WAKATI wowote Coastal Union inaweza kuishtua Simba ikipanga kuhamisha mchezo huo wa Ligi Kuu utakaopigwa Machi Mosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Tangu msimu uanze Coastal imetumia viwanja vitatu tofauti vya nyumbani ikianza na KMC Complex, kisha Azam Complex na sasa Sheikh Amri Abeid uliopo Arusha kutoka na Mkwakwani kufungiwa ili kupisha mboresho.
Wagosi hao wanaoshika nafasi ya saba katika ligi, huenda wakarejea katika uwanja wake wa nyumbani na kukutana na Simba hapo kutokana na maboresho hayo kukamilika kwa asilimia kubwa.
Meneja wa Uwanja huo, Nassoro Makau alisema bado kuna asilimia chache zimesalia kukamilika kwa marekebisho yaliyokusudiwa, huku akikiri wakati wowote kuanzia Machi unaweza kurudi kwenye matumizi.
“Uwanja upo kwenye hatua za mwisho kukamilika naweza kusema kama asilimia 85-90 hivi, kuna mambo machache sana yamesalia yakikamilika tutawajulisha kwa taarifa rasmi, hii nakujibu kwa kuwa mmepiga simu kuuliza.
“Kuhusu Coastal kama wanapanga kuutumia kwenye mechi zijazo, hili ni suala la muda kwanza likiwa kwenye nafasi ya sisi kulizungumza tutatoa taarifa.”
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almasi Kasongo alisema, bado hawajapata taarifa kamili, ila kikanuni Na hata muda bado upo kuweza kufanya maamuzi hayo hivyo Kama utatumika watatoa taarifa.
“Kikanuni baada ya siku saba kabla ya mchezo ndio ratiba hujulikana kama watabaki Arusha au watarejea nyumbani.
“Tusubiri siku mbili hizi huenda mambo yakabadilika kwa sababu upo kwenye maboresho basi lolote linaweza kutokea.”
Katika misimu miwili iliyopita Coastal haijawahi kuifunga Simba Mkwakwani na msimu huu katika mechi ya awali zilitoka sare 2-2 Simba ikiwa wenyeji.