Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Mohamed Abdallah, ameahidi kupigania ushiriki wa wanawake wa chama hicho katika nafasi za uamuzi kwenye uchaguzi wa 2025, pamoja na kusukuma mbele mabadiliko ya kisera kwa lengo la kulinda haki na maslahi yao nchini.
Amesema ingawa jukumu lake kuu ni kuhakikisha chama kinapata uungwaji mkono kutoka kwa wananchi, anatazama uteuzi wake kama fursa muhimu kwa wanawake kuonekana na kung’ara zaidi katika uongozi.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu katika Ofisi za CUF zilizopo Buguruni Rozana, Dar es Salaam jana Jumatatu Februari 17, 2025, Husna amebainisha kuwa wanachama watarajiea mabadiliko makubwa ndani ya chama.
Husna aliteuliwa kushika wadhifa huo na wajumbe wa chama hicho kwa kura 19 dhidi ya kura 11, alizopata Ali Abarani baada ya majina yao kuwasilishwa kwenye kikao na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kupigiwa kura.
Anakuwa Katibu mkuu wa sita na wa kwanza mwanamke tangu kuanzishwa kwa chama hicho, Mei 28,1992.

Baada ya kuungana taasisi mbili za harakati ya kidemokrasia ikiwemo Kamahuru ya Zanzibar na Civic Movement kutoka Tanzania Bara na kutengeneza chama cha kisiasa cha Wananchi (CUF), kilichokuwa kinapigania haki za binadamu.
Watangulizi wake waliowahi kushika wadhifa huo ni Shaaban Khamis Mloo, Maalim Seif Shariff Hamad, Khalifa Suleyman Khalifa, Haroub Mohamed Shamis na Hamad Masoud Hamad.
Akizungumza zaidi, Husna amesema jinsia ya kike inaandamwa na vikwazo vingi vinavyo kwamisha kufikia ndoto zao mathalani uongozi.
“Nitatoa elimu kwanza wajue, mtu kuwa mwanamke na mwanaume ni maamuzi ya Mungu, haimaanishi kuwa mwanamke ni gredi namba mbili, ikilinganishwa na wanaume kwa sababu ni wote tunahaki sawa,” anasema.
Amesema anatamani kufanya mabadiliko makubwa ili wanawake waione kesho iliyobora kwa kujieleza na kuchangamkia fursa bila kujali jamii inayowazunguka itawachukuliaje.
“Mimi ni Mwanamke nazijua hizi changamoto, nataka kuweka alama ndani ya chama chetu, wanikumbuke katika nafasi hii ya utendaji kuwatia nguvu wanawake kwamba inawezekana kushika nafasi yeyote wakiamua,” amesema Husna.
Amesema anatamani kuona fursa sawa zinatolewa kwa wote huku akieleza hata katika uchaguzi ujao atahakikisha wanawake wenye uwezo wanajitokeza na kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi kuanzia kwenye Udiwani na Ubunge.
“Wanawake wanahitaji kushirikishwa na waliowengi udhaifu wao, wamejawa na hofu, kutojihamini na baadhi hawana elimu toshelezi ya kutimiza ndoto zao, kwanza kwenye ushirikishwaji nitaamsha morali na ari zao na kuwafanya wawe wafanisi zaidi,” amesema.
Mbali na hilo, amesema anajua wengi wao wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Anasema sababu kuna baadhi ya ndoto ili waweze kuzifikia, wanahitaji raslimali fedha, hivyo anasema kuna haja y kuwa na sera itakayoongoza katika hilo.
“Pamoja na haiba zao kuwa jasiri jambo lingine wanakosa kuungwa mkono na familia au jamii inayozunguka lakini kila wanapotaka kupiga hatua wanakumbana na vikwazo ikiwemo wivu wa waume au mila na silika za jamii zetu,” amesema katibu mkuu huyo.
Amesema mara nyingi, wazazi nao huweza kuwa kikwazo kwa vijana wa kike kushiriki siasa, kwa kuhofia kwamba kupanda kwao majukwaani kutatafsiriwa kama kujitangaza binafsi.
Aidha, aina fulani za siasa zinazoendeshwa zimekuwa na matukio ya udhalilishaji wa kijinsia, jambo linalokatisha tamaa wanawake kushiriki kikamilifu.
“Changamoto hii inahitaji sheria kali ili kuwawajibisha wanaobainika kufanya makosa hayo ya kijinsia. Hatua hiyo itawezesha kundi hili muhimu kupata nafasi yake stahiki, nami nitasimamia kuhakikisha haki inatendeka,” amesema.
Jukumu lake ndani ya chama
Amesema kwa kuwa chama kimemuamini kumpa nafasi hiyo, hana budi kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na uaminifu ili kurudisha imani waliyoonyesha kwake. Lengo lake ni kurejesha nguvu za chama kama ilivyokuwa awali.
“Nimejipanga kuimarisha chama kwa kuongeza wanachama wapya na kuwalinda waliopo, kwani wanachama ni mtaji muhimu katika kufanikisha malengo ya kushika dola,” amesema Husna.
Pia ameeleza kuwa moja ya changamoto zilizopunguza uungwaji mkono wa chama ni mtikisiko uliotokea kati ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad (sasa marehemu) na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
“Tofauti kati ya viongozi hawa wawili zilichangia kugawanyika kwa chama na kusababisha makundi mawili, moja likimuunga mkono Profesa Lipumba na jingine ambalo walikuwa wengi wakiwa upande wa Maalim Seif,” amesema.
Hata hivyo, anaamini kuwa ana nafasi nzuri ya kuwarejesha wanachama waliokwenda ACT-Wazalendo na kuwaunganisha tena chini ya CUF.
“Wengi walikwenda kule kwa mapenzi yao kwa Maalim Seif, lakini bado wanakipenda CUF. Nafasi ipo ya kuwarudisha, ingawa sijaanza mazungumzo nao rasmi,” amesema.
Amesisitiza licha ya changamoto zilizopita, wanachama wengi bado wana imani na chama kutokana na misingi yake thabiti ya kupigania haki kwa wote.