Dawasa yapewa masharti kutoa maji saa 24, fedha za usumbufu kila mwezi

Dar es Salaam. Wenyeviti 142 wa Serikali ya mitaa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam wameingia makubaliano na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) ikiwamo sharti uhakika wa maji kwa saa 24 na fedha za mawasiliano kila mwezi.

Makubaliano hayo yaliingiwa leo, Alhamisi Februari 20, 2025 kwenye semina iliyoandaliwa na Dawasa ya kutoa elimu na kutengeneza daraja la mawasiliano ya utoaji huduma ya maji kwa wananchi.

Semina hiyo iliyofanyika Manispaa ya Temeke, Dawasa iliwasilisha taarifa yake na kutoa fursa kwa wenyeviti hao 142 kuuliza maswali ya kero zinazowasumbua na kupatiwa majibu.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni namna wenyeviti wa mitaa wanaweza kusaidia kuwabaini wadaiwa sugu wa maji, wezi wa maji, waharibifu wa miundombinu ya maji na ukusanyaji wa madeni wanaokwepa kulipa kwenye mitaa yao.

Hoja hizo ziliwafikisha Dawasa na viongozi hao wa mitaa kuingia makubaliano yatakayorahisisha utendaji wao wa kazi.

Miongoni mwa makubaliano hayo ni Dawasa kuwapa wenyeviti hao Sh20,000 kila mwezi kuanzi mwezi ujao kwa ajili ya kuwawezesha kufanya mawasiliano na uhakika wa huduma ya maji kwa saa 24.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo Sh20,000 kila mwezi zinatakiwa kuanza kutolewa mwezi ujao, fedha ambazo ni gharama ya kushughulikia kero zinazohusu huduma hiyo na kuwasilisha kwa Dawasa.

Pia, wamekubaliana madeni yanayokusanywa kwenye mitaa yao, ya wateja wasiolipa bili na  wanaohujumu miundombinu wakifanikiwa kukusanya baada ya viongozi hao kutoa taarifa asilimia 30 ya fedha itakayopatika iachwe mtaa husika.

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Temeke, Sharif Jumbe amesema maazimio waliyokubaliana  baada ya kuwasilisha kero zao yasije yakavunjwa na mtu mwingine kwani wananchi wao wanachohitaji ni huduma.

Hata hivyo, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire amewaangukia viongozi hao wasamehewe kwa mapungufu yaliyojitokeza na kuahidi kwenda kuyafanyika kazi ili wajenge mahusiano endelevu.

“Tulichokifanya hapa huu ni mwanzo na baada ya kupata uelewa huu wa pamoja, tunachohitaji ni uwajibikaji kwa watendaji wetu kwakuwa tunafanya kazi kwa ngazi,” amesema Bwire.

Bwire amesema ili waweze kufanya kazi kwa ushirikiano na kusogeza huduma na uwajibikaji wanatarajia kuanza kuwapa vocha kila mwezi ya Sh20,000.

“Vocha hizi zitatolewa kuanzia Machi mwaka huu, lakini tunataka mtusaidie kubaini wanaohujumu miundombinu ya maji na tukifanikiwa wote watakaopigwa faini asilimia 30 ya fedha watakuwa wanagawana  itakuwa inarudi katika mtaa husika,” amesema.

Ilivyokuwa katika mkutano huo

Wenyeviti hao wamedai wao ni wanasiasa na bado wanahitaji madaraka, lakini kero ya kukosekana kwa huduma hiyo muda mwingi na Dawasa wako kimya inawatesa kiasi cha kushindwa kufurahia kukalia nafasi hizo.

Wamesema wanachojua wanawadharau kwa kudhani wao ni darasa la saba hawajui kitu  kwani, kuna wakati hata wakiwapigia simu watendaji wa mamlaka hiyo kutaka kuwaeleza malalamiko ya wananchi wao, lakini hawapewi ushirikiano.

“Mtaani kwangu kila siku kuna watu wanakuja kuniletea kero ya maji, miundombinu kila kitu kipo lakini maji hakuna namaliza wiki, na hivi wengi wana matumaini kutokana na ahadi tulizowaahidi tunakosa majibu,” amesema Alhaji Abdul, Mwenyekiti wa Mtaa Kimbangulile.

“Ili ndoa yetu idumu nilazima tuliyokubaliana yaanze kutekelezwa,” amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Jangwela, Mussa Bakari kutoka Chama cha   ACT -Wazalendo, amesema eneo lake maji yanamwagika ovyo kila wakitoa taarifa, lakini hawaendi kutengeneza.

“Mbali na changamoto hiyo wananchi wangu wanalalamika wanatumia maji ya chumvi tunahitaji majisafi na salama wananchi kila siku wanakuja kunilalamikia,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda alianza kwa kusema maji ni miongoni mwa kero zinazowasumbua wananchi wake, zingine ni umeme na barabara huku akizitaka taasisi hizo kuiga mfumo waliokuja nao Dawasa.

“Huduma ya maji inatugusa kwa asilimia 150, na maji inaonekana huduma ya maana pale inapoonekana haipo, umeme asilimia 150, barabara 150, afya asilimia 150 lakini haya yote niliyoyasema yanasimamiwa na taasisi zake zilizopo kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Amesema wenyeviti wapo tayari kufanya kazi lakini wanakosa watu wa kufanya nao kazi, ingawa Dawasa walivunja daraja la mahusiano wenyewe na sasa wameamua kurudisha.

“Dawasa tambueni wenyeviti wa mitaa wana watu, mkitengeneza mahusiano mazuri hakuna litakaloshindikana kama kuna sehemu inavujisha maji mtapata taarifa mapema. Tukimaliza hili nitazifuata taasisi zingine zinazotoa huduma kwa umma kufanya hivi,” amesema.

Mkurugenzi wa miundombinu kutoka Dawasa, Ramadhani Mtindasi amesema mamlaka hiyo inahudumia wateja milioni 6.8 katika majimbo 18 ya uchaguzi.

“Wilaya ya Temeke pekee tunahudumia huduma ya majisafi kwa asilimia 83.9, changamoto haipati maji masaa 24, na hiyo inatokana na iko mwishoni, ingawa bado tunaendelea kuboresha huduma hadi kufikia mwaka 2030 tuhudumie kwa asilimia 100,” amesema.

Amesema matarajio yao baada ya kukamilika mradi wa Bangulo unaojengwa Wilaya ya Ilala utakuwa mkombozi katika eneo la Temeke na mengine kwa kuwasogezea huduma ya maji.

Related Posts