Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru, mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Willibrod Slaa (76) kupelekwa mahakamani hapo Machi 4, 2025 wakati kesi yake ya kusambaza taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii, itakapotajwa.
Dk Slaa ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mgombea urais kupitia chama hicho katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, anakabiliwa na shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika Mtandao wa X, kinyume cha sheria.
Amri hiyo imetolewa leo Jumatano, Februari 19, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Ushindi Swallo baada ya mshtakiwa huyo kushindwa kupelekwa mahakamani hapo wakati kesi yake ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Swallo ametoa amri hiyo baada ya upande wa utetezi kuwasilisha ombi mahakamani hapo wakiomba mteja wao awe anapelekwa mahakamani hapo wakati kesi yake inapotajwa.
Awali, kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema ameieleza mahakama hiyo upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na wakisubiri taratibu za rufaa waliyokata Mahakama ya Rufani dhidi ya mshtakiwa huyo.
“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa, huku tukisubiria taratibu za rufani tuliyomkatia mshtakiwa huu Mahakama ya Rufani,” amedai wakili Mrema.
Mrema baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi Sanga Melikiori, amehoji sababu ya mshitakiwa kutoletwa mahakamani ikiwa mahakama ilitoa amri ya kuletwa.
Melikiori ameomba mahakama tarehe ijayo mteja wake huyo apelekwe mahakamani hapo ili aje asikilize kesi yake.
Akijibu hoja hiyo, wakili Mrema amedai upande wa mashtaka haujapata amri ya kumleta mshitakiwa huyo mahakamani na pia kwa asili ya kesi hiyo inaweza kusikilizwa kwa njia ya video.
Hakimu Swallo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote, amekubaliana na hoja ya upande wa utetezi na kuamuru tarehe ijayo ya kesi hiyo, Dk Slaa aletwe mahakamani.
Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 4, 2025 kwa kutajwa na kesi hiyo ilisikilizwa mahakamani na siyo kwa njia ya video.
Hata hivyo, licha ya kesi hiyo kutajwa mahakamani, tayari Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania amewasilisisha kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi uliotolewa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambao ulielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa huyo pamoja na mambo mengine.
Kusudio hilo la kupinga uamuzi huo iliwasilishwa Mahakama ya Rufani na kusajiliwa katika mfumo Januari 30, 2025 na sasa inasubiriwa kupangiwa Jaji kwa ajili ya usikilizwaji.
Kutokana na DPP kuwasilisha kusudio hilo la kukata rufaa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haitaweza kuendelea na kesi ya msingi hadi hapo Mahakama ya Rufaa itakaposikiliza rufaa iliyokatwa na DPP na kuitolewa uamuzi, ndipo kesi ya msingi itaendelea Mahakama ya Kisutu.
Kwa hali hiyo, kwa kuwa mshtakiwa yupo rumande kutokana na upande wa mashtaka kuweka zuio la dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo, hivyo kesi hiyo itakuwa inatajwa kila baada ya siku 14 katika Mahakama ya Kisutu kama sheria inavyoelekeza kwa washtakiwa ambao hawana dhamana, kesi zao zinatakiwa kutajwa mahakamani kila baada ya siku 14.
Dk Slaa anakabiliwa na kesi ya Jinai namba 993 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao ya kijamii wa X.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Mwanasiasa huyo mkongwe anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai aliandika ujumbe uliosomeka kama ifuatavyo.
“Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya,…na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahili atatoa pesa…hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.”
Pia, aliandika katika akaunti maneno yalisomeka kama: “Samia toka muda mrefu haangaikii tena Maendeleo ya nchi anahangaikia namna ya kurudi Ikulu, na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe,” wakati akijua taarifa hizo ni za uongo.