Korti yaruhusu wanandoa kufanya mazungumzo na DPP

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu wanandoa wanaokabiliwa na kesi ya kusafirisha gramu 41.49 za dawa za kulevya aina ya heroini kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ili kuimaliza kesi yao.

Wanandoa hao ni Shabani Adamu na mkewe Husna Issa, pamoja na mtoto wao, Mussa Shabani, wote wakazi wa Manzese.

Jana Jumanne, Februari 18, 2025, Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, kuwa tayari wamepokea barua ya kufanya majadiliano.

Roida alidai kuwa wamepokea barua ya kufanya maridhiano na maombi hayo yaliwasilishwa na mshtakiwa wa kwanza kwa niaba ya wenzake.

“Kutokana na hali hiyo, tunaomba mahakama itupangie muda kwa ajili ya kuanza vikao vya majadiliano ‘Plea Bargain’,” alidai Roida.

Hata hivyo, washtakiwa hao kupitia wakili wao, Nehemia Nkonko, walidai kuwa taarifa hiyo ya kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi iliingizwa katika mfumo wa mahakama Januari 26, 2025.

Hakimu Mhini, baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, alitoa siku 14 kwa ajili ya upande wa mashtaka na ule wa utetezi kuanza majadiliano.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 3, 2025, kwa ajili ya kutajwa, na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 11, 2024, eneo la Manzese, ambapo wanadaiwa kukutwa na gramu 41.49 za heroini, kinyume cha sheria.

Related Posts