Pemba ina mikoa miwili. Mmoja Kusini Pemba, mwingine Kaskazini Pemba. Kusini ndiyo mjini, makao makuu ya Kisiwa cha Pemba. Hata Uwanja wa Ndege wa Pemba, upo Kusini Pemba.
Tuanzie Kaskazini Pemba. Nenda Wilaya ya Wete, tembelea shehia ya Mtambwe Kaskazini. Mtaa wa Mtambwe, kuna msikiti, unaitwa Masjid Ijumaa Nyali. Pembeni ya msikiti huo, ndipo lilipo kaburi la mwanasiasa mwenye historia kubwa Zanzibar na Tanzania yote, Seif Sharif Hamad “Maalim”.
Februari 17, 2025, ilitimia miaka minne tangu Maalim Seif, alipoliendea pumziko la uhai duniani. Kisha akalazwa kaburini kwenye uwanja wa Msikiti wa Ijumaa Nyali. Kaburi limejengwa vizuri, marumaru na changarawe, halafu mageti mawili. Vilevile uzio, upo wa kwanza na wa pili.
Unapokwenda kuzuru kaburi la Maalim Seif, hupati wakati mgumu unapofika Mtambwe. Kila mtu anajua lilipo. Mmoja wa wenyeji akaning’ata sikio kuwa kaburi la Maalim Seif ni maarufu kuliko lingine lolote Mkoa Kaskazini Pemba.
Nipofika kaburini, nilikuta mageti yenye komeo bila kufuli. Nilifungua geti la kwanza, kisha la pili. Nikawa tayari kaburini. Maandishi yaliyosanifiwa kidigitali: “Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad. Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Amezaliwa Oktoba 22, 1943. Amefariki Februari 17, 2021. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, ameen.”
Kaburini, sikukuta mlinzi wala mwangalizi yeyote. Nikauliza kwa wenyeji kama kaburi lina mlinzi, jibu ni hakuna. Msikiti wa Ijumaa Nyali na wakazi jirani, ndiyo hulitazama kaburi hilo. Hujitolea kwa mapenzi mema waliyonayo juu ya Maalim Seif.
Nikakumbuka hekaya kuwa kaburi la Maalim Seif hunukia hasa usiku, watu hutembelea kuchota mchanga, kwa imani kwamba una baraka. Mazingira yalionesha kuwa upo urahisi wa watu kufika kaburini na kuchota mchanga.

Viongozi na wafuasi wa Chadema wakiomba dua mbele ya kaburi la Maalim Seif
Ukirudi Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Chakechake, eneo la Wawi Mavapacha, lipo kaburi lingine la mtu mashuhuri, ni Dk Omar Ali Juma, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 1995 mpaka 2001. Dk Juma pia alipata kuwa Waziri Kiongozi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Ramani ya kaburi la Dk Juma ni sawa kabisa na Maalim Seif. Uzio upo awamu mbili, vivyo hivyo mageti. Hata maandishi kaburini, usanifu wake unafanana. Tofauti ya kwanza ni kuwa sehemu inayozunguka kaburi la Dk Juma ni marumaru tupu, wakati kwa Seif zimemwagwa changarawe.
Kaburi la Dk Juma lina ulinzi. Huingii kaburini mpaka ujieleze, ndipo uruhusiwe na walinzi. Hapo ndipo unaona utofauti.
Kaburi la Maalim Seif lina upweke, hakuna walinzi wala waangalizi. Kaburi la Dk Juma lina ulinzi. Nilipofika kaburini kwa Dk Juma, nilikuta watu wanne wakipata mlo wa mchana, kwenye kibanda cha mlinzi. Ni walinzi na waangalizi wa kaburi.
Inatengeneza maswali, ni kwa nini kaburi la Maalim Seif halina ulinzi, wala kibanda cha mlinzi, wakati la Dk Juma lina vyote? Wote ni viongozi wa Serikali. Kila mmoja kwa wakati wake alikuwa Waziri Kiongozi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Halafu, Dk Juma akawa Makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Maalim Seif Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Ajabu, kaburi la Dk Juma, licha ya kuwa na walinzi, lilikuwa chafu, kuonesha watu hawalifanyii usafi. Nyasi zilikuwa zimeota kwenye kaburi. Kwa Maalim Seif, pamoja na kukosekana walinzi au waangalizi, lakini kaburi lilikuwa nadhifu.
Nilipokuwa Wete, nilipata wasaa wa kuzungumza na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa. Katika mazungumzo yetu, aligusia kuhusu Maalim Seif. Mberwa alisema, wao kama CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, wana kawaida ya kwenda kusoma dua kaburini kwa Maalim Seif kila baada ya miezi sita.
Mberwa alisema pamoja na kusoma dua kila miezi sita, walikuwa na mpango wa kuanzisha tawi la CCM (maskani), mtaa wa Mtambwe, maana ziara zao kwenda kaburini kwa Maalim Seif, zimevutia wananchi wa Mtambwe kuipenda CCM.
“Sisi tunaamini Maalim Seif alikuwa mtu mzuri sana, tatizo lilikuwa watu waliokuwa wamemzunguka. Ndiyo maana tunakwenda kumwombea dua. Wapenzi wengi wa Maalim Seif wameanza kuipenda CCM, baada ya kuona sisi tunakuwa mstari wa mbele kumwombea dua za rehema Maalim Seif kuliko chama chake,” alisema Mberwa.
Maalim Seif ni mmoja wa waasisi wa Chama cha Wananchi (CUF), alishakuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, kisha akawa Katibu Mkuu mpaka alipohamia ACT-Wazalendo mwaka 2019. Akiwa ACT-Wazalendo, Maalim Seif alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
Huu ni mwaka 2025, kwa kalenda ya Tanzania ni mwaka wa uchaguzi. Zanzibar, tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urejeshwe Julai Mosi, 1992, itakuwa mara ya kwanza karatasi ya kupigia kura za urais kumkosa Maalim Seif.
Sura ya Seif ilikuwa moja ya alama za kawaida kwenye karatasi za kupigia kura za urais Zanzibar tangu Uchaguzi Mkuu 1995. Tokea wakati huo, Seif aligombea urais mara sita. Mara tano akiwa na tiketi ya CUF na alipeperusha bendera ya ACT-Wazalendo mara moja.
Pemba, Mtambwe, ndipo Seif alipozaliwa. Kisiwa chote cha Pemba kilibeba nguvu nyingi za kisiasa za Seif. Mara nyingi, aliweza kushinda majimbo yote ya uchaguzi kwenda Bunge la Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Mchuano wa urais Zanzibar, Uchaguzi Mkuu 2025, unatarajiwa kuwa baina ya Rais Hussein Mwinyi dhidi ya Othman Masoud Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. Othman alichukua nafasi baada ya kifo cha Seif.
Nikiwa Pemba, nilisikia mengi jinsi Othman anavyojidhatiti Pemba. Mara kwa mara hufanya ziara mikoa ya Pemba, wilaya hadi wilaya, shehia kwa shehia. Hiyo yote ni kuhakikisha anapita kwenye nyayo za mtangulizi wake, Maalim Seif.
Kipindi Maalim Seif akitiimiza miaka nne tangu alipoipa kisogo dunia, wasiwasi upo chinichini kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, hususan upande wa Zanzibar. Ni Seif aliyewaambia Wazanzibari watulie na warudi nyumbani pale hali ya kisiasa ilipochafuka, na wananchi walimtii.
Je, nani atakuwa Seif, awaambie Wazanzibari waondoke barabarani na warejee nyumbani, kisha wamtii? Nani mwingine asiyependa damu kumwagika, akubali kukosa urais ili amani itawale Zanzibar? Ni miaka minne tangu kifo cha Maalim Seif kitokee, lakini bado inaonekana kuna wasiwasi mkubwa Zanzibar kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.