Musoma. Mahakama Kuu imetoa kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama (judicial review) kwa aliyekuwa muuguzi daraja la II, Chacha Nyakahemba, ili aweze kupinga kuachishwa kazi kwa kuwa ana elimu ya darasa la saba.
Nyakahemba alifungua maombi namba 29058 ya mwaka 2024 dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mjibu maombi wa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kama mjibu maombi wa pili katika kesi hiyo.
Katika uamuzi wake alioutoa Februari 18, 2025 na kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama leo Jumatano Februari 19, 2025, Jaji Marlin Komba wa Kanda ya Musoma, ametoa kibali hicho na kumpa siku 30 kufungua maombi hayo ya mapitio.
Kulingana na hati ya kiapo, Nyakahemba anaeleza kuwa mwaka 2007 aliajiriwa kama muuguzi daraja la pili na wakati anaajiriwa, alitakiwa kuwa na elimu ya darasa la saba, pamoja na sifa zingine, ili kuingia katika utumishi wa umma.
Mei 15, 2023, Ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ilimwachisha kazi kwa tuhuma kuwa kwa kiwango cha elimu alichonacho, kilimnyima sifa za kuwa mtumishi wa umma na kuwa alipotosha kuhusu elimu yake.
Alikata rufaa kwenye Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) bila mafanikio na baadaye akakata rufaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye naye alibariki maamuzi hayo na hivyo kumlazimu kukimbilia kortini kuomba kibali hicho.
Wajibu maombi kupitia kwa wakili wa Serikali, Anesius Kamugisha alieleza kwa kifupi tu kuwa amepitia maombi hayo na kuona yaliwasilishwa ndani ya muda na kuonyesha tatizo lilipo, hivyo hawana pingamizi akipewa kibali.
Katika uamuzi wake, Jaji Komba amesema amepitia maombi hayo na mawasilisho ya pande zote mbili na anaona shauri hilo linaangukia katika sheria ya utawala (administrative law) ambayo inahusu matendo na maamuzi ya mamlaka ya umma.
Akinukuu uamuzi wa mahakama katika shauri linalofanana na hilo, Jaji Komba anasema mapitio ya mahakama ni silaha muhimu mikononi mwa majaji, ambayo raia wanaweza kuitumia kupinga maamuzi kandamizi ya kiutawala.
Jaji amesema kuna mambo ya msingi ya awali ambayo mahakama inapaswa kuyazingatia wakati wa kutoa kibali cha kufungua maombi ya mapitio, ikiwamo kwamba muombaji yuko ndani ya muda wa miezi sita anapowasilisha maombi.
“Katika maombi yaliyopo mbele yangu, muombaji anakusudia kupinga uamuzi wa Rais kubariki kufukuzwa kwake kazi, ambao ulianzia kwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Tarime na Tume ya Utumishi wa Umma,” amesema Jaji.
“Baada ya kupitia hati ya kiapo cha muombaji, naungana na Anesius Kamugisha na wakili wa Serikali kwamba shauri hili linafaa kwa ajili ya mapitio ya mahakama kwa kuwa limekidhi vigezo vyote vya kisheria,” anaeleza Jaji.
Jaji akasema kutokana na msimamo huo, anaona kuna hoja zinazofaa kusikilizwa na mahakama, hususan kwenye suala la sifa ya kielimu ya kuajiriwa kwake, hivyo anampa mwombaji siku 30 kuanzia tarehe ya uamuzi, awe amefungua maombi yake.