SIMBA inashuka uwanjani ugenini Jumatano hii dhidi ya Namungo kwenye mchezo mgumu wa Ligi Kuu Bara lakini Kocha wa Wekundu hao, Fadlu Davids kuna ishu kaishitukia kuhusu watani wao wa jadi, Yanga.
Simba ipo nafasi ya pili na pointi 47 ambazo ni tano nyuma ya vinara Yanga ambao wamecheza michezo miwili zaidi, inaingia uwanjani wa Majaliwa Lindi kucheza mchezo wa 19 wa ligi hiyo, ikiwa inatafuta ushindi muhimu ili kuendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania ubingwa huo baada ya kuukosa kwa miaka mitatu mfululuzo.
Hata hivyo, wakati anauendea mchezo huu, Fadlu ambaye amekuwa na mbinu kali kwenye mechi zake amesema ameshtukia jambo kuhusu Yanga na kama hatafanya kazi kubwa basi anaweza akaukosa ubingwa huo msimu huu.
Fadlu amesema kuwa kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi hicho ili kuhakikisha kinafunga mabao mengi kwa kuwa wapinzani wao wameshawaacha nyuma kwa idadi kubwa ya mabao na hilo linaweza kuwanyima ubingwa endapo watalingana pointi mwishoni mwa msimu haswa kutokana na jinsi wanavyobadilishana nafasi mbili za juu kila uchwao. Mabadiliko hayo yanaweza yakaanza kuonekana katika mechi yao dhidi ya Namungo FC ambayo inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo na pointi 21.
“Ili tusikose ubingwa kwa namna yoyote ile, lazima idadi ya mabao iongezeke kwenye mechi zetu, katika msimamo wa Ligi Kuu hasa nafasi ya kwanza ambayo wapo wapinzani wetu ( Yanga), kumekuwa na mabadiliko makubwa kwao, kila mechi zikichezwa.
“Kuna mabadiliko ninayoyafanyia kazi haraka sana baada ya kuona wapinzani wetu, mechi zinazokuja ikiwemo hii dhidi ya Namungo naamini zitakuwa na matunda, tunakwenda mwisho wa msimu kila timu inapambania malengo yake nasi lazima tuhakikishe tunabadilisha baadhi ya vitu,” alisema Fadlu ambaye ni raia wa Afrika Kusini.
“Ukiona mbio za ubingwa bado zipo wazi sana, lolote linaweza kutokea, tunaendelea kushinda mechi zetu hatutaki kurudia makosa ya kuangusha pointi kirahisi, lakini lazima tufunge mabao ya kutosha kwa kuwa huko mbele yanaweza kuwa sehemu ya timu kutwaa ubingwa msimu huu,” alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
Hadi sasa ikiwa imecheza michezo 20, Yanga ndio kinara wa kufunga mabao ikiwa nayo 50 na kuruhusu tisa, huku Simba ikiwa nafasi ya pili baada ya kufunga mabao 38 na kuruhusu sita, hivyo Simba inatakiwa kufunga mabao tisa bila kuruhusu bao ili kuifikia idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa ya Yanga. Kwa michezo ya hivi karibuni, Yanga imefunga mabao 12 kwenye michezo miwili, ikiichapa Ken Gold 6-1 sawa na KMC ikiweka rekodi ya timu iliyoifunga mabao mengi kwenye mchezo mmoja wa ligi hadi sasa.
Idadi hiyo ya mabao kwenye michezo miwili ni zaidi ya mabao yote yaliyofungwa na Pamba (11), JKT Tanzania (11) pamoja na Prisons (9), kwenye michezo yote 20 ya ligi msimu huu hadi sasa.
Hata hivyo, Fadlu ambaye kama akitwaa ubingwa huu utakuwa wa kwanza kwake akiwa kocha mkuu kuanzia ameanza kufundisha soka, anataka kuepuka Simba kukosa ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kama ilivyotokea msimu wa 2016/2017, ambapo Yanga iliiubeba baada ya timu zote mbili kukusanya pointi 68, lakini Yanga ilichukua ubingwa huo baada ya kufunga mabao 57 na kuruhusu 14, huku Simba ikifunga 50 na kuruhusu 17 tu.