DC Msando atangaza msako wanafunzi 356 wasioripoti shuleni

Handeni. Mkuu wa Wilaya ya Handeni (DC) mkoani Tanga, Albert Msando ameliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na watendaji wa kata kuwatafuta wanafunzi 356 wa kidato cha kwanza wa shule za sekondari ambao hawakuripoti shule mpaka msasa.

Msando amesema ameshamuagiza kamanda wa polisi Wilaya ya Handeni akiwa na polisi kata, kuwatafuta wanafunzi hao kwa kuwa, Serikali haina taarifa walipo na wanatakiwa kuripoti shuleni kuendelea na masomo yao ya sekondari.

Akizungumza kwenye kikao cha kawaida cha madiwani wa Halmashauri ya Mji ya Handeni leo Alhamisi, Februari 20, 2025, mkuu huyo wa wilaya ameagiza polisi kata wakishirikiana watendaji, kutafuta sehemu walipo wanafunzi hao na kuwapeleka shuleni kuungana na wenzao.

Amesema wazazi wa watoto hao pia wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria na kueleza sababu za kushindwa kusimamia wanafunzi kuhudhuria masomo wakati Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kugharamia masomo yao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni, Mussa Mkombati akizungumza kwenye baraza hilo amesema wanazo taarifa baadhi ya wanafunzi wameolewa, kupelekwa kufanyakazi za ndani, kwenda kwenye migodi na shughuli nyingine kinyume cha utaratibu.

Amesema baraza la madiwani lipo tayari kutoa ushirikiano kwenye vyombo vya kamati ya ulinzi na usalama ili kufanikisha kupatikana kwa wanafunzi na mwisho wa kuripoti kwao ilikuwa Februari 15, kwa hiyo waliopuuza wanatakiwa kuchukuliwa hatua.

Mkombati amesema pia wapo wanafunzi wa kidato cha pili ambao matokeo yao yamekuwa sio ya kuridhisha na wao warudi shule haraka  kuwa wanatakiwa kuendelea na masomo kama wengine licha ufaulu wao kutokuwa wa kuridhisha.

Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji Handeni, Mtendeji Kingimali amesema jumla ya wanafunzi wote ambao wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza ni 2,048 kati yao tayari 1,600 wamesharipoti na bado wengine 356 hawajaripoti.

Amesema ofisi ya mkurugenzi kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama, madiwani na viongozi wengine tayari wameshaanza msako wa kutafuta wanafunzi hao.

Aidha amesema athari ya kuchelewa kuripoti kwa wanafunzi hao ni kukosa masomo ya awali hasa Kiingereza ambacho hufundishwa kwa hatua za awali ili kuweza kudumu masomo yao mengine.

Related Posts