Maofisa watatu wa polisi wa usalama barabarani jijini Nairobi, Kenya wamekamatwa na kitengo maalum cha kuzuia rushwa wakipokea rushwa kutoka kwa madereva.
Bila kujua kwamba wapo mtegoni katika eneo la mzunguko wa Gloves Cinema, polisi hao walionekana wakisimamisha magari kisha kupewa kitu kidogo na madereva.
Polisi hao walinaswa kwenye purukushani ya ukamataji ambapo kila polisi alikumbana na makachero watatu wa kupambana na ufisadi na wakatiwa mbaroni kisha kupelekwa ofisi ya mkurugenzi wa makosa ya jinai (DCI) ambapo walihojiwa na walipopekuliwa walikutwa na jumla ya shilingi za Kenya shilingi 48,250 ambazo ni sawa na takribani shilingi 976,474 ambazo walizipata kwa kusimamisha magari kwa saa tatu tu walizokaa barabarani hapo.
Tukio kama hilo liliwahi kutokea Tanzania baada ya videoya tukio hilo kusambaa mitandaoni na kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro alilitolea ufafanuzi na kusema wamekamatwa na wangechukuliwa hatua za kipolisi.