Musoma. Mkazi wa Kijiji cha Busekela wilayani Musoma Mkoa wa Mara, Helment Turutumbi (45) hajulikani alipo baada kuchukuliwa na watu wasiojulikana ambao walifika kijijini hapo na kujitambulisha kama usalama wa taifa kutoka Dodoma.
Turutumbi ambaye ni mvuvi na mfanyabiashara wa dagaa katika mwalo wa Busekela, alichukuliwa na watu hao kijijini hapo Februari 14, 2025 saa 11 jioni.
Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amekiri kufahamu tukio hilo, na kuwa hadi sasa bado haijajulikana alipo Turutumbi.
Amesema tayari wameanza uchunguzi huku akitoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zitakazoliwezesha jeshi hilo kufahamu alipo Turutumbi ajitokeze kulisaidia Jeshi la Polisi.
“Hadi sasa hatujui huyu mtu (Turutumbi) yuko wapi na hatujajua lengo au sababu ya hao watu kumkamata kwani hayupo kwenye vituo vyetu vya polisi, tayari uchunguzi umeanza na tunaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili tuweze kujua alipo,” amesema Lutumo.
Akizungumza kijijini hapo Februari 18, 2025, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burungu, Matibabu Mbogora amesema siku ya tukio walifika watu watano akiwepo mwanamke mmoja ambao walijitambulisha kama watu wa usalama wa taifa na kwamba walikuwa wanamtafuta Turutumbi.
“Walifika hapa na kujitambulisha kisha wakanionyesha picha kuwa wanamtafuta huyo mtu, kwa vile ni mtu ambaye namfahamu nikawaambia ni mkazi wa hapa na shughuli zake anazifanyia hapa, ndipo wakasema wana shida naye,” amesema.
Mwenyekiti huyo amesema baada ya kujitambulisha aliwaelekeza alipo Turutumbi kisha wakaenda na kumkamata akiwa mwaloni anaedelea na shughuli zake na kuondoka naye, bila kutoa maelezo zaidi juu ya wapi wanampeleka wala kosa lake.
Amesema kabla ya mfanyabishara huyo kukamatwa, mwenyekiti huyo aliwasiliana na mtendaji wa kijiji na kumweleza juu ya ujio wa watu hao, mtendaji alipiga simu katika Kituo cha Polisi Busekela kujua kama walikuwa na taarifa juu ya ujio wa watu hao.
“OCD alimwambia hana taarifa zozote juu ya uwepo wa watu hao, ndipo mtendaji alipoamua kuja eneo la tukio lakini alipofika alikuta tayari jamaa ameshakamatwa na walikuwa kwenye harakati za kuondoka naye,” amefafanua.
Mbogora amesema tangu siku hiyo hawajapata taarifa juu ya alipo mkazi huyo na kwamba wamejaribu kufuatilia polisi bila mafanikio.
Mke wa mfanyabishara huyo, Pendo Turutumbi amesema hadi sasa hajui mume wake alipo na ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili kujua alipo na hatimaye kurejeshwa nyumbani.
“Sikuwahi kusikia kama mume wangu ana ugomvi na mtu yeyote wala kuwa na kesi yoyote mahali popote sasa, sijui hawa watu waliomchukua wana nia gani,” amesema mama huyo wa watoto watano.
Amesema kufuatia kutoweka kwa mume wake, familia yake inaishi kwa wasiwasi kwani hawajui lengo la watu hao lilikuwa ni nini.
Amesema pia wanaishi katika mazingira magumu hasa ikizingatiwa kuwa familia ilikuwa ikimtegemea kwa ajili ya mahitaji ya kila siku.
“Mimi ni mama tu wa nyumbani, mume wangu kama baba wa familia yeye ndiye alikuwa anajua tunakula nini na kuvaa nini, sasa hayupo maisha yamekuwa magumu naomba Serikali inisaidie aweze kurudi,” amesema.
Amesema alionana na mume wake saa moja kabla ya kuchukuliwa na watu hao baada ya yeye kwenda eneo la mwaloni kwa lengo la kumuaga, kwa kuwa alikuwa anakwenda sehemu kwa ajili ya kununua mahitaji ya nyumbani.
Amesema akiwa anatoka kwa mume wake alikutana na gari jeupe likiwa linaelekea uelekeo wa mwaloni, hakulitilia shaka kwani ni jambo la kawaida magari kufika katika eneo hilo kutokana na shughuli za uvuvi na uuzaji wa dagaa unofanyika.
Amesema kabla ya kurejea nyumbani alifuatwa na mtoto wake ambaye alimueleza juu ya kukamatwa kwa baba wake na kwamba aliporudi mwaloni hakumuona tena, kwa kuwa watu hao walikuwa wameondoka naye.
Malima Ndaro ambaye alishuhudia tukio hilo amesema wakiwa wanacheza karata mwaloni, watu hao walifika na kuwaslimia kisha kusema walikuwa na shida na Turutumbi.
“Walichukua simu yao na kumuonyesha namba ambayo mimi sikuiona, wakamuuliza kama anaitambua, akasema ndiyo wakamuuliza iko wapi, wakamwambia wanaitaka kisha wakaondoka naye kwenda nyumbani kwake,” amesema.
Amesema walipofika nyumbani watu hao walichukua simu mbili ambazo hata hivyo hakufahamu ni za akina nani, kisha wakaondoka naye na kuelekea kusikojulikana.
Amina Salum, amesema hadi sasa hawajui chanzo cha mfanyabiashara huyo kukamatwa kwani hawakuwahi kusikia kama ana ugomvi ama kutofautiana na mtu yeyote.
“Ni mtu mpole tangu nimemfahamu sijawahi kumuona akigombana na mtu na hata kuhusishwa na vitendo vya kihalifu, kwa kweli sijui shida ni nini,” amesema.