyo, kitendo cha timu hiyo ambayo imetwaa ubingwa mara tatu mfululizo kuruhusu mabao matatu kwenye mechi tatu zilizopita, kimeshtua kocha huyo na kuitisha kikao cha haraka na kipa wake kujadili nini ambacho kimekuwa kikitokea.

Miloud ambaye ameiongoza Yanga kwenye michezo mitatu, akishinda miwili na kutoa sare mmoja, huku kikosi chake kikifunga jumla ya mabao nane na kuruhusu matatu ambayo ndio msingi wa kikao hicho.

Kwenye mabao hayo, mawili yamekuwa yakionekana kuwa si ya kufungwa kipa aina ya Diarra ambaye ni  namba moja wa Mali. Ni dhidi ya KenGold ambalo lilifungwa na Selemani Bwenzi kwa shuti kali kutoka katikati ya Uwanja na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 6-1, pamoja na lile la juzi dhidi ya Singida ambalo lilipachikwa na Jonathan Sowah baada ya kipa huyo kuudaka mpira na kuuachia ukamkuta mfungaji, huku Yanga ikishinda 2-1.

Akizungumza na Mwanaspoti pamoja na kuwasifia washambuliaji wake, Miloud alisema ameona wepesi wa mabao ambayo wameyaruhusu tangu atue Yanga lakini kwanza anataka kufanya kikao cha ndani na kipa wake Diarra kujua mambo flani hivi ambayo hakutaka kuyaweka wazi.

Kocha huyo, amekiri kwamba baadhi ya mabao ambayo wameyaruhusu yanatokana na kupungua kwa umakini kwa kipa huyo na hata mabeki wake.

“Bila shaka kuna makosa kwenye eneo la ulinzi, ndiyo tunaweza kufanya makosa lakini kuna makosa hatutakiwi kuyafanya kwa kuyarudia kwa timu kubwa kama hii, kuna eneo unaona msingi wa makosa haya ni kupungua kwa umakini, inaweza kuwa kwa kipa wetu au hata wenzake.

“Kuna nyakati unaona kama kuna baadhi ya wachezaji wanaona kama mechi imekwisha na wanapoteza umakini, hili linatakiwa kufanyiwa kazi haraka kwani tusipolirekebisha linaweza kuja kutuweka kwenye wakati mgumu.

“Nimepanga kwanza nitakuwa na kikao na kipa wangu (Djigui Diarra), kikao cha ndani nitazungumza naye mawili matatu na baada ya hapo nitazungumza na wote wanaocheza kule nyuma, tunatakiwa kujikita kuimarisha safu yetu ya ulinzi ili kuondoa hatari kama hizi,” alisema kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika.

Takwimu zinaonyesha Yanga msimu uliopita ndani ya mechi 20 ilizocheza kama sasa ilikuwa imefunga mabao 48 huku ikiruhusu mabao tisa sawa na msimu huu ikiwa na jumla ya pointi 55 lakini sasa imekusanya pointi 52 .

Miloud alisema washambuliaji wake na hata viungo wameonyesha uchu wa kufunga mabao ambapo sasa anataka kuwaongezea utulivu ili kufunga mengi zaidi. “Kuna kazi nzuri na kubwa inafanywa kule mbele unaona namna washambuliaji wanafunga, lakini pia hata viungo, kasi yetu tukielekea lango la wapinzani ni nzuri sambamba na kutengeneza nafasi.

“Nilisema awali, napenda kuwa na timu inayoshambulia kwa nguvu ni sawa tunafunga lakini bado tunaweza kutengeneza mabao zaidi kutokana na nafasi ambazo tunazitengeneza, hiki tutaendelea kukiboresha taratibu, tunataka vijana wakifika pale mbele watulie wafunge mabao,” alisema kocha huyo.

Clement Mzize ana mabao 10 huku Prince Dube akiwa nayo tisa kileleni mwa msimamo wa ufungaji.

Related Posts