Bosi Jatu ahoji upelelezi kutokukamilika miaka mitatu

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, imeitaka Serikali tarehe ijayo, itoe majibu sababu gani inayosababisha upelelezi wa kesi ya iwasilishe majibu kuhusiana mshtakiwa, Peter Gasaya (33) ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya JATU PLC, kutokukamilika mpaka sasa.

Gasaya anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Februari 20, 2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mhina amefikia uamuzi huo, baada ya mshtakiwa kudai mahakamani hapo kuwa kesi yake imefikisha miaka mitatu bila upelelezi kukamilika.

Awali, kabla ya kutoa uamuzi huo, Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele amedai kesi hivyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mwakamele baada ya kueleza hayo, mshtakiwa alinyoosha mkono juu aliashiria kuwa anaomba kupewa nafasi ya kuongea.

Mahakama ilivyompatia nafasi ya kuongea amedai kesi yake imefikisha miaka mitatu bila upelelezi kukamilika, hivyo amehoji ni upelelezi wa aina gani ambao unachukua muda mrefu kukamilika.

“Kesi hii ni ya muda mrefu, imeshafikisha miaka mitatu na upelelezi wake bado haujakamilika na mahakama haisemi chochote,” amedai Gasaya.

“Huko nyuma upande wa mashtaka walisema upelelezi umekamilika na wakapangiwa tarehe kwa ajili ya kunisomea hoja za awali (PH), lakini siku hiyo ilipofika ya kunisomea PH, upande wa mashtaka waliifuta kesi hiyo na kunifungulia nyingine ambayo hadi leo upelelezi wake haujakamilika,” amedai.

Pia, mshtakiwa huyo amedai alishawahi kuingia katika makubaliano ya kukiri mashtaka kwa kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), lakini hajui ni kwanini upelelezi wa kesi hiyo haukamili.

“Mheshimiwa hakimu, pia hivi karibuni nilihojiwa na Takukuru na kuelezwa kuwa upelelezi utakamilika haraka, lakini mpaka sasa upelelezi haujakamilika, ni upelelezi gani huo ambao haujakamilika kwa miaka mitatu,” amehoji mshtakiwa.

Baada ya kusikiliza hoja ya mshtakiwa, hakimu Mhini ameelekeza upande wa mashtaka ufuatilie na tarehe ijayo waje na majibu, upelelezi wa kesi hiyo umefikia hatua gani.

“Upande wa mashtaka mfuatilie na tarehe ijayo mje na majibu, upelelezi umefikia hatua gani na kama mliingia majadiliano na DPP, sasa kitu gani kinachokwamisha upelelezi wa kesi hiyo usikamilike,” amehoji Hakimu Mhini.

Baada ya kutoa maelekezo hayo, aliahirisha kesi hiyi hadi Machi 6, 2025 kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana.

Kwa mara ya kwanza Gasaya alifikishwa katika Mahakamani hapo, Desemba 29, 2022 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili ambayo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5.13 bilioni kutoka Saccos ya Jatu.

Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa siyo kweli.

Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.

Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh5.13 bilioni kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo Benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC liyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Related Posts