NA VICTOR MASANGU, PWANI
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani imetumia kiasi cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya kununua vifaa na mahitaji mbali mbali kwa ajili ya kutoa msaada kwa jamii pamoja na maeneo mbali mbali ikiwemo sekta ya afya pamoja na sekta ya elimu ikiwa ni moja ya kurudisha kwa jamii kwa kile ambacho wanakikusanya katika suala zima la ukusanyaji wa mapato.
Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Masawa Masatu ameyabainisha hayo wakati wa ziara maalumu ya kwenda kutoa misaada mbali mbali kwa jamii ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha kwamba wanaendelea kudumisha mahusiano mazuri kwa jamii inayowazunguka pamoja na walipa kodi.
“Kama tunavyofahamu serikali ya awamu ya sita kupitia kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa na kampeni maalumu kwa lengo la kuhakikisha kwamba TRA inakuwa na mahusiano mazuri na walipa kodi mbali mbali na kwamba katika Mkoa wa Pwani tunatekeleza kampeni hiyo kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa mahitaji mbali mbali.
Aidha Meneja huyo amebainisha kwamba wanatambua mchango mkubwa ambao unafanya na walipa kodi ambao wameweza kufanya vizuri katika kipindi cha mwaka wa 2023 na mwaka 2024 ikiwa sambamba na kuwashukuru kwa dhati wale walipa kodi wote ambao wamekuwa mstari wa mbele katika suala zima la ulipaji wa kodi.
Pia amesema kwamba katika kampeni hiyo wameweza kutoa msaada wa vitu mbali mbali ikiwemo mifuko ya saruji katika zahanati ya misugusugu kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa wodi ya mama na mtoto, vifaa tiba mbali mbali katika kituo cha afya Mkoani, viti mwendo,taulo za watoto, kitanda katika Hospitali ya Kisarawe sambamba na kusaidia mipira ya kuchezea katika shule msingi Mkoani kitengo cha elimu maalumu.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mkoani Abdulkadir Sultan ameishukuru kwa dhati TRA Mkoa wa Pwani kwa kuweza kutekeleza ahadi yake kwa vitendo ya kutoa misaada na mahitaji mbali mbali ambayo yataweza kuwa ni mkombozi mkubwa katika suala zima la kuwahudumia wagonjwa.
Naye Mganga mfawidhi katika Hospital ya Kisarawe Dkt. Yona Kabata amesema kwamba msaada ambao wamepatiwa na TRA ikiwemo kitanda maalumu kwa ajili ya kujifungulia wakinamama utakuwa ni mkombozi mkubwa kwani hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitanda.
Afisa Elimu kata ya Tumbi Inocensia Mfuru amesema msaada ambao wamepatiwa wa viti maalumu ni moja ya hatua kubwa katika kuwasaidia watoto hao ambao walikuwa wanapata shida katika kutembea hivyo kutaweza kuleta mabadiliko chanya katika kuboresha sekta ya elimu hasa kwa watoto wadogo.
Mamlaka ya mapato (TRA) Mkoa wa Pwani imetekeleza kwa vitendo maelekezo ya serikali ya awamu ya sita na kufanikiwa kutembelea katika Wilaya za Kibaha, Kisarawe, na Wilaya ya Kibiti na kukabidhi misaada mbali mbali ikiwemo, vitanda kwa ajili ya kujifungulia, mifuko ya Saruji,vifaa tiba Vitimwendo , taulo za watoto na mipira ya kuchezea vyote vikiwa na thamani ya kiasi cha shilingi milioni 15.