Jopo la majaji jijini Los Angeles, Jumanne, Februari 18, limemuachia huru rapa maarufu kwa jina la A$AP Rocky baada ya kumkuta hana hatia katika mashitaka mawili ya uhalifu ya kushambulia kwa silaha yaliyokuwa yakimkabili kutokana na tukio la mwaka 2021 dhidi ya msanii mwenzake wa hip-hop huko Hollywood, Marekani.
Rocky, ambaye ni mpenzi wa mwanamuziki Rihanna na baba wa watoto wao wawili, mara baada ya kutolewa hukumu, aliruka kwa furaha na kujitupa moja kwa moja kwa Rihanna na mashabiki wake mahakamani hapo. Alikumbatiana na wafuasi wake huku shangwe kubwa zikisikika ndani ya mahakama.
“Asanteni kwa kuniokoa,” Rocky aliwaambia majaji 12 waliotoa uamuzi huo.
Rapa huyo alishtakiwa kwa kumuelekezea bastola aliyekuwa rafiki yake, Terell Ephron, wakati wa ugomvi mkali, kisha kufyatua risasi mbili kuelekea Ephron katika mzozo wa pili. Matukio yote mawili yalitokea tarehe 6 Novemba 2021.
Kwa mujibu wa Ephron, alipata jeraha dogo baada ya risasi kugusa vifundo vya vidole vyake.
Hata hivyo, mawakili wa Rocky walitetea kwamba silaha iliyohusika ilikuwa ni bastola ya maigizo iliyotumiwa kwenye video ya muziki na kwamba ilifyatua risasi bandia. Pia walidai kuwa Ephron ndiye aliyekuwa mchokozi katika tukio hilo.
“Tunamshukuru Mungu kwanza,” Rocky alisema nje ya mahakama akiwa amesimama kati ya Rihanna na wakili wake. “Hili ni jambo la kushangaza.”
“Najihisi mwenye bahati na nashukuru kuwa huru sasa hivi na kuzungumza nanyi,” aliongeza.
Rihanna alihudhuria mahakamani mara kadhaa wakati wa kesi hiyo, na wakati mwingine aliwaleta mahakamani watoto wao, RZA (miaka 2) na Riot (mwaka 1), kushuhudia hoja za mwisho za kesi hiyo.
ASAP ALIVYOMRUKIA RIHANNA BAADA YA KUSHINDA KESI