Dar es Salaam. Utafiti mpya uliofanywa na Taasisi ya Economic and Social Research Foundation (ESRF) umebaini wagonjwa wa saratani hufika hospitali ugonjwa ukiwa hatua za awali, lakini wataalamu ndio hushindwa kutambua tatizo hilo mapema.
Utafiti huo umebani, wagonjwa wengi, hususani wenye saratani ya mlango wa kizazi, ini pamoja na titi, huambiwa wanasumbuliwa na maradhi mengine kama maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), tumbo pamoja na homa.
Takwimu za Wizara ya Afya kupitia Mfumo wa Taarifa za Utoaji wa Huduma za Afya (Mtuha), zinaonyesha idadi ya wagonjwa wapya wa saratani, inaongezeka kila mwaka, ikiwa imetoka wagonjwa 33,484 mwaka 2019 mpaka 49,215 mwaka 2023.
“Wagonjwa wapya wa saratani takribani 44,931 wanagundulika katika maeneo mbalimbali ya nchi na vifo 29,743 vinaripotiwa kila mwaka,” inaeleza taarifa ya Mtuha.
Utafiti wa sasa wa ESRF unaibua hayo wakati wataalamu wa afya katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), wanaeleza wagonjwa wa saratani wanaofikishwa kupatiwa matibabu ndani ya taasisi hiyo hufika ugonjwa ukiwa hatua ya mwisho ambayo haitibiki.
Yaliyomo ndani ya utafiti huo yamebainishwa leo Alhamisi, Februari 20, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF-Tanzania, Profesa Fortunata Makene katika wasilisho la kitabu, Cancer Care in Pandemic Times, chenye matokeo ya utafiti huo uliofanyika tangu mwaka 2018.
Utafiti uliofanyika kwa ushirikiano baina ya Tanzania, Kenya, Uingereza na India, uliangalia ‘ubunifu wa namna gani unahitajika kutatua tatizo la saratani na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa matibabu ya ugonjwa huo.
“Kwa ugonjwa wa saratani tuliwauliza wagonjwa walianza kujisikia kutokuwa sawa lini na walichukua hatua gani, kilichotushtua wagonjwa wanafika hospitali tatizo likiwa hatua za mwanzo, anapimwa anaambiwa una maambukizi ya njia ya mkojo, tatizo la tumbo, sasa hadi apewe rufaa tatizo likatambulike hospitali za rufaa za mikoa tayari anakuwa amezungushwa sana,” amesema.
Profesa Fortunata amesema kutokana na mzunguko huo na mgonjwa kukosa fedha, anapofika hospitali, tayari tatizo limeenea mwilini na halitibiki tena, hivyo si kweli kwamba wagonjwa wa saratani wanachelewa kufika hospitali.
Pia, amesema hali hiyo imechangiwa na kukosa wataalamu wa kutosha katika hospitali zilizopo nchini, wenye uwezo wa kugundua saratani mapema.
Amesema wapo wanazunguka vijijini kwa zaidi ya miaka minne kuhangaikia vipimo vya kubaini aina ya maradhi yanayowasumbua.
Suluhisho la tatizo hilo ni kuwajengea uwezo wataalamu wa afya na kuwezesha kufanyika kwa utafiti wa tatizo la saratani nchini, pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa upatikanaji wa takwimu za tatizo hilo.
Mtaalamu wa uchumi sekta ya afya wa Chuo Kikuu Huria nchini Uingereza, Maureen Mackintosh amesema kitabu kilichozinduliwa kinaelezea uzoefu wa wagonjwa na watoa huduma na watu waliopona ugonjwa wa saratani.
Dk Mercy Njeru wa Taasisi ya Utafiti wa magonjwa Kenya (KEMRI), amesema ili kutatua tatizo la saratani, ni lazima Wizara ya Afya ijenge ushirikiano na wizara zingine kushughulikia tatizo hilo.
“Tunahitaji kushirikiana na sekta zetu, tunajaribu kuunganisha afya na sekta ya viwanda katika kutafuta suluhu kwa watu wetu,” ameeleza.
Vikwazo utafiti wa saratani
Kupitia mdahalo wa wanazuoni wa masuala ya afya uliohusu kufanyika tafiti za saratani nchini, gharama kubwa ya kufanya utafiti zilielezwa kuwa mwiba kwa utafiti wa ugonjwa huo.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Afya Sayansi Shirikishi (Muhas), Elia Mbaga amesema utafiti wa ugonjwa wa saratani huhitaji rasilimali nyingi kwenye hatua ya uchunguzi na vipimo.
“Tunahitaji kuwa na uwezo wa kufuatilia matukio ya saratani nchini na kuainisha vifaa muhimu vinavyohitajika katika maeneo mbalimbali pamoja na kuwa na uwezo wa kufanya makadirio ya ukubwa wa tatizo la saratani mbalimbali zilizopo.
Hii itatusaidia kuhakikisha rasilimali tulizonazo zinatumiwa vizuri na kwa usahihi, na pia kuimarisha utambuzi na matibabu ya saratani katika nchi yetu,” amesema.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Crisprin Kahesa, amesema ili kuwa na utafiti wa aina mbalimbali wa saratani ni muhimu kuweka kipaumbele katika ugawaji wa rasilimali watu, fedha na muda kwa watafiti.
Takwimu za Mtuha zinaonyesha kuwa saratani tano zinazoongoza nchini ni pamoja na saratani ya mlango wa kizazi asilimia 24.1 ikifuatiwa na tezi dume (asilimia 10), saratani ya matiti (asilimia 9.1), ya koo (asilimia 7.9) na saratani ya utumbo mpana ( asilimia 4.9).