Mifumo mitano ya Tehama kukuza uchumi wa kidijitali

Arusha. Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, katika kipindi cha mwaka 2024/25 imewezesha ujenzi wa mifumo mitano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), itakayochangia maendeleo ya nchi hususani ukuzaji wa uchumi wa kidijitali.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi, akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, leo Jumatano Februari 19, 2025.

Ameitaja mifumo huyo kuwa ni mfumo wa ubadilishanaji taarifa (Jamii X-change na ZanXchange), mfumo wa utambuzi kidijitali, Jamii Namba, mfumo wa utambuzi wa wateja (e-KYC), mfumo wa malipo ya kidijitali jamii Pay na mfumo wa usajili na uwezeshaji wa wadau wa ikolojia ya tafiti.

“Baraza hili linapaswa kufanya kazi kwa ufanisi na kuhakikisha kwamba dhamana iliyokabidhiwa Wizara na Serikali ya kusimamia sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inafikiwa na inachangia maendeleo ya nchi yetu, kuharakisha kufikiwa kwa uchumi wa kidijitali,” amesema.

Ametaja mafanikio mengine ni ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 316 wa Kada ya Tehama katika ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Vyuo Vikuu mbalimbali vilivyopo nchini Uingereza, Ujerumani, Malaysia, Uturuki na Sweden.

Kadhalika amesema Wizara inasimamia ujenzi wa Chuo Mahiri cha Tehama (DTI) kwa kushirikiana na Benki ya Exim (Korea) pamoja na Benki ya Dunia (WB) ambapo Chuo hicho kitakachojengwa Nala jijini Dodoma, kitagharimu zaidi ya Dola za Marekani 175.8 milioni.

“Kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi Serikali inafanya maboresho ya Mkakati wa Taifa wa Usalama wa Mtandao pamoja na kusimamia zoezi la uhuishaji wa mfumo wa takwimu za makosa ya mtandao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,” amesema.

Kuhusu mkutano huo, amesema Baraza hilo ni kiungo madhubuti kati ya menejimenti na wafanyakazi na kuwataka watumishi kutimiza wajibu wao ili kuwezesha haki zao kupatikana kwa kuwa hakuna haki bila wajibu.

Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Khamis Abdulla, aliwataka watumishi hao kutunza siri na nyaraka za Serikali kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa.

“Wafanyakazi tuendelee kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na tuwe na ubunifu wa hali ya juu hasa ikizingatiwa teknolojia inakua kila siku. Tuna wajibu wa kutunza siri na nyaraka za serikali kwa maslahi mapanya ya nchi,” amesema.

“Ni kosa kuvujisha siri kwenye mitandao ya kijamii au kwa watu wasiohusika, sote tunatambua taratibu za utumishi wa umma tuzifuate,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) tawi la Wizara hiyo, Laurencia Masigo alisisitiza ushirikianao kati ya waajiri na watumishi kwani bila ushirikiano hawataweza kutatua changamoto pamoja na kusimamia utekelezaji wa majukumu yao.

Related Posts