Mashujaa yazinduka, Azam ikibanwa Arachuga

MASHUJAA ikiwa kwenye Uwanja wa nyumbani wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma imejivua joho la unyonge baada ya kuzinduka na kupata ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Pamba Jiji, huku Azam ikiwa ugenini ilibanwa na Wagosi wa Kaya katika mechi za Ligi Kuu zilizopigwa jioni hii.

Mashujaa ilishuka uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kucheza mechi nane mfululizo bila kuonja ushindi, kwani mara ya mwisho kushinda ilikuwa Novemba 23 mwaka jana dhidi ya Namungo.

Katika mchezo huo, wenyeji walionekana kujiandaa vya kutosha kwa kufanuikiwa kuizima na kuitubulia  Pamba iliyotoka kushinda mechi tatu mfululizo tangu kurejea kwa Ligi hiyo mapema mwezi huu.

Mabao ya kila kipindi, moja likiwa likiwekwa kimiani na Hassan Hadji ‘Cheda’ dakika ya 35 aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Pamba, Yona Amos baada ya Danny Lyanga kukosa mkwaju wa penalti.

Penalti hiyo ilitokana na mshambuliaji  Jaffar Kibaya kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari na mwamuzi kuamuru mkwaju huo na uliookolewa Cheda alipata nafasi ya kuuzamisha, japo marudio ya Azam TV ilionekana alikuwa eneo la kuotea sambamba na Lyanga na kufanya wachezaji wa Pamba pamoja na benchi la ufundi kulilalamikia bao, lakini hakuna kilichobadilika.

Bao hilo lilidumu hadi mapumziko na katika kipindi cha pili dakika ya 62, Pamba ilijikuta ikipata pigo baada ya mchezaji wake, Abalkassim Suleiman kulimwa kadi nyekundu, ikiwa ni mara ya pili kwa msimu huu kuonyesha katika Ligi Kuu baada ya awali kupewa wakati akiwa Fountain Gate ilipokuwa ikiumana na Pamba.

Kitendo cha Pamba kucheza pungufu kiliwapa faida wenyeji ambapo dakika ya 83 waliandika bao la pili lililofungwa na David Ulomi kwa shuti kali akipokea pasi ya Jaffary Kibaya na kuihakikisha Mashujaa kupata ushindi huo baada ya awali kucheza dakika 720 bila kuonja raha hiyo.

Lakini kipigo hicho kimemaliza rekodi ya Pamba kucheza mechi tatu mfululizo ikigawa kipigo kwa kupoteza na kuifanya isaliwe na pointi 21 ikiwa nafasi ya 12 baada ya mechi 20, wakati wenyeji kwa matokeo hayo yameifanya itoke nafasi ya 13 na kuchupa nafasi ya sita ikifikisha pointi 23 kwa mechi 20.

Huo ulikuwa ni ushindi wa tano kwa Mashujaa, ikiwa pia na sare nane na ikipoteza michezo saba na kufunga mabao 17, huku yenyewe ikifungwa 18. Bao alililofunga Ulomi limemfanya afikishe manne hadi sasa katika ligi hiyo itakayofikia tamati Mei 15 mwaka huu.

Katika mchezo mwingine uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC ilishindwa kuendeleza wimbi la ushindi kwa kulazimishwa suluhu na wenyeji wao, Coastal Union na kuendelea kusalia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43 baada ya mechi 20.

Azam iliingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi iliyopita kwa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa, huku kwa upande wa Coastal Union ikihitaji ushindi baada ya mechi ya mwisho kuchapwa dhidi ya Pamba Jiji mabao 2-0.

Mchezo wa mwisho baina ya timu hizo uliopigwa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, ulikuwa wa Kombe la FA hatua ya nusu fainali uliopigwa Mei 29,2022 na kushuhudia Coastal Union ikishinda kwa mikwaju ya penalti 6-5.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza kwa msimu huu iliyopigwa Septemba 22, mwaka jana ambapo Azam C ilishinda bao 1-0 na matokeo hayo yameifanya Coastal Union kufikisha pointi 23 katika nafasi ya saba baada ya kucheza michezo 20, ikishinda mitano, sare nane na kupoteza saba, huku ikifunga  mabao 18 na kuruhusu 20.

Azam inarudi jijini Dar es Salaam sasa kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Simba utakaopigwa Jumatatu ijayo kwenye Uwanja wa KMC Complex, wakati Coastal itakuwa ugenini kuvaana na Namungo mchezo utakaopigwa Jumamosi ya Februari 23 kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Related Posts