Polisi, RC, Chadema walivyojadili madai kutekwa Katibu wa Bavicha

Mwanza. Kamati ya ulinzi na usalama mkoani Mwanza imekanusha tuhuma za kuhusika katika kutoweka kwa Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Mwanza, Amani Manengelo ambaye inadaiwa alichukuliwa na watu waliojitambulisha ni maofisa wa polisi.

Manengelo anadaiwa kutoweka Februari 14, 2025, akiwa nyumbani kwa rafiki yake wa kike, Pendo. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema watu watatu, akiwemo Pendo, wanashikiliwa kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.

Akizungumza na viongozi wa Chadema waliojitokeza leo Jumatano Februari 19, 2025, katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kufuatilia hatima ya Manengelo, Mkuu wa mkoa huo, Said Mtanda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, amesema Jeshi la Polisi halihusiki na kutoweka kwake.

“Tumefanya uchunguzi na hakuna taarifa zinazoonyesha kuwa Manengelo anashikiliwa katika kituo chochote cha polisi hapa Mwanza. Aidha, waliomchukua kutoka kwa mtu anayefahamika kwa jina la Pendo si maofisa wa polisi,” amesema Mtanda.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Boniface Nkobe (wapili kushoto) akimueleza jambo Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbrod Mutafungwa baada ya kikao cha kujua hatma ya alipo Katibu wa Bavicha Mkoa wa Mwanza, Amani Manengelo aliyetoweka Februari 14, 2025 wilayani Misungwi. Picha na Saada Amir

Ameongeza kuwa Pendo hakutoa taarifa mara moja kuhusu kutoweka kwa Manengelo hadi Februari 17, ambapo mwenyekiti wa Chadema wa wilaya aliwasilisha taarifa polisi.

Amesema kwa sasa, timu maalumu ya uchunguzi kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi ipo Mwanza ikifuatilia tukio hilo kwa njia za kisayansi, huku akiwataka wanachama wa Chadema kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa taarifa zitakazosaidia uchunguzi.

Akizungumza baada ya kikao kilichotumia takribani saa moja kati ya Mtanda, kamati ya ulinzi na usalama na makada hao wa Chadema, Kamanda Mutafungwa amesema; “Mpaka sasa tunapoongea tunawashikilia watu watatu ambao wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hili la kupotea kwa bwana Amani.”

Amesema wataendelea kuwahoji watu mbalimbali waliokuwepo kwenye mazingira ambayo Amani alitoweka wakiwemo ndugu na majirani.

“Yamekuwepo maneno yanayotajwa kuwa wanaohusika ni jeshi la polisi, nipende kusema kwamba jeshi la polisi halihusiki na tukio hilo hata kidogo hata wale mashahidi ambao wameendelea kuhojiwa hakuna anayetaja kwamba amekuwepo ofisa wa jeshi la polisi, kwa hiyo jeshi la polisi haliusiki kwa namna yoyote ile na jambo hilo, sisi tupo katika upande wa kufuatilia ili tupate ukweli,” amesema.

Mutafungwa amesema kikao hicho kilifanyika na kumalizika kwa utulivu, huku akiwahimiza wananchi na makada wa Chadema kushirikiana na vyombo vya usalama ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.

Aidha, ametoa onyo kwa wale wanaopanga kufanya maandamano ambayo yalitangazwa jana, akieleza kuwa hayana uhalali wowote. Amesema Jeshi la Polisi limejiandaa tangu asubuhi kudhibiti matukio yoyote ya uvunjifu wa sheria au fujo zitakazojitokeza.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Boniface Nkobe (wapili kushoto) akimueleza jambo Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbrod Mutafungwa baada ya kikao cha kujua hatma ya alipo Katibu wa Bavicha Mkoa wa Mwanza, Amani Manengelo aliyetoweka Februari 14, 2025 wilayani Misungwi. Picha na Saada Amir

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Boniface Nkobe amesema baada ya kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu suala hilo, Mkuu wa Mkoa aliwaalika kwa mazungumzo.

Katika kikao hicho, amewahakikishia ushirikiano na kutoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kutoweka kwa Manengelo.

“Nafikiri tunapaswa kuwa na subira ili Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wake kwa maelekezo ya mkuu wa mkoa. Tunahitaji kupata maelezo sahihi kuhusu alipo na kile kilichomsibu. Kwa sasa, hatujui sababu ya kukamatwa kwake, hatufahamu alipo, tunachojua ni kwamba ametoweka. Tunahitaji kumpata kwanza, kisha tutaelewa zaidi,” amesema Nkobe.

Kabla ya kikao hicho, kulikuwa na ulinzi mkali katika barabara mbalimbali za Jiji la Mwanza, ikiwemo ile inayopita karibu na Ofisi ya Kanda ya Victoria ya Chadema eneo la Nyegezi.

Vilevile, barabara inayoelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilizingirwa na askari wa polisi wenye silaha, ambao walikuwa wakihoji na kukagua watu waliokuwa wakielekea eneo hilo ili kudhibiti hali ya usalama.

Related Posts