Dar es Salaam. Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umesema barua ya malalamiko kuhusu uteuzi wa viongozi watendaji wa juu na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, iliyowasilishwa na kada wa chama hicho, ‘haina mambo magumu’ ya kukisumbua.
Hata hivyo, wakati Chadema kikieleza hayo, kada huyo, Lembrus Mchome, amesema hatakubali kupokea majibu mepesi wakati hoja zake mbili za akidi na wajumbe wasiohusika kupiga kura kwenye baraza kuu ni nzito.
“Hata kama barua yangu haina mambo magumu ya kunijibu, ninachohitaji kujibiwa ni barua yangu ambayo nimeonyesha ina mambo makuu mawili; la akidi kutotimia kwenye kikao cha baraza kuu na uwepo wa wanachama wasio wajumbe wa baraza kuu, lakini walipiga kura za kuwaidhinisha viongozi,” amesema Mchome.
Hata hivyo, amesema itategemea kama ataridhika na majibu yao, na kama hataridhika ataona nini cha kufanya kwa lengo la kuilinda Katiba ya Chadema.
Katika barua hiyo, Mchome, ambaye awali alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) mkoani Kilimanjaro, anapinga uteuzi wa viongozi hao uliofanywa na Mwenyekiti, Tundu Lissu, Januari 22, 2025, akidai umekiuka katiba ya chama hicho.
Mchome, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, amesema uteuzi wa vigogo hao uliidhinishwa bila akidi ya kikao cha baraza kuu kutimia.
Kwa mujibu wa Mchome, viongozi waliopatikana katika utaratibu huo ni pamoja na Katibu Mkuu, John Mnyika, Aman Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).
Katika barua hiyo, Mchome amesema wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na kikao hicho kuwa ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk. Rugemeleza Nshala, akidai uteuzi wao ni batili.
Akizungumza na Mwananchi leo, Alhamisi, Februari 20, 2025, Golugwa amesema: “Ni barua ambayo haina mambo magumu. Ni barua itakayojibiwa kwa page (kurasa) moja tu, itakuwa imejitosheleza. Itakavyofanyiwa kazi, atajibiwa mhusika aliyeandika. Utaratibu wa kiutawala, barua itakwenda kwa mhusika.
“Itakavyojibiwa, atapewa mhusika. Tayari imepokelewa, ipo kwa makarani wa chama ambao tutawapa maelekezo waindike ili mhusika apewe,” amesema Golugwa, bila kueleza siku watakayompatia majibu Mchome.
Kwenye barua hiyo, Mchome, ambaye pia ni mjumbe wa Mkutano Mkuu na Baraza Kuu la Chadema, alipeleka nakala Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Jana, Jumatano, Februari 19, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alikiri kuipokea na kusema kilichoandikwa kina mantiki.
“Kwa sababu barua imeandikwa kwa Katibu Mkuu, tunasubiri ifanyiwe kazi kwanza ndani ya chama, lakini tumeiona ina malalamiko ya msingi sana. Kwa utaratibu uliopo, wasiporidhika, anakuja kwetu ambao tunasimamia Katiba na sheria za vyama,” amesema Nyahoza.
Amesema kwa sasa nao pia wanasubiri majibu kutoka Chadema ili waone suala hilo limekaaje.
“Kwa sababu huwezi kujua ukweli wa jambo hadi usikilize pande zote mbili. Tunasubiri, lakini ukiyasoma unaona mantiki yake, ila huo ni upande mmoja. Lazima tusikilize na upande wa pili,” amesema Naibu Msajili huyo.
Kwa mujibu wa Nyahoza, kama mlalamikaji (Mchome) hataridhika na majibu atakayopewa, atawasilisha katika ofisi ya msajili kwa sababu mambo ya katiba hayaishii ndani ya chama.
Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na sakata hilo, mchambuzi wa siasa, Ramadhani Manyeko, amesema kinachotakiwa ni uongozi wa Chadema kuweka ushahidi wa muhtasari wa kikao cha Baraza Kuu utakaoeleza wajumbe waliohudhuria, saini zao, ajenda zilizojadiliwa, na akidi itaonekana.
“Maana nimeona wengine wanahoji uteuzi wa Katibu Mkuu. Hili nalo litaelezwa hapo. Cha msingi ni Chadema kupeleka ushahidi wa muhtasari wa kikao. Hili ndilo litakalokuwa suluhisho,” amesema.
“Vinginevyo, kama hakutakuwa na muhtasari, basi kutakuwa na ubatili wa wajumbe na Kamati Kuu. Kwa kipindi hiki cha uchaguzi, ni hatari sana chama kuwa na mvutano. Muda si rafiki kuingia kwenye mgogoro, chama kinatakiwa kiwe na umoja,” amesema.
Manyeko alikitolea mfano Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimeamua kumaliza mapema suala la mgombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.
“Licha ya jambo hilo kuwa na manung’uniko, ikiwemo wanachama kusema taratibu zilikiukwa na wengine wamefukuzwa uanachama, lakini CCM ni tofauti na vyama vingine ambavyo, kukiwa na mgogoro, vinashindwa kuuhimili,” amesema Manyeko.
Katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika jijini Dodoma, Januari 19, 2025, chama hicho kiliwapitisha kwa kauli moja Samia Suluhu Hassan kuwania urais wa Tanzania, Dk Hussein Ali Mwinyi kugombea urais wa Zanzibar, na Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa Samia.