Singida BS yaleta fundi Mhispania, Tambwe akipewa umeneja

SAA chache tangu ilipotoka kucheza na Yanga na kupoteza kwa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, mabosi wa Singida Black Stars umemtangaza kumshusha fundi kutoka Hispania, Juan Carlos Magro Oliva kuwa kocha msaidizi wa kikosi hicho akisaidiana na kaimu Kocha mkuu, David Ouma.

Ouma alikaimishwa nafasi hiyo kuchukua mikoba ya aliyekuwa kocha mkuu, Miloud Hamdi aliyejiunga na Yanga baada ya Sead Ramovic kuitema ghafla timu hiyo na kuibukia CR Belouizdad ya Algeria.

Taarifa ya kuboreshwa kwa benchi hilo la ufundi la Singida BS imetolewa asubuhi hii, ili kuunga na makocha waliopo ambao wameifanya timu hiyo kuwa nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 37 baada ya mechi 20.

Juan mwenye Leseni ya UEFA Pro alizaliwa Machi 26, 1976 huko Valencia Hispania huku akifanya kazi katika timu za Be1 NFA Jugend, Sarawak FA, Leiknir Reykjavik (U-19), Gibraltar United FC, Berekum Chelsea FC, BE1 National Football Academy na Guangxi Pingguo (U-21).

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na uongozi wa kikosi hicho, ilieleza Juan atasaidiana na Ouma, huku kwa upande wa Muhibu Kanu aliyekuwa kocha msaidizi namba moja ndani ya timu hiyo kwa sasa atakuwa ni msaidizi namba mbili.

Pia, uongozi wa timu hiyo umemuongeza aliyekuwa mshambuliaji nyota wa zamani wa Yanga na Simba, Amissi Tambwe ili awe meneja wa kikosi hicho, huku Fredy Chalamila akihamishiwa kwenye nafasi ya Mratibu mkuu wa klabu zote kikosini humo.

Tambwe anakumbukwa na mashabiki kwa soka alililolipiga akiwa na klabu kongwe za Simba na Yanga na kutwaa misimu miwili tuzo ya Mfungaji Bora kabla ya kuichezea DTB iliyokuja kufahamika kama Singida Big Stars iliyoungana na Fountain Gate na kuwa Singida FG.

Tambwe amewahi pia kucheza soka la kulipwa Oman na Djibouti kabla ya kurejea nchini kuichezea DTB na kuipandisha daraja kabla ya kuitwa Singida Big Stars.

Related Posts