Hizi ndizo changamoto zinazom­kandamiza mtoto wa kike, kungwi watajwa

Dar es Salaam. Wakati mapambano ya usawa wa kijinsia yakiendelea si Tanzania pekee bali duniani, wadau eneo hilo wamekuja na mradi wa jinsia wenye lengo la kuipa jamii elimu pamoja na kutokomeza ukandamizwaji wa mtoto wa kike.

Katika mradi huo ulioanza mwaka 2022 ambao unatarajiwa kukamilika mwaka huu 2025 ulioandaliwa na Taasisi ya Aga Khan (AKF), unaangazia changamoto zinazoikabili jamii katika suala zima la usawa ikiwemo ukeketaji, unyanyasaji wa kijinsia.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Februari 20, 2025 kwenye warsha iliyowakutanisha nchi tano jijini Dar es Salaam, Msimamizi wa Kanda wa mradi huo wa Aga Khan, Kennedy Chande amesema wamegundua uwepo wa watu katika jamii wanaojihusisha kuwafundisha watoto tabia wasizozitaka waitwao makungwi.

“Tunashughulika na suala la ukeketaji pia tukaona makungwi wanachangia watoto kulazimishwa kufanya mambo wasiyoyapenda ambapo baadaye yanawaathiri katika maisha yao.

“Baada ya hapo tukakaa nao tukawaeleza kazi hiyo inadhalilisha watoto wakike na mwisho wa siku wakakubali. Ndipo tukaunda mradi mfano kwa upande wa mkoani Mtwara tukawawezesha kuanzisha biashara sasa wanajipatia kipato kwa njia nyingine na kuachana na kazi hiyo,” amebainisha.

Amesema katika mradi huo tathmini inaendelea kufanyika huku hadi sasa wameshaona wanawake na wasichana wanajiamini ikiwemo kuanzia katika uongozi, shughuli za kiuchumi kama maamuzi katika kilimo.

Amesema changamoto katika eneo hilo zinazomkandamiza mwanamke ni nyingi ikiwemo kutojiamini kutokana na mfumo wa jamii, tamaduni, jamii kuona mtoto wa kiume ni bora kuliko wa kike pamoja na sera.

“Sasa kuna ujasiri kuanzia kuongea mbele za watu, kuongoza na hata kufanya maamuzi katika sekta ya uchumi ikiwemo kilimo,” ametaja matokeo ya mradi huo. 

Aidha katika warsha hiyo ya mafunzo ya kikanda ijulikanayo kama AGECS, imewakutanisha wataalamu wa maendeleo, watunga sera, na wadau wakuu kutoka nchi tano barani Afrika kwa lengo la kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake. 

Alfred Okuonzi kutoka Uganda amesema juhudi mbalimbali zinaendelea ikiwemo kuwawezesha kiuchumi ushirikishwaji wa kifedha wa wanawake na wasichana, hasa kujenga uwezo wao katika ujuzi wa kifedha ambapo vyama vya Akiba na Mikopo vya vijiji vilifunguliwa.

“Sasa hivi katika baadhi ya familia mama ndio anawezesha mlo na maisha yanaenda kwa ujumla, wakati zamani walikuwa wanajulikana kama walinzi wa nyumba tu” amesema.

“Nchini Uganda, wanawake hawangoji wanaume.  Hata kama wanaume hawapo, chakula bado kipo mezani ili wanafamilia wale, na wanaume hufika jioni na kukuta chakula kikiwa tayari mezani kinawasubiri,” amesema Okuonzi.

Naibu Katibu Mkuu Maendeleo ya Jinsia na Wanawake, Felister Mdemu amesema ni furaha kujadili usawa huku nchi za Madagascar, Msumbiji, Kenya, Tanzania, na Uganda zikikutana hapa nchini.

“Nimeelezwa kuwa mkutano huu ni warsha ya kujifunza iliyopangwa chini ya mpango wa Kuendeleza Usawa wa Kijinsia Kupitia Asasi za Kiraia, mpango wa nchi nyingi ambao umetumia mbinu bunifu kushughulikia ukosefu wa usawa wa kijinsia katika ngazi mbalimbali.

“Tunapongeza Aga Khan Foundation kwa kuandaa warsha hii inayotoa fursa muhimu kwa wadau kujifunza juu ya mbinu zinazofanya kazi na zile zisizofanya kazi.

Amesema Serikali itaendelea kuwa mtetezi wa haki za kijinsia na haki za wanawake na wasichana inatambua kuwa usawa wa kijinsia si suala la haki za binadamu pekee, bali ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi, utulivu wa kijamii, na maendeleo ya taifa.

“Kama nchi, tunatambua kuwa maendeleo ni maendeleo pale tunapotembea pamoja na kila mtu anapopewa nafasi na fursa sawa ya kufanikiwa jambo linaloendana na kauli mbiu ya ‘Kumwacha Mtu Nyuma Haikubaliki’.

Vilevile, Serikali inaendana na juhudi za kimataifa kama Azimio la Mkutano wa Dunia wa 2005 juu ya Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake. Ndani ya nchi, sera kama ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000), Azimio la SADC juu ya Jinsia na Maendeleo (1999), na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) (1998) zinatekelezwa kikamilifu ili kuimarisha dhamira hizi.

Serikali ya Tanzania pia imepitisha mikakati kama Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ambayo sasa inakaguliwa upya, ikiwa na dhamira ya kufanikisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika nyanja zote za jamii ifikapo mwaka 2025.

Serikali imeanzisha sera na sheria zinazolenga matumizi bora ya rasilimali za ardhi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Sera ya Taifa ya Ardhi ya 1997 inahimiza usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi, huku Sheria ya Ardhi ya 2004 ikiruhusu ardhi kuwa dhamana kwa mikopo kwa ridhaa ya wenza, hivyo kuwawezesha wanawake kupata mikopo ya benki na kujitegemea kifedha.

Pia, juhudi mbalimbali za kuendeleza usawa wa kijinsia zinafanyika hivi sasa ikiwemo: Elimu bure na ya lazima kwa mtazamo wa kijinsia ili kuhakikisha ujumuishi. Utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

Kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Ujenzi wa miundombinu ya shule na ajira kwa walimu. Kuwezesha jamii zote kupata maji safi kupitia mpango wa Mtue Ndoo Mama.

Uanzishwaji wa Wizara maalumh inayohusika na maendeleo ya jinsia na uundaji wa Madawati ya Jinsia katika ngazi za serikali. Kuendeleza ushiriki wa wanawake katika uongozi na maamuzi.

Amesema kila mafanikio tunayopata katika kuwaendeleza wanawake na wasichana ni mafanikio kwa taifa zima. Kuwawezesha wanawake siyo tu jambo sahihi kufanya, bali pia ni jambo la busara.

Related Posts