Faida mbili malori kutumia matairi makubwa

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwaita watu wenye ubunifu unaoweza kuongeza thamani katika sekta ya usafirishaji, imevitaka vyuo kufanya tafiti ili kujua faida za matumizi ya matairi makubwa (super single tire) katika malori.

Agizo hilo limetolewa kufuatia kuwapo kwa taarifa matumizi ya tairi hizo yanasaidia katika kupunguza matumizi ya mafuta na kulinda barabara.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa katika maadhimisho ya miaka 35 ya ushirikiano kati ya Superdoll Tanzania na Kampuni ya BWP yaliyofanyika leo jijini hapa.

Profesa Mbarawa amesema Serikali iko tayari kupokea bunifu yoyote ambayo inalenga kuongeza tija katika sekta ya usafirishaji kwani lengo la Tanzania ni kuwa kitovu cha usafirishaji ukanda wa Afrika ya Mashariki.

Alitolea mfano wa bunifu mbalimbali ikiwemo ya breki ya upepo ambayo imefanywa na Superdoll amesema imefanya vyema katika kusaidia usafirishaji.

“Kuna hii nyingine ya Super single tire inatajwa kuwa na faida ya kupunguza matumizi ya mafuta na kufanya barabara ziwe salama lakini bado bado sisi hatuitumii, najua kuna watakaopinga ili ni vyema tukawaelimisha watu ili tuweze kutumia super single tire hapa nchini,” amesema Profesa Mbarawa. 

 Kufuatia faida hizo alivitaka vyuo hapa nchini kufanya tafitii kujua kwanini tairi hizo haziwezi kutumika Tanzania.

“Nchi kama Ujerumani wanatumia tairi hizi kwanini isiwe Tanzania, pia ni vyema mnapofanya tafiti hizi mkatumia tairi zile ambazo ni halisi na si zilizochakachuliwa,” amesema Profesa Mbarawa na kuongeza.

Waziri wa uchukuzi, Prof Makame Mbarawa akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 35 ya ushirikiano ya kampuni ya Supardoll na BWP iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Jumatano Februari 19, 2025. Picha na Michael Matemanga

“Watu wa vyuo vikuu waite waje watusaidie kufanya tafiti kwanini isitumike Tanzania lazima tuwashirikishe pia Tanroads katika hili, ndiyo ubunifu wenyewe,” amesema.

Amesema Serikali inatoa kipaumbele kwa wawekezaji kwani inaamini Tanzania itaendelea ikiwa kazi zinafanyika kwa ushirikiano na Sekta binafsi.

Hiyo ni kwa sababu sekta ya usafiri wa reli na barabara ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi kwani njia hizo zinarahisishaji ufikishwaji wa bidhaa na huduma kwa watu.

Hiyo pia inaunganisha wafanyabiashara na masoko, wakulima na walaji, viwanda na wasambazaji hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi kuongeza ajira na kuimarisha biashara za ndani na kikanda.

“Serikali hii imeamua kwa dhati kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo katika ujenzi wa reli ya kisasa. Nafikiri Afrika ni nchi pekee ambayo inajenga reli yenye urefu mkubwa inayotumia umeme yenye uwezo wa kwenda kilomita 160 kwa saa,” amesema Profesa Mbarawa.

Akizungumzia miaka 35 ya ushirikiano wa kampuni hizi, Profesa Mbarawa amesema umeleta mabadiliko katika sekta ya usafirishaji si Tanzania tu bali pia katika baadhi ya maeneo ndani ya Afrika.

Awali, Mkurugenzi mkuu wa Superdoll Tanzania, Seif Ally Seif amesema uwepo wa kampuni hizo umewezesha kukua kwa viwanda na usafiriahaji.

Hiyo ndiyo imefanya kuwapo kwa ongezeko la   teknlojia mbalimbali zinazoletwa nchini zikilenga kuongeza ufanisi.

“BwP ni kampuni ambayo ina miaka 127 kwahiyo wana teknolojia kunwa walizobobea duniani ndiyo hiyo tuneiiga na tunazalisha bidhaa zenye ubora wa kimataifa,” amesema Seif.

Related Posts