Jaji wa Mahama nchini Marekani ameruhusu idara inayoongozwa na Elon Musk, inayojulikana kama Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE), kuendelea na zoezi lake kufukuza na kupungaza wafanyakazi wa serikali kuu na kupewa mifumo ya data ya mashirika ya shirikisho.
Hata hivyo, jaji huyo ameonyesha wasiwasi kuhusu mamlaka makubwa anayoshikilia Musk kama msaidizi mkuu wa Rais Donald Trump.
Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani mjini Washington, Tanya Chutkan, jana Jumanne Februari 18 alikataa ombi lililowasilishwa na zaidi ya majimbo kumi na mawili kutaka kuzuia DOGE kutumia mifumo ya kompyuta ya mashirika saba ya serikali au kufuta ajira za wafanyakazi wa umma wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani.
Musk, ambaye ndiye mtu tajiri zaidi duniani, anaongoza DOGE, taasisi inayotekeleza mpango wa rais wa chama cha Republican wa kupunguza ukubwa wa serikali na kuifanyia marekebisho makubwa.
Katika uamuzi wake, Jaji Chutkan aliandika kuwa majimbo yaliyoleta kesi hiyo yana “sababu halali ya kuhoji mamlaka yasiyo na mipaka ya mtu ambaye hajachaguliwa na taasisi ambayo haijaidhinishwa na Kongresi wala haina usimamizi wake.” Hata hivyo, alibainisha kuwa majimbo hayo hayakuonyesha sababu za kutosha kupokea agizo la dharura la kuzuia hatua za DOGE.
Kesi hiyo ililenga kuzuia DOGE kupata data au kuamuru kufukuzwa kwa wafanyakazi wa mashirika ya Kazi, Elimu, Afya na Huduma za Kijamii, Nishati, Uchukuzi, Biashara, pamoja na Ofisi ya Usimamizi wa Rasilimali Watu.
Jaji Chutkan anaweza baadaye kutoa uamuzi unaounga mkono majimbo hayo, lakini katika hukumu yake ya sasa, alisema ombi lao lilikuwa pana mno na halikuwa na uthibitisho wa kutosha wa dharura.
Ikulu ya White House haijatoa maoni mara moja kuhusu suala hilo. Mwanasheria Mkuu wa Arizona, Kris Mayes, mmoja wa maafisa waliofungua kesi hiyo, alisema ofisi yake itaendelea “kupambana mahakamani kulinda haki za wananchi wa Arizona dhidi ya matumizi mabaya ya mamlaka ya kiutendaji.”