Joto kuendelea kutikisa Dar mvua zikinyesha Ruvuma, Njombe

Dar e Salaam. Wakati mikoa ya Ruvuma na Njombe ikitarajiwa kupata mvua mkubwa ndani ya saa 24 zijazo, hali ya joto itaendelea kutikisa Zanzibar na mikoa ya Dar es Salaam na Tanga.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 19, 2025 na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) iliyoeleza utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3 usiku.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa maeneo mbalimbali ya mikoa ya Ruvuma na Njombe itapata mawingu, mvua na ngurumo.

Hali ya mawingu kiasi, mvua, ngurumo na vipindi vichache vya jua itashuhudiwa pia katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, Iringa, Songwe, Mbeya, Lindi na Mtwara.

Wakati hali ikiwa hivyo kwenye maeneo hayo hali ya joto itaendelea kusumbua katika Jiji la Dar es Salaam ambapo kiwango cha juu cha joto kinatarajiwa kuwa nyuzi 34.

Kiwango kama hicho kinatarajiwa kuwepo Zanzibar ikifuatiwa na Mkoa wa Tanga unaotarajiwa kuwa na nyuzi joto 33.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya utabiri watumiaji wa bahari wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kuwa hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa kiasi.

Hali ya mvua kiasi na vipindi vya jua vitashuhudiwa katika mikoa ya Tabora, Singida, Dodoma, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Pwani, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na Simiyu.

Related Posts