WANANCHI WA KIJIJI CHA MTYANGIMBOLE WASHUKURU SERIKALI KWA KUJENGA SHULE YA SEKONDARI

 NA BELINDA JOSEPH, RUVUMA.

Wananchi wa Kijiji cha Mtyangimbole kata ya Mtyangimbole Halmashauri ya Madaba, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Mbunge wa Jimbo la Madaba Mhe Joseph Kizito Mhagama,  kwa kujenga shule ya sekondari katika eneo hilo ambayo imeondoa adha kubwa iliyokuwa ikiwakumba wanafunzi kulazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita nne kufuata elimu, na hivyo kuongeza muda wa kupumzika na kujisomea kwa wanafunzi.

Kwa mujibu wa Jackson Lomanus Luambano Mkazi wa Kijiji cha Mtyangimbole, ujenzi wa shule ya sekondari umeleta faraja kubwa kwa jamii kwani wanafunzi sasa wataweza kupata elimu bora katika mazingira bora, huku wananchi wakitoa pongezi kwa Rais Samia  kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu ambayo imekuwa chachu ya maendeleo katika jimbo hilo.

Yolanda Ngonyani , amesema kuwa watoto wao walikuwa wanapata shida kubwa kwenda shuleni Nguruma, ambapo walilazimika kubeba mabegi mazito na kutembea umbali mrefu Hali hiyo ilikuwa ikiwachosha na mara nyingi walikuwa wakishindwa kushiriki kazi za nyumbani kutokana na uchovu wa kutembea umbali mrefu.

Akizungumza Mbunge wa Jimbo la Madaba Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama akiwa katika ziara yake ya kikazi, amewahimiza wananchi kutokubali kulaghaiwa na watu wanaoshutumu juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu, akiyataja mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ujenzi wa shule za msingi na sekondari huku akisisitiza kwamba mabadiliko hayo ni matokeo ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake.

Amesema Halmashauri ya Madaba inajivunia kuwa kinara kitaaluma katika Mkoa wa Ruvuma, kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, Hii imewezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri na matokeo bora kitaaluma.

Naye, Mkazi wa Kijiji cha Mtyangimbole, Ndg. Side Nyoni, alitoa shukrani za dhati kwa Mbunge Mhagama kwa kuendelea kusikiliza changamoto za wananchi na kutoa taarifa ya maendeleo ya jimbo. Aliahidi kumuunga mkono Mbunge huyo na kumueleza mahitaji ya maendeleo katika kijiji chao.

Ziara ya Mhagama bado inaendelea katika vijiji mbalimbali vya Jimbo la Madaba, huku akipokea changamoto za wananchi na kuhakikisha utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi unaendelea kwa manufaa ya wananchi wote.

Related Posts