Milio ya risasi ilisikika katika mji wa mpakani wa Uvira, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jumatano, vyanzo vya ndani vilisema, huku mapigano yakizuka kati ya vikosi vya washirika katikati ya kusonga mbele kwa waasi wanaoungwa mkono na Rwanda.
Wakazi na maofisa wameeleza hali ya uporaji, miili ikiwa mitaani na wanajeshi wa serikali wakiteka boti ili kukimbilia Ziwa Tanganyika. Gereza la eneo hilo pia lilifunguliwa, waliripoti.
Waasi wa M23 wamekuwa wakielekea Kusini kuelekea Uvira, mji unaopakana na Burundi kupitia ziwa, tangu waliponyakua mji mkuu wa Jimbo la Bukavu mwishoni mwa wiki pigo kubwa zaidi kwa Congo tangu kuanguka kwa jiji kubwa la Goma mwishoni mwa Januari.
Kuingia kwa waasi katika mji wa Kamanyola Jumanne kumesababisha hofu Uvira, umbali wa kilomita 80 (maili 50) kusini. Tangu Bukavu kuanguka, wanajeshi wa Congo waliokuwa wakirudi nyuma wamejikuta wakipigana na wanamgambo washirika wanaoitwa Wazalendo, ambao hawataki kurudi nyuma.
“Tuliamka na risasi zikirindima kutokana na kusonga mbele kwa waasi, ingawa bado wako mbali,” Ofisa mmoja wa eneo hilo alisema kwa masharti ya kutotajwa jina.
“Vikosi tulivyovitegemea, FARDC (jeshi) na Wazalendo, haviko sawa. Kuna vifo na uporaji.”
Wakazi wanne wa Uvira pia walithibitisha kusikia milio ya risasi mjini. Chanzo cha kuyokq shirika la misaada ya kibinadamu kilisema kuwa miili imejaa mitaani, huku zaidi ya miili 30 ikiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha mji huo, na zaidi ya watu 100 wakiwa hospitalini na majeraha mabaya.
Reuters haikuweza kuthibitisha idadi hiyo
Machafuko haya yanaonyesha udhaifu wa mamlaka ya Congo Mashariki, ambako M23 imechukua maeneo makubwa, pamoja na sehemu zenye madini yenye thamani, hali inayozua hofu ya vita vikubwa zaidi.
Wanajeshi wengi walikuwa wakijazana kwenye boti wakikimbia Uvira, chanzo cha usalama kilisema, na kuongeza kuwa hatua hiyo ilisababisha hali ya taharuki miongoni mwa wale waliokuwa hawawezi kuondoka, huku risasi zikifyatuliwa ovyo ovyo.
Gereza la eneo hilo lilifunguliwa, ikiwa ni pamoja na wanajeshi 228 waliokamatwa kwa kukimbia vita, chanzo cha usalama kilisema. Haikufahamika kama wafungwa walitoroka kwa nguvu au waliachiliwa kwa makusudi.
Taarifa kutoka kwa vyanzo vya habari zinasema matumaini ya Congo kujihami dhidi ya waasi wa M23 yamepungua baada ya wanajeshi wa Burundi waliokuwa wakisaidiana kuondoka. Hata hivyo, Burundi imekanusha madai hayo.
Wakati huohuo, mapigano kati ya waasi na jeshi la Congo yameongezeka katika jimbo jirani la Kivu Kaskazini, msemaji wa jeshi, Mak Hazukay, alisema Jumatano, akibainisha kuwa baadhi ya wanajeshi wameziacha nafasi zao, hali inayosababisha hofu zaidi.
Waasi wa M23, ambao wana silaha za kisasa, ni sehemu ya harakati ndefu za waasi wa Kitutsi Mashariki mwa Congo, mgogoro unaoendelea kutokana na mvutano wa kikabila, mamlaka, na rasilimali za madini, tangu mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda.
Rwanda inakanusha madai ya Congo na Umoja wa Mataifa kuwa inaunga mkono kundi hilo kwa silaha na wanajeshi.
Badala yake, inadai inajilinda dhidi ya wanamgambo wa Kihutu wanaopigana kwa kushirikiana na jeshi la Congo.
Congo inakataa madai ya Rwanda na kusema kuwa Rwanda inatumia wanamgambo wake kuiba madini kama vile coltan, ambayo hutumika katika utengenezaji wa simu na kompyuta.
Machafuko hayo yamezua hofu hata umbali wa kilomita 1,600 (maili 1,000) mjini Kinshasa, ambako baadhi ya wakazi wanapanga kuwahamishia familia zao nje ya nchi, huku kukiwa na tetesi za mapinduzi.