Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameitaka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) itilie mkazo malengo yake ya kutoa huduma na uwezeshaji, badala ya kuweka kipaumbele utozaji tozo katika shughuli za mionzi.
Kauli yake hiyo inatokana na kile alichofafanua, licha ya TAEC kuwa na wajibu wa utozaji tozo katika shughuli za mionzi, isijikute inasahau malengo mengine na hatimaye kuwa kikwazo badala ya kuwezesha.
Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Jumatano Februari 19, 2025 wakati akizundua Bodi ya TAEC baada ya kuiteuwa.
Amesema kwa hali ilivyo, tume hiyo kwa sasa inachanganya lengo la usimamizi na kukusanya tozo, kiasi kwamba taasisi zinazoshughulika na mionzi zinakuwa na wakati mgumu.
“Tayari kuna Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wengine mnapoweka tozo muhakikishe zinakuwa zile ambazo zinawezesha mambo yenu na sio kuwa kikwazo,” amesema.
Katika maelezo yake, amesema kuna wakati mzigo unapelekwa kwenye nchi ambazo haitoi sharti la ukaguzi wa mionzi, lakini TAEC inalazimisha kukagua ili ipate tozo.
“Kwenye kukagua kuna tozo, usipokagua unapoteza, kwa hiyo unakuta lengo la tozo linazidi lengo la usimamizi,” amesema huku akisisitiza haja ya kuangalia upya jambo hilo.
Profesa Mkenda amesema pamoja na tume hiyo kutumia vema fedha za tozo inazokusanya, lakini haipaswi kutoza kiasi cha kuweka vikwazo katika mazingira ya biashara.
“Tukumbuke kazi yetu vile vile ni kuwezesha na sio kuwa kikwazo cha shughuli za biashara. Kwa hiyo hili bodi tunawaomba mliangalie lengo letu kubwa sio tozo ni kusimamia, tozo ni nyenzo tu ya kuendesha mambo yetu,” amesema.
Sambamba na hilo, ameiagiza bodi hiyo kuweka kipaumbele ufadhili wa masomo ya mionzi kwa Watanzania ili kuongeza idadi ya wataalamu hao nchini.
Amesema inapaswa kuhakikisha inaanza na watumishi ndani ya tume hiyo, kisha vyuo vikuu na hatimaye Watanzania kwa ujumla wake.
Kwa sababu ya umuhimu wa hilo, ameipa bodi hiyo mamlaka ya mwisho ya kuwachagua wanafunzi watakaokidhi vigezo vya kupata ufadhili huo.
Amesema wanaopaswa kwenda ni wanafunzi wazuri ili wanapohitimu wahakikishe wanafadhiliwa kuendelea na shahada ya uzamivu.
Waziri huyo pia, ameitaka tume hiyo kuimarisha uhusiano wake na vyuo vikuu hasa kwenye masuala ya utafiti.
Kwa sababu vyuo mara nyingi vinakosa fedha za kufadhili tafiti, ametaka TAEC ihakikishe wakati mwingine inapokuja na bajeti ifanikishe hilo.
Mwenyekiti wa Bodi TAEC, Profesa Joseph Msambichaka, amesema amekiri aghalabu wanapokuwa ndani ya tume wanachoona ni kiasi cha tozo wanachopata.
Amesema kwa maelekezo hayo ya Profesa Mkenda, inabidi waangalie wanachotakiwa kutoa hasa ni huduma na mkazo uwekwe kwenye eneo hilo, badala ya kukusanya zaidi.
“Hilo tutalifanyia kazi kuhakikisha tunatoa huduma kiwango kinachomridhisha kila mtu,” amesema.
Amesema wanachotakiwa kufanya ni kuwezesha shughuli zinazoendelea badala ya kuwa kikwazo cha shughuli zinazohusiana na mionzi.
Kuhusu ufadhili wa masomo, amesema watahakikisha uongozi unalisimamia ili lipate msukumo unaokusudiwa.