Kauli ya Sheikh Ponda kwenye maziko ya Sheikh Muwinge

Morogoro. Waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kwa ujumla wametakiwa kuishi wakiwa na jukumu la kuhakikisha wanaacha alama njema duniani kwa kuwa, maisha ya mwanadamu ni safari fupi.

Wito huo umetolewa leo Jumatano, Februari 19, 2025 na Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu, Sheikh Issa Ponda wakati akizungumza kabla ya mazishi ya mwanazuoni mkongwe Sheikh Ayub Muwinge, aliyefariki dunia Februari 18, 2025 kwa maradhi ya moyo. Sheikh Ponda amewahimiza waumini kuishi kwa misingi ya haki, uadilifu na kuhudumia jamii yenye uhitaji.

Amesema kuwa alimfahamu Sheikh Muwinge akisema alikuwa kiongozi na mwalimu mahiri aliyetoa mchango mkubwa katika kuupigania uislamu na kuwapigania waislamu kuacha maasi na badala yake kumcha Mwenyezi Mungu.

“Amefundisha masheikh wengi, alihimiza maadili mema na uongozi hivyo, alama yake itaendelea kuishi kwa vizazi vijavyo,” amesema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda amesema ingawa kifo cha Sheikh Muwinge ni pigo kwa jamii ya Kiislamu, lakini ni somo la kutafakari thamani ya matendo mema yanayoacha alama isiyofutika.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Sheikh Muwinge, ambaye alimfahamu kama mwanazuoni na mtu aliyejitoa katika kuupigania uislamu kwa nguvu, mali na maarifa.

“Bahati mbaya nimepata taarifa za msiba huu leo asubuhi nikiwa Ifakara kwenye ziara, najua viongozi wenzangu watakuwa wameniwakilisha vyema. Namuombea dua Sheikh Muwinge Mwenyezi Mungu ampekee na amlipe mema yake aliyoyatenda huku duniani,” amesema Malima.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro, Fikiri Juma amesema marehemu Sheikh Muwinge alijipambanua katika kuupigania uislamu na waislamu na katika uhai wake alipenda kusaidia yatima na wenye uhitaji

“Pamoja na mengi mema ya Sheikh Muwinge, lakini katika uhai wake alikuwa mjumbe wa bodi mbalimbali zinazoshughulika na masuala ya uislamu. Alikuwa mwalimu mahiri aliyependa kuona wanafunzi wanafika mbali na hilo linajidhihirisha kwani, kwa sasa kuna masheikh na walimu wengi nchini,” amesema.

Related Posts