Morogoro. Mwanazuoni mkongwe na mwalimu wa dini ya Kiislamu Mkoa wa Morogoro, Sheikh Ayubu Muwinge amefariki dunia Jumanne, Februari 18, 2025 katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.
Mwili wa Sheikh Muwinge utazikwa leo Jumatano, Februari 19, 2025 katika makaburi ya Kola yaliyopo Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Mwananchi, mdogo wa marehemu, Hahibu Muwinge amesema hali ya afya ya kaka yake ilianza kuwa mbaya mwishoni mwa mwaka jana na alikuwa akilazwa mara kwa mara kwenye hospitali mbalimbali mkoani humo.
Amesema juzi Jumatatu hali ilizidi kuwa mbaya na walimpeleka hospitali na jana akafariki dunia.
“Sheikh Muwinge atazikwa leo saa saba mchana katika makaburi ya Kola yaliyopo Manispaa ya Morogoro ambapo viongozi mbalimbali wa dini na Serikali wanatarajia kushiriki mazishi hayo,” amesema Habibu.
Sheikh Muwinge enzi ya uhai wake alitembea maeneo mbalimbali nchini kusoma na kufundisha dini. Baadhi ya mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Pwani na Zanzibar na mpaka anafariki dunia alikuwa ni muasisi wa Taasisi ya kufundisha dini inayoitwa Asasudin Madrasa, yenye makazi yake mkoani Morogoro.
Muwinge amesema marehemu kaka yake pia aliwahi kuwa kiongozi wa Baraza Kuu la Kiislamu Tanzania (Batwaka) lakini pia mwalimu wa iliyokuwa shule ya sekondari ya Kiislamu ya Jabar Hilla mkoani Morogoro na viongozi wengi wa Serikali na diini wamepita kwenye mikono yake.
Kaimu imamu wa msikiti wa Kingo Manispaa ya Morogoro, Sheikh Jafari Jaka amesema masheikh wengi na wenye majina makubwa wamefundishwa na Sheikh Muwinge kupitia madrasa mbalimbali alizofundisha kipindi cha uhai wake.
Sheikh Jaka ambaye naye ni miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Muwinge amesema mbali ya kuwa mwanazuoni na mwalimu wa dini, Sheikh Muwinge alishika nafasi mbalimbali ikiwemo mwenyekiti wa baraza kuu linaloshughulika na Uislamu ambalo mwenyekiti wa kitaifa ni Sheikh Ponda Issa Ponda.
Amesema nafasi nyingine alizowahi kushika Sheikh Muwinge ni pamoja na uimamu wa msikiti maarufu mjini Morogoro unaojulikana kwa jina la ‘Mungu Moja’ na pia mpaka anafariki alikuwa akiendelea kufundisha dini kwenye misitiki na madrasa mbalimbali mkoani hapa.
“Mimi mwenyewe nimeijua dini kupitia marehemu Sheikh Muwinge, yeye ndiye aliyenifindisha kusoma ‘alifu’ na kwenye Uislamu alifu ndio msingi kwa kusoma Quran, na mpaka leo hii nimekuwa sheikh mzuri ni kwa sababu ya mchango wake,” amesema Jaka.
Kifo cha Sheikh Muwinge ni pigo la pili kwa Waislamu wa mkoa wa Morogoro baada ya kufariki kwa Qadhi wa Mkoa Sheikh Mussa Bolingo ,miezi mitatu iliyopita.
Baadhi ya Waislamu mkoa wa Morogoro wamesema kifo cha mwanazuoni huyo ni pigo kwa Waislamu wa mkoa wa Morogoro hasa kutokana na mchango wake katika kufundisha elimu ya duni.
Mmoja wa Waislamu wa Mkoa wa Morogoro, Aziz Msuya amesema Sheikh Muwinge alikuwa ni mwalimu wa dini ya Kiislamu ambapo masheikh wengi ndani na nje ya mkoa wa Morogoro wamepita kwenye mikono yake.
Msuya amesema mbali ya kuwa mwalimu wa dini, pia aliweza kuendesha haraka nyingi za kuupigania Uislamu na Waislamu na aliweza kushiriki kwenye mabaraza na makongamano mengi ya kiislamu hapa nchini.