Simanjiro. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi ametoa onyo kali kwa viongozi wa serikali za vijiji wanaotokana na chama hicho akiwataka kuacha tabia ya kujiona miungu watu kwa kuwaonea wananchi na kupora mali zao.
Mbali na hilo, Hapi amewahakikishia wananchi, hususan jamii ya wafugaji na wakulima wa Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara kuwa CCM itaendelea kuisimamia Serikali ili kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinafanyiwa kazi kwa haraka na kwa ufanisi.
Hapi amesema hayo leo Alhamisi, Februari 20, 2025 katika ziara aliyoianza mkoani Manyara. Akiwa wilayani Simanjiro kijiji cha Narakawo, Kata ya Loiborsireti, Hapi amesema chama hicho hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wanaokwenda kinyume na misingi ya uadilifu na haki katika utumishi wao.

Wakazi wa Kata ya Loiborsiret wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Taifa Ally Hapi alipoanza ziara yake. Picha na Joseph Lyimo
“Viongozi wa vijiji wanapaswa kuwa mfano wa haki na uwajibikaji, kama kuna yeyote anayenyanyasa wananchi au kupora mali zao, basi CCM haitamfumbia macho,” ameisisitiza.
Pia, Hapi amewataka viongozi wa chama na serikali kujikita zaidi katika kutatua kero za wananchi ili kuhakikisha CCM inaendelea kupata ushindi wa kishindo katika chaguzi zijazo.
Amesema mafanikio ya chama yanategemea utendaji wa viongozi wake katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi kwa uwazi na uwajibikaji.
“Wananchi wanahitaji viongozi waadilifu, wanaowatumikia kwa dhati, CCM itaendelea kuwa chama imara endapo viongozi wake watazingatia majukumu yao kwa haki na uaminifu,” amesema Hapi.
Kauli hiyo imekuja wakati serikali ikiendelea na juhudi za kuboresha huduma kwa wananchi, huku ikisisitiza uwajibikaji kwa viongozi wa ngazi zote za uongozi nchini.
Mwenyekiti wa wazazi wilaya ya Simanjiro, Haiyo Mamasita amesema wamefanikiwa kuanza ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa jumuiya hiyo.
Mamasita amesema kutokana na kasi ya ujenzi wa nyumba hiyo ya mtumishi wa jumuiya ya wazazi, wanatarajia itakamilika hivi karibuni ili aweze kuhamia.
Hapi amesema CCM imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, hasa katika kulinda masilahi ya wakulima na wafugaji.
“CCM ipo bega kwa bega na serikali kuhakikisha kuwa wakulima na wafugaji wanafanya shughuli zao kwa amani na usalama, tunatambua changamoto zilizopo na tutaendelea kuisimamia serikali ili kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” amesema Hapi.
Amesisitiza pia umuhimu wa amani na usalama kwa maendeleo ya taifa, akieleza kuwa bila amani hakuna jambo lolote linaloweza kufanikiwa.
“Amani ni tunu kubwa kwa taifa letu, bila amani, hakuna kilimo, hakuna ufugaji, hakuna biashara na hakuna maendeleo, hivyo ni jukumu letu sote kulinda amani kwa kila hali,” amesema Hapi.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka amesema namna serikali ya awamu ya sita inavyoshughulikia changamoto za wananchi kwa vitendo.
Ole Sendeka amesema moja ya hatua kubwa zilizochukuliwa ni ujenzi wa bwawa maalumu kwa ajili ya mifugo, linalofadhiliwa na serikali, ili kusaidia upatikanaji wa maji kwa wafugaji.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inatekeleza ahadi zake kwa vitendo, hili bwawa kwa ajili ya mifugo ni moja ya miradi muhimu iliyofanikishwa kwa fedha za serikali ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji kwa wafugaji wetu,” amesema Ole Sendeka.

Mbunge wa Viti Maalumu, Asia Halamga amesema namna Serikali inavyofanya kazi kwa bidii kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ya kweli.
“Tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, tumeona mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali. Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ajili ya wananchi na sisi kama viongozi tunaendelea kuhakikisha kuwa jamii wananufaika na miradi hiyo,” amesema.
Mwenyekiti wa wazazi Mkoa wa Manyara, Janes Darabe amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia imewajali watu wote hususani wafugaji na wakulima.
Diwani wa Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Mardadi) amesema jamii imeoma namna mipango ya serikali inavyowanufaisha kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi walioshiriki mkutano huo akiwemo Lowasa Sindilopa na Daniel Pakasi wameeleza kwamba licha ya kuwa na imani na serikali, bado wanahitaji hatua zaidi za kutatua changamoto zao, hususani zinazohusiana na upatikanaji wa marishsho ya mifugo na huduma bora za kijamii na miundombinu.
“Tuna imani na serikali, lakini bado tunahitaji msaada zaidi katika kutatua changamoto zetu, suala la maji, barabara na huduma za afya linapaswa kupewa kipaumbele zaidi,” amesema Pakasi.