JANUARI mwaka jana, Kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche ambaye ni raia wa Algeria alipigwa rungu la kufungiwa kujihusisha na usimamizi wa benchi la ufundi kwa mechi nane, adhabu ambayo ilitolewa na Shirikisho la Soka Afrika(Caf).
Amrouche alipewa adhabu hiyo baada ya kutoa kauli ambayo ilionekana kulitia doa shirikisho hilo akidai linaipendelea Morocco kwa kuipa nguvu ya kufanya maamuzi mengi yanayohusu soka la Afrika ikiwemo kujichagulia marefa.
Adhabu ile ilituchanganya sana hapa kijiweni maana ilitolewa wakati Taifa Stars inashiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) na yule ndiye alikuwa kiongozi wetu wa benchi la ufundi tukawa tunajifikiria mambo yatakavyoenda baada ya hapo.
Hata hivyo, ilikuwa ni kama bahati kwa kocha msaidizi, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye alikaimu nafasi hiyo na timu haikupoteza mechi zake mbili za mwisho na hata baada ya hapo, Taifa Stars ikafanya vizuri katika mechi zilizofuata.
Ikafuzu Afcon 2025 ikiwa chini ya Morocco na katika kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 ipo katika nafasi ya tatu kwenye kundi lake na inaonyesha matumaini lolote linaweza kutokea.
Hii imesababisha Watanzania wengi kutamani Morocco aendelee kubakia katika nafasi ya ukocha mkuu wa Taifa Stars kwa ajira ya kudumu yeye na wazawa wenzake kwa vile timu imeonekana kucheza vizuri na kupata matokeo mazuri chini yao.
Hata hivyo, Amrouche amepindua meza na hivi karibuni adhabu yake imetenguliwa hivyo kwa vile bado ana mkataba unaoisha mwakani na Taifa Stars, nafasi yake kama kocha mkuu bado inatambulika na ana haki ya kurudi katika kitu chake.
Tukiamua kubaki na Morocco, maana yake tutalazimika kulipa kiasi kikubwa cha fedha ili kuvunja mkataba wa Amrouche ambaye amebakisha karibia mwaka na nusu katika mkataba wake.
Tukisema tusipoteze hizo hela, maana yake tunairudisha timu kwenye kuanza upya na kile ambacho Morocco alikuwa ameshakianza tutakivuruga.