‘No reforms, no elections’ yawaweka Chadema njiapanda

Dar es Salaam. Kampeni inayoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya ‘No reforms, no elections’ ikimaanisha “Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi”, imewaweka njiapanda baadhi ya viongozi na makada wa chama hicho.

Wanaobaki njiapanda, ni makada ambao kwa namna moja au nyingine wana nia ya kugombea katika uchaguzi mkuu Oktoba 2025 kusaka udiwani, ubunge na hata urais, ambao wanaingia hofu ya kukosa fursa hiyo.

Makada hao hawajui iwapo wajiandae kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho au waendelee kuwa wasikilizia kauli ya chama iliyosisitizwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kwamba kwa sasa nguvu kubwa zinaelekezwa kwenye kupigania mabadiliko ya mifumo ya kiuchaguzi na si vinginevyo.

Wakati Chadema ikiendelea kujiuliza na kupigania mabadiliko, vyama vingine vinaendelea na maandalizi ya uchaguzi. Mathalan, ACT Wazalendo kimeshatangaza wanaotaka kuwania udiwani, ubunge, uwakilishi na urais wajitokeze na kutangaza nia.

Tayari Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othuman Masoud ameweka nia kuwania urais Zanzibar na Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu ametamgaza kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chama tawala CCM kimekwishapitisha wagombea wake wa uraia; Rais Samia Suluhu Hassan (muungano) na Dk Hussein Ali Mwinyi (Zanzibar). Dk Emmanuel Nchimbi amepitishwa kuwa mgombea mwenza wa Rais wa Tanzania.

Kwa nyakati tofauti Lissu aliyeshika wadhifa huo Januari 22, 2025, amekuwa akisisitiza dhana hiyo, kuwa iwapo hakutakuwa na mabadiliko kwenye mfumo wa kisheria, Chadema itafanya kila linalowezekana kuhakikisha uchaguzi haufanyiki.

“Hatuzungumzii kususuia uchaguzi, hatutasusia bali tutaenda kuwaambia Watanzania, jumuiya ya kimataifa na walimwengu kwamba kama CCM na Serikali hawako tayari kufanya mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi ili kuwepo chaguzi huru na haki, uchaguzi wa mwaka huu usifanyike kabisa,” alisema Lissu katika moja ya hotuba zake.

Msimamo huo umemwibua Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi ambaye anasema kwa ajuavyo yeye mageuzi yalikwishafanyika.

“Mimi nimeona mageuzi yapo, sasa kama mwenzangu hayaoni, hata ukitwambia hakuna uchaguzi, wewe unayezuia kwani ndiye unayechagua pekee? Uchaguzi unafanywa na wananchi na ndio wanaopiga kura,” amesema Maswi.

Msimamo huo unaokuja ikiwa imebaki miezi michache kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu wa wabunge, madiwani na urais, unawaacha makada n ahata viongozi waandamizi katika wakati mgumu, hasa pale wanapoona vyama vingine vinafanya maandalizi.

Pia, Mwananchi inazo taarifa za kwamba wapo wana Chadema wanaotaka chama hicho kiingie katika uchaguzi ili kisije kufa, endapo hakitashiriki kwa sababu kitakosa ruzuku za kujiendesha.

Taarifa zinadai baadhi ya makada hao walishawekeza kwenye maandalizi na wanaona kuna mwanga wa chama hicho kuibuka kidedea kutokana na mwenendo wa siasa, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2020.

“Unajua wengi kwenye chama tunataka tushiriki uchaguzi, tumejipanga muda mrefu lakini kauli za mwenyekiti kwa kweli zinatuvuruga sana. Hatujui tuendelee kujipanga na timu zetu au tusubiri,” amesema mjumbe wa kamati kuu na mwenyekiti wa kanda, aliyeomba jina lake lisitajwe.

Hoja hiyo inazungumzwa na mwenyekiti mmoja wa mkoa wa Chadema anayesema: “Tusipokuwa makini tunakwenda kukizamisha hiki chama. Wenzetu wanajiandaa huko, sisi tunapigania ‘no reform’ no election’, ni sahihi lakini na maandalizi yanapaswa kufanyika.”

Kiongozi mwingine anayetokea kanda ya kati amesema: “Kwenye suala la No reforsm no elections si wote wanaounga mkono, bali wengi wanataka chama kishiriki uchaguzi kwa sababu walishawekeza kwenye maandalizi ya uchaguzi wa udiwani na ubunge, hivyo msimamo huu unatuweka wengi wetu njia panda.”

Kampeni hiyo licha ya kuwagawa makada hao, ilibuniwa na kamati kuu ya Chadema ilioyomaliza muda wake chini ya Freeman Mbowe na baadaye likabarikiwa na Baraza Kuu na Mkutano Mkuu ulioenda sambamba na uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama uliokuwa na vuta nikuvute.

Kutokana na mvutano na mgawanyiko uliokuwepo wakati wa uchaguzi, suala la “No reform No Election” sasa ni kama limeachwa kama mzigo na kipimo cha wa uongozi mpya.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, leo Jumatano, Februari 19, 2025, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesisitiza kipaumbele cha chama hicho kwa sasa ni kaulimbiu hiyo ya ‘No reform, No Election.’

Mnyika ambaye amesisitiza hawako tayari kuhamisha mjadala kutoka kwenye kampeni hiyo, badala yake wanataka majibu ya Serikali kuhusu hitaji lao la mageuzi kabla ya uchaguzi.

 “Msimamo na kipaumbele chetu kwa sasa, ni kushinikiza mageuzi kabla ya uchaguzi na hatutaki kuhamisha mjadala kwenye hilo,” amesema Mnyika.

Kwa mujibu wa mtendaji mkuu huyo wa Chadema, msisitizo wao ni kuzitaka taasisi zote nchini ziiulize Serikali kupata majibu ya mpango ilionao kuhusu mageuzi yanayohitajika.

“Hata wewe nenda kaiulize Serikali itupe majibu kuhusu lini na ina mpango gani na mageuzi ya kisera na kisheria kuhusu uchaguzi, hatuwezi kuhamisha mjadala kwa kuongelea maandalizi ya uchaguzi, maana kipaumbele ni mageuzi,” amesisitiza.

Kwa umuhimu wa kampeni hiyo, Mnyika amesema chama hicho kitaendelea kutoa elimu kwa wanachama wake na wadau wengine hadi waelewe msimamo huo na nini hasa wanalenga.

‘Pengine hawajajiandaa’

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi amesema anachofahamu mwaka jana Bunge lilifanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi.

Sambamba na hilo, Maswi amesema Rais Samia kupitia falsafa yake ya 4R, ameleta ushirikishwaji wa wadau, vikiwemo vyama vya siasa katika mageuzi ya kisera na kisheria kuhusu uchaguzi.

Katika mazingira hayo, Maswi amesema anayesema ‘no reform no election’ anapaswa kuulizwa anataka nini la ziada, na pengine analalamika kwa sababu hakujiandaa kwa uchaguzi.

“Mtu akikwambia ‘no reform, no election’ muulize anachotaka nini, ujue mtu akiwa hajajiandaa, haishiwi sababu na malalamiko,” amesema Maswi.

Kwa mujibu wa Maswi, pamoja na mambo mengine  4R (ustahimilivu, mageuzi, kujenga upya na maridhiano) inahusu mageuzi, kama wanaodai mageuzi hayo ni waungwana wangeomba kukutana na Serikali kujadiliana mabadiliko wanayohitaji ili yafanyike kwa masilahi ya nchi.

 “Sasa unaposema no reform no election, mageuzi yatafanyika ukiwa nyumbani? Anayetaka mageuzi aje akae na Rais Samia, ameruhusu maridhiano kupitia 4R, tujadiliane tufanye hilo kwa masilahi ya nchi,” amesema.

Amesisitiza moja ya kazi kubwa walizonazo ndani ya Serikali ni kukaa pamoja na kufanyia kazi na yeyote anayetaka mabadiliko ya nchi, kama ilivyofanyika kwa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

“Rais wa TLS (Boniface Mwabukusi) si amekuja ameeleza maeneo yanayohitaji mageuzi, tumejadiliana na tunaendelea kujadiliana ili kufikia hatua inayotarajiwa kwa masilahi ya nchi, unaona analalamika? Kwa sababu amekuja tumejadiliana, huo ndio uungwana na ndio njia sahihi.

Kwa kuwa Rais Samia ameruhusu maridhiano, Maswi amesema anayetaka mageuzi yoyote, yakiwemo ya kisera na kisheria, akae na mamlaka wajadiliane, hakuna aliyekataa hilo ndani ya Serikali.

“Mimi nimeona mageuzi yapo, sasa kama mwenzangu huyaoni, hata ukituambia hakuna uchaguzi, wewe unayezuia kwani ndiye unayechagua pekee? Uchaguzi unafanywa na wananchi na ndio wanaopiga kura. Wewe mwandishi ukiambiwa usikichague chombo chako cha habari utakubali?” amesema.

Related Posts